Saturday, November 18, 2023

RAIS DKT. MWINYI AWAKARIBISHA WAROMANIA KUWEKEZA ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis Ikulu Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezikaribisha kampuni za Romania kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta za Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Novemba 18, 2023 Ikulu Zanzibar wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa ziara ya Rais Iohannis ni heshima kubwa kwa Zanzibar na imedhihirisha kuwa licha ya nchi hizo mbili kuwa mbali kijiografia lakini zinaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi mapana ya pande zote mbili. 

Aidha, Rais Mwinyi alitoa wito kwa watu wa Romania kuja Zanzibar, kisiwa kilichojaliwa vivutio vingi vya utalii na vinavyovutia.

Alimuhakikishia Rais Iohannis ambaye amepanga kutembelea Mji Mkongwe kuwa hatajutia uamuzi wake kwani atafurahia historia na mandhari nzuri ya Mji huo.

Kwa upande wake, Rais wa Romania alifurahishwa na dira ya Maendeleo ya Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na Zanzibar ili kufanikisha utekelezaji wa Dira hiyo. Amesema ziara yake ni moja ya jitihada za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Romania na Tanzania ambao mwezi Mei 2024 utafikisha miaka 60 tangu ulipoanzishwa mwaka 1964.

Rais Iohannis atamaliza ziara yake nchini Novemba 19, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, wakati wa ziara hiyo imeshuhudiwa uwekaji saini wa Hati za Makubaliano kuhusu kushirikiana katika masuala ya utafiti wa kisayansi katika kilimo na usalama wa chakula pamoja na kukabiliana na majanga

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis Ikulu Zanzibar

Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis Ikulu Zanzibar
Rais wa Romania, Mhe. Klaus Iohannis akizungumza kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima yake Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.