Picha ya pamoja ========================================================
Tanzania yashinda kwa mara ya pili Tuzo ya Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India.
Tanzania imeibuka
mshindi wa kwanza wa Banda Bora katika maonesho ya Kimataifa ya Utalii yajulikanayo
kama Outbound Travel Mart 2020 (OTM 2020)
yaliyofanyika nchini India hivi karibuni.
Ubalozi wa Tanzania,
New Delhi, Taasisi za Serikali na kampuni binafsi mbalimbali za utalii nchini
zimeshiriki Maonesho hayo kwa lengo la kutangaza na kutafuta fursa mpya za soko
la utalii nchini humo.
Maonesho hayo maarufu
na makubwa katika ukanda wa Asia na Pasifiki ambayo hufanyika kila mwaka jijini
Mumbai na kuzishirikisha taasisi mbalimbali za utalii duniani, yamefanyika
kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari, 2020.
Wakati wa maonesho hayo, Banda la Tanzania
limeibuka tena Mshindi wa Kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu
na kuvutia watu wengi (The winner of Best Decoration Award). Tanzania imeshinda
tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo ambapo katika maonesho ya mwaka 2019,
Tanzania pia ilishinda tuzo hiyo.
Akizungumzia maonesho
hayo, Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda amesema kuwa maonesho
hayo ni fursa nyingine adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii ambapo
wafanyabiashara wapatao 15,000 wanaojishughulisha na masuala ya utalii
walishiriki kutoka katika mataifa zaidi ya 50 duniani. Aidha alisema kuwa, Washiriki
wamepata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya
biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na
kufanya biashara.
Kadhalika,
Balozi Luvanda ameeleza kuwa, maonesho yalisaidia washiriki wa Tanzania
kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua
soko la utalii nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu
vivutio vilivyopo nchini na faida zake.
“Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote
walioshiriki katika Banda letu la Tanzania la Maonesho kwa kazi nzuri ya
kutangaza vivutio vya utalii nchini iliyowezesha tupate ushindi mwingine katika
maonesho haya kwa mara ya pili kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu
na kuvutia watu wengi (The winner of Best Decoration Award)”, alisema
Balozi Luvanda.
Kwa
ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Idadi ya watalii kutoka India
wanaokwenda Tanzania sasa imeongezeka mara dufu baada ya kuanza kwa safari za
ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) moja kwa moja kutoka
Tanzania kuja India na katika hilo alitoa wito kwa wafanyabiashara hao kuendelea kutumia
fursa hiyo kuongeza idadi ya watalii wa India kutembelea Tanzania.
Taasisi za Serikali ya
Tanzania zilizoshiriki ni pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya
Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika
la Ndege la Tanzania (Air Tanzania). Kampuni binafsi zilizoshiriki ni pamoja na
Zara Tours, Mount Meru Hotel na Nature’s Land Safaris & Rentals.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.