Thursday, February 19, 2026

TANZANIA NA MSUMBIJI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA AFYA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kulia) akiwa  na Balozi wa Msumbiji nchini  Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida (Kushoto).


Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msumbiji zimeeleza dhamira ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili katika maeneo ya kimkakati, ikiwemo Sekta ya Afya ili kuleta maendeleo ya wananchi wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Balozi wa Msumbiji nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida, wameeleza dhamira hiyo walipokutana na kufanya mazungumzo tarehe 18 Februari, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalilenga kubainisha maeneo ya ushirikiano zaidi kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kuongeza ushirikiano katika Sekta ya afya, kukuza uchumi, na kujadili maandalizi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka huu.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Kombo pia amewakaribisha wananchi wa Msumbiji kunufaika na huduma za Afya za kibingwa na kibobezi zinazopatikana nchini ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Msumbiji.

Naye Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Ricardo Mtumbuida, ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano wa kindugu unaoendelea kuipatia nchi yake, na kusisitiza azma ya Msumbiji ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania ili kukuza ustawi wa wananchi wa mataifa yote mawili


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo 


Balozi wa Msumbiji nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kulia) akiwa  na Balozi wa Msumbiji nchini  Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida (Kushoto) wakati mazungumzo yakiendelea kwenye Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar-es-Salaam.

















No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.