Kamati ya Kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Kurekebisha Mifumo ya Haki Jinai nchini imekutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaowakilisha nchi na taasisi zao nchini.
Kamati hiyo imewahakikishia Mabalozi na wawakilishi hao kuwa baadhi ya mapendekezo yameanza kufanyiwa kazi na Serikali.
Akizungumza na mabalozi na wawakilishi hao kuwapa mrejesho wa taarifa ya tume ya kuboresha muundo wa taasisi za haki jinai Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Kurekebisha Mifumo ya Haki Jinai, Jaji Mstaafu Mhe. Othman Chande amesema Serikali imeanza kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa na tume hiyo.
Amesema baadhi ya mapendekezo yaliyoanza kutekelezwa ni pamoja na kufunguliwa kwa Ofisi 50 za Mkurugenzi wa Mashitaka katika ngazi ya wilaya nchini ili kusaidia upatikanaji wa haki nchini ikiwa ni moja ya mapendekezo ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.
Amesema kufunguliwa kwa ofisi hizo za mashitaka katika wilaya 50 nchini ni jambo lililopendekezwa na tume tangu awali.
Mhe. Jaji Mustafa Chande alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda tume hiyo mwezi Januari 2023 ikiwa na wajumbe tisa na kuipa kazi ya kupitia na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa taasisi za haki jinai nchini kazi iliyokamilika na kuwasilishwa mwezi Julai 2023.
Aliongeza kuwa baada ya kupokea mapendekezo zaidi ya 360 ya tume hiyo yaliyolenga kuboresha taasisi za haki jinai, aliibadilisha tume hiyo na kuwa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa mapendekezo hayo na kusaidia Serikali kuandaa mpango wa utekelezaji wa mapendekezo hayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Kiongozi wa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Balozi wa Visiwa vya Comoro, Dkt. Ahamada El Badaoui alisema kazi iliyofanywa na tume ni njema na wao kama mabalozi wanaunga mkono juhudi za serikali katika kutoa haki na kuahidi kuendelea kutoa mchango wao wa ushirikiano na Tanzania.
Naye Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa ameipongeza Kamati kwa kufanya kazi ndani ya muda mfupi na kuja na mapendekezo ambayo ni mazuri na kusema Tanzania ikiyatekeleza itapiga hatua zaidi na kusema Nigeria wana cha kujifunza kupitia tume hiyo.
“Tumefarijika na taarifa hii, kwa kweli Nigeria tutakuja kuiga mfano huu wa kutekeleza haki jinai hapa Tanzania,” Alisema Balozi Takamawa
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Bi. Shalini Bahuguna ameipongeza tume kwa kuweka mapendekezo ya kuboresha haki za mtoto na kueleza kuwa UNICEF ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kuimarishwa zaidi.
Sehemu ya Mabalozi wakifuatilia kikao |
Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Tri Yogo Jatmiko akichangia jambo wakati wa Mabalozi wakipatiwa taarifa ya tume ya kuboresha muundo wa taasisi za haki jinai Jijini Dar es Salaam |
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akizungumza kwenye kikao hicho |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.