TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kuwahudumia Wakimbizi ni jukumu la Wote sio la Nchi moja
Kazi ya kuwahudumia wakimbizi
ni Ubinadamu na ni jukumu la kimataifa na ni kitu cha kushangaza kuona nchi
zilizoendelea zinaziachia nchi masikini kubeba mzigo wa kugharamia wakimbizi.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais
Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti
mwenza wa Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council-WRC), Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete wakati wa kuwasilisha ripoti ya Baraza hilo kwenye Umoja wa
Mataifa New York, Marekani tarehe 24 Januari 2019.
Rais Mstaafu alitanabainisha kwamba
Baraza lao lilipokea msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kukataa
mpango wa kukopa Benki ya Dunia ili kuwahudumia wakimbizi wakati yenyewe
inadaiwa mikopo ya kimaendeleo iliyonayo. Serikali inaamini kazi ya kuhudumia
wakimbizi ni ya kibinadamu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa badala ya
kuibebesha nchi moja mzigo wa madeni.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa
tatizo la wakimbizi limekuwa kubwa sana duniani wakati huu kuliko wakati wowote
ule tangu vita vya Pili vya Dunia.
Mathalan, kuna idadi ya watu milioni 68.5 waliopoteza makwao (Internally
displaced persons) mwaka 2017 na kati yao, milioni tatu wamepoteza makwao kwa
sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na uchafuzi wa mazingira.
Ripoti inaeleza kuwa, kumekuwa
na ongezeko kubwa la wakimbizi na wanaopoteza makwao kusini mwa jangwa la Sahara
ambao walifikia milioni 18.4 mwaka 2017 ukilinganisha na idadi ya milioni 14.1
mwaka 2015.
Ripoti inabainisha kuwa ongezeko
hilo limetokana na sababu mbalimbali zikwemo upvotevu wa amani katika nchi zao.
Ripoti inazidi kubainisha kuwa asilimia 30 ya
watu wote duniani mwaka 2017 walikuwa wakimbizi na waliopoteza makwao ukilinganisha
na asilimia 23 ya mwaka 2015. Kati ya idadi hiyo, wanaotoka Afrika, asilimia
79% wanatoka katika nchi za Somalia, Nigeria, Sudan kusini na Jamhuri ya Afrika
ya Kati.
Ripoti imeeleza nchi zinazopokea
wakimbizi wengi kuwa ni pamoja na Uganda, wakimbizi milioni moja na laki nne; Ethiopia,
laki Tisa; Tanzania laki tatu na ishirini na Sita elfu; na Rwanda elfu 84. Baadhi ya nchi zimechukua wakimbizi hao
ikiwemo Marekani, Canada, Australia na Finland ingawa idadi yao ni ndogo mno.
Katika ripoti hiyo, baraza
limetoa mependekezo mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani. Mapendekezo makubwa ni pamoja na kudhibiti
nchi ambazo zinachochea au kuanzisha migogoro kwa kuweka mfumo thabiti wa
kimataifa, kuongeza usuluhishi wa migogoro, kutowanyanyapaa wakimbizi kwa
kujenga ukuta na kusaidia juhudi za kutafuta amani katika maeneo yenye migogoro.
Baraza la Wakimbizi duniani
ni chombo kilichoundwa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, watafiti na
watunga sera kwa lengo la kufanya utafiti wa kina utakaosaidia kubuni njia na
mbinu za kitaalamu na za ubunifu zitakazosaidia kukabiliana na kumaliza kabisa
tatizo la wakimbizi duniani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Dodoma
27 Januari 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.