Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Tanzania, Bi. Mara Marwick ameihakikishia
Serikali ya Tanzania ushirikiano katika sekta mbalimbali ili kufikia maendeleo
yaliyokusudiwa.
Bi.
Marwick ameyasema hayo leo tarehe 5
Februari 2020 alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi katika
Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es Salaam.
Bi. Marwick amesema uhususiano baina ya benki
hiyo na Tanzania ni mzuri na kwamba Benki ya Dunia inathamini uhusiano huo wa
tangu miaka ya 1960 hadi leo na iko tayari kuendelea kuunga mkono kwa njia ya
ufadhili au mikopo miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
"Tuna
uhusiano mzuri katika miradi na uwekezaji ambapo tunaiwezesha serikali katika
maeneo mbalimbali. Pia tunafanya kazi pamoja katika masuala muhimu kama vile
uchambuzi wa sera za maendeleo hii inaashiria kuwa Benki ya Dunia itaendeleza
ushirikiano huu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na mahusiano imara
pamoja na maendeleo endelevu," Amesema Bi. Marwick.
Ameongeza
kuwa katika mazungumzo hayo, wamejadili masuala muhimu kuhusu maendeleo ya
Tanzania hususani elimu, miradi ya miundombinu, uchumi wa viwanda, pamoja na
maendeleo ya wananchi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema Tanzania itaendeleza mahusiano na Benki ya
Dunia na kuwataka watanzania kupuuza uzushi na uvumi unaosambazwa katika
mitandao ya kijamii kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Benki hiyo na badala
yake wasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Serikali na Benki ya dunia.
"Uhusiano
kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni imara na unaendelea vizuri, na Mkurugenzi
wa Benki ya Dunia ametuhakikishia kwamba katika kipindi hiki ambacho yeye ni
mkurugenzi hapa atauendeleza uhusiano huo huo. Mengi yanasemwa lakini mengi
hayana ukweli na wakati mwingine si busara kwa kila yanayosemwa kuyajibu
kwasababu yanaweza kuwaondoa kwenye shughuli za msingi na mkajikuta kila siku
mnajibu uvumi au uzushi katika mitandao ya kijamii na mambo mengine,"
Amesema Prof. Kabudi.
Prof.
Kabudi ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo pia wamegusia miradi ya kimkakati
ambayo Tanzania inaitekeleza, mingine kwa fedha za ndani au kwa kupata mkopo kutoka
Benki ya Dunia.
"Tumezungumza
kwa kirefu kuhusu mashirikiano katika elimu hasa elimu ya wasichana na kukuza
rasilimali watu na kutaja maeneo mengine ya mashirikiano ambayo ni pamoja na sekta za miundombinu, afya, maji na nishati,"
Ameongeza Prof. Kabudi.
Prof.
Kabudi ameongeza kuwa Tanzania inakopesheka kwenye benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo
ya Afrika, Benki ya Afrika Mashariki ya Maendeleo na taasisi nyingi sana za
kifedha na daima Serikali huhakikisha kuwa vigezo vyote vinavyotakiwa
vinasimamiwa lakini kikubwa hulipa madeni iliyokopa na ndiyo maana inaaminiwa
na kukopeshwa zaidi na fedha yote inayokopwa hupelekwa kwenye miradi ya msingi
ya kulifanya taifa kujitegemea lenyewe katika miaka michache ijayo.
Katika
tukio jingiene, Waziri kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu
Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stegomena Taxi
na kujalidiana nae mambo mbalimbali kuhusu SADC.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Marwick wakati
Bi. Marwack alipomtembelea Waziri katika ofisi ndogo za Wizara leo jijini Dar
es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.