Mhe. Balozi Shelukindo (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya Wajumbe kutoka UNESCO wakiangalia machapisho mbalimbali ya Lugha ya Kiswahili yaliyoandaliwa na Ubalozi baada ya kushiriki mjadala kuhusu Lugha ya Kiswahili ulioandaliwa na Ubalozi kwa kushirikiana na UNESCO. ===========================================================================
UNESCO YATAMBUA
KISWAHILI KAMA LUGHA ITAKAYOSAIDIA KUKUZA UTANGAMANO BARANI AFRIKA
Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeitambua Lugha ya Kiswahili
kama lugha itakayosaidia kukuza utangamano Barani Afrika wakati wa kuadhimisha Siku
ya Kimataifa ya Lugha Mama yenye kaulimbiu “Lugha Bila Mipaka” iliyofanyika
jijini Paris, Ufaransa hivi karibuni.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Ubalozi wa Tanzania nchini
Ufaransa kwa kushirikiana na UNESCO uliandaa mjadala kuhusu "Fursa na
Changamoto za Kukitambua Kiswahili kama Lugha rasmi ya Bara la Afrika kwa ajili
ya kukuza Utangamano".
Akizungumza wakati wa Mjadala huo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na
Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Mhe. Samwel Shelukindo pamoja na mambo
mengine, alieleza hatua iliyochukuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC) chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukifanya Kiswahili kuwa moja ya
lugha zitakazotumika katika Jumuiya hiyo.
Aidha, Mhe. Balozi Shelukindo alizipongeza nchi za Afrika Kusini na Namibia kwa kuwa nchi za kwanza
Kusini mwa Afrika zilizoamua kuanzisha ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili
katika shule mbalimbali. Mjadala huo uliwashirikisha Wataalam mbalimbali
akiwemo Prof. Aldin Mutembei kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Kufanyika kwa mjadala huo katika UNESCO ni moja ya juhudi zinazofanywa na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kupitia Ubalozi
wa Tanzania nchini Ufaransa za kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha
zitakazotumika katika UNESCO.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.