Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara
mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima
(Pravasi Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind. Tuzo
hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India (15th
Pravasi Bharatiya Divas 2019) uliofanyika kwenye mji wa Varanasi, Uttar
Pradesh tarehe 23 Januari, 2019.
Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa India, Mhe.
Narendra Modi uliwahusisha viongozi mbalimbali wa ndani na
nje ya India akiwemo Waziri Mkuu wa
Mauritania, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Sushma Swaraj,
Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje ya India, Mhe. Gen
[Dr.) V. K. Singh na Waziri Kiongozi wa Jimbo la Utter Pradesh, Mhe. Yogi
Adityanath.
Mama Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango
wake mkubwa kwa jamii hususan katika masuala ya akina mama na kudumisha amani
na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini.
Wakati akimtunuku tuzo hiyo, Rais Kovind alieleza kutambua
mchango mkubwa wa Mama Shamim Khan katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo
baina ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na
Serikali ya Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi
baina ya nchi zao. Aidha, alimpongeza kwa utumishi uliotukuka.
Kwa upande wake, Mama Shamim Khan alimshukuru sana Rais Kovind
na kueleza kufarijika kwake kwa kutunukiwa Tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa
kwake. Aidha, Mama Shamim Khan alipongeza juhudi za Serikali ya India kwa
kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina ya
Tanzania na India na amemuomba Mhe. Rais Kovind kuendelea kusaidia juhudi za
Serikali ya Mhe.Rais Dkt. John P. Magufuli katika kuwaletea maendeleo
watanzania.
Tuzo hiyo hutolewa
kwa raia wenye asili ya India ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo
ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India. Hivyo hii imekuwa
ni heshima kubwa sio tu kwa Mama Shamim Khan bali kwa Tanzania kwa ujumla.
Mama Shamim Khan aliongozana na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dkt.
Kheri Goloka kwenye hafla hiyo.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.