Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano, kutoka kulia ni Bw. Hangi Mgaka, Bw. Odilo Fidelis na Bw. Fred Maro. |
Mkutano ukiendelea |
=======================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU TAARIFA ZA
KUTESWA KWA WATANZANIA WANAOKWENDA KUFANYA KAZI OMAN NA NCHI NYINGINE ZA
MASHARIKI YA KATI
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
inachukua fursa hii leo kupeleka taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari juu
ya habari zilizochapishwa katika gazeti moja kuhusu mateso wanayopata Watanzania
wanaofanya kazi za ndani nchini Oman ili kuondoa utata uliojitokeza kutokana na habari
hiyo. Aidha, Wizara inapenda kutoa uelewa na ufafanuzi ili kupata
ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kukabiliana na changamoto wanazopata
Watanzania nje ya nchi wakitafuta maslahi ya kiuchumi.
Ndugu Wanahabari,
Jana siku ya Jumanne tarehe 4 Oktoba 2016, Gazeti la
Tanzania Mpya katika toleo lake Na.23 katika ukurasa wake wa mbele lilichapisha
habari yenye kichwa cha maneno watanzania wateswa nchini Oman na kuwa wengine
hunyofolewa figo zao na kupewa ndugu wa waajiri wenye mahitaji. Habari hii
ambayo imeendelea ukurasa wa pili na watano imeambatana na picha ya Mheshimiwa
Dr. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
na hivyo kuwafanya wasomaji wengi kuamini kuwa taarifa ile imetolewa na
Mheshimiwa Waziri.
Kitendo hiki cha kuchapisha habari hii na kutumia picha ya
Mheshimiwa Waziri kimeleta usumbufu kwa mheshimiwa Waziri na pia kwa wasomaji kwani
wengi wameamini kuwa taarifa ile imetolewa na Mhe. Waziri.
Wizara inapenda kuutangazia umma kwa ujumla kwamba
Mheshimiwa Dr. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki hausiki na taarifa hiyo
na wala hakuwahi kuzungumza na mwandishi wa habari wa makala husika na kuwa
yaliyomo kwenye taarifa hiyo ni maoni binafsi ya mwandishi na gazeti husika na
kwa vyovyote vile hayawakilishi msimamo wa Mheshimiwa Waziri na Wizara
anayoiongoza na serikali kwa ujumla.
Habari hii ni mfululizo wa uchapishaji wa habari zenye
maudhui kama haya kwenye baadhi ya magazeti na mitandao ya kijamii ambazo
hazijafanyiwa utafiti wa kina na kuwa na taarifa sahihi kuhusu mada husika. Taarifa
hizi zinaweza kuharibu uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na
Oman kati ya serikali na serikali na pia watu wake ambao wengi wana uhusiano wa
damu
Ndugu Wanahabari,
Baada ya kusema hayo sasa naomba kutoa taarifa ya kina
kuhusu suala zima la watanzania wanaokwenda kufanya kazi nchini Oman na nchi nyingine
za mashariki ya kati na utaratibu ambao serikali imeweka katika kuratibu zoezi
zima
Eneo la mashariki ya kati linaundwa na nchi za Oman ,
Saudi Arabia, Qatar, Bahrain, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu ( Abu Dhabi,
Dubai, Ajman, Al Ain, Fujairah, Ras Al Khaimah na Sharjah), Lebanon, Syria,
Iran, Iraq, Yemen.
Nchi hizi kwa kiasi kikubwa ni tegemezi ya nguvu kazi
kutoka nje ya eneo hili na hivyo kuwa soko kubwa la ajira kwa nchi mbalimbali,
ajira hizi ni kuanzia watendaji wakuu, watendaji wa ngazi mbalimbali hadi
wahudumu na watumishi wa majumbani
Kati ya nchi za mashariki ya kati Oman imekuwa na uhusiano
wa karibu sana ambao ni wa kihistoria na kidamu, ambapo nusu ya familia za Oman
asili yake ni Tanzania na hivyo kufanya kuwa na muingiliano wa karibu.
