Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameitaja ziara ya Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis ni ya kihistoria na ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Taifa hilo kutembelea nchini na imesaidia kuimarisha ushirikiano katika maeneno ya kimkakati.
Rais samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Novemba 2023 Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu waliyokubaliana na mgeni wake.
Rais Samia ameeleza kuwa katika mazungumzo na mgeni wake wamekubaliana kuwa mataifa yao yataimarisha ushirikiano katika sekta za afya, hususan utengenezaji wa dawa, usindikaji wa mazao ya kilimo, madini pamoja na mbinu za kukabiliana na majanga.
Maeneo mengine ya ushirikiano ambayo viongozi hao wamedhamiria kuyapa kipaumbele ni ufadhili wa masomo ambapo Romania itatoa nafasi 10 kwa ajili ya watanzania kusoma masomo ya udaktari na ufamasia katika mwaka huu wa masomo. Aidha, Tanzania imetoa nafasi tano za masomo kwa wanafunzi wa Romania kuja kusoma nchini katika vyuo watakavyochagua wenyewe.
Rais samia aliongeza kuwa nchi hizo zimedhamiria kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji ambacho kwa sasa hakiridhishi licha ya nchi zao kuwa na fursa lukuki za uwekezaji.
Viongozi hao pia waliokubaliana kushirikiana katika masuala ya kimataifa na hasa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo itajadiliwa kwa kina katika mkutano wa COP28 uliopangwa kufanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwezi Novemba 2023.
Rais Samia alihitimisha maelezo yake kwa kueleza kuwa Mheshimiwa Iohannis na ujumbe wake watatembelea Zanzibar kuzungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 18 Novemba, 2023. Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano hususan uchumi wa buluu na utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa Zanzibar.
Naye Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis amesema Romania imekuwa na ushirikiano mzuri na imara wakati wote, na lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kuimarisha zaidi uhusiano baina ya mataifa hayo.
Tumekuwa na uhusiano mzuri na imara wakati wote, na katika kuendelea kuimarisha uhusianoi wetu tumekubaliana kuimarisha uhusianio wetu kwenye maeneo ya kimkakati na Tanzania katika sekta za kilimo, ulinzi wa raia, ulinzi wa kimtandao, teknolojia na uchumi,” alisema Rais Iohannis
“kusainiwa na hati hizi mbili za makubaliano ya ushirikiano ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wetu,” aliongeza Rais Iohannis
Pamoja na mambo mengine, Rais Iohannis amesema kuwa Romania itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mambo waliyokubaliana kwa maslahi ya mapana ya pande zote mbili.
Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.