Kwa kuzingatia uhusiano huu Oman imekuwa ikipokea
wafanyakazi mbalimbali kutoka Tanzania katika kada za madaktari, walimu,
wauguzi, wahadhiri, wapishi, wahudumu katika masaluni ( nywele na kuchora
Heena), madereva, wahudumu wa mashamba na bustani na watumishi wa nyumbani.
Kuanzia miaka ya 2010 wimbi la watanzania kwenda kufanya
kazi Oman lilishika kasi na hivyo kuongeza idadi ya watanzania wanaoingia Oman
kwa ajili ya kufanyakazi mbalimbali hasa majumbani ( Housemaids) , kufuatia
wimbi hili ubalozi ulianza kupokea watanzania wanaolalamikia mazingira magumu
ya kufanyia kazi, malalamiko yao yalihusu kufanya kazi masaa mengi, mshahara
mdogo, kukosa mapumziko, kutoruhusiwa kutoka nje ya nyumba, kufanya kazi zaidi
ya nyumba moja , kunyanyaswa kijinsia , kufanyishwa kazi ziadi ya kazi za Housemaid.
Katika mazungumzo na watumishi husika, ubalozi ulibaini
kutokuwepo kwa utaratibu maalum wa kuratibu ajira zao kuja Oman, hivyo basi
Ubalozi kwa kushirikiana na wadau wengine hapa Tanzania ( Uhamiaji, Wizara ya
Kazi, Wakala wa huduma za ajira Tanzania (TAESA) , Kamisheni ya kazi Zanzibar,
Mamlaka ya viwanja vya ndege, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa) vilianza
utekelezaji wa utaratibu wa kufuatwa kwa wale wanaokwenda kufanya kazi nje ya
nchi na hasa Oman.
Ndugu wanahabari
Chini ya utaratibu huu, Raia wa Oman mwenye nia ya
kumwajiri mtanazania anapaswa kwenda Ubalozini na kujaza fomu ya kuomba
kumwajiri mtanzania, baada ya fomu yake kuridhiwa na Ubalozi atapewa mkataba
ambao atajaza na kuurudisha Ubalozi akiambatanisha nakala ya kitambulisho chake
cha taifa, Uthibitisho wa makazi ( bili ya maji au umeme), nakala ya pasipoti
ya mfanya kazi, hati ya kiapo na dhamana ya rial 100 .
Baada ya Ubalozi kuridhika na vielelezo vyake, ubalozi
utapitisha mkataba na kumtaka mwajiri husika kuuwasilisha Tanzania kwa mtumishi
husika ambae ataupokea na kuuwasilisha TAESA au kamisheni ya kazi ambao nao watamuhoji
muhusika na kujiridhisha kuwa anaulewa wa kazi anayokwenda kufanya pamoja na
masharti yake, wakijiridhisha watampa kibali ambacho ni barua ikimuomba kamishna
wa uhamiaji amruhusu muhusika kusafiri nje ya nchi baada ya kutimiza utaratibu
uliowekwa.
Ndugu wanahabari
Utekelezaji wa utaratibu huu umekuwa na mafanikio na pia changamoto,
kwa kiasi kikubwa uratibu huu umeweza kupunguza matatizo waliyokuwa wanayapata
ndugu zetu, kuongeza mshahara wao, kuwapatia haki ya kupumzika na mawasiliano
na pia kuongeza uelewa wa watanzania juu ya haki zao na namna ya kuzipata pale
zinapokiukwa.
Kufuatia kufanikiwa kwa utekelezaji wa utaratibu huu
nchini Oman, serikali sasa imeanza kutumia utaratibu huu katika nchi yingine za
mashariki ya kati
Pamoja na mafanikio kumekuwa na changamoto kama vile
baadhi ya watu kukwepa kufuata utaratibu husika kwa kuwapitisha wahusika njia
za panya, kughushi nyaraka husika, kuwepo kwa mawakala bubu na kuwa na tamaa ya
kufanikiwa haraka, watanzania kutokuwa na ujuzi au uzoefu wa kazi wanayokwenda
kuifanya, kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa maadili kama vile wizi,
udanganyifu nk
Ndugu wanahabari
Ndugu wana habari, naomba nitumie nafasi hii pia kutoa
ufafanuzi kuhusu malalamiko ya kunyang’anywa hati za kusafiria, huu ni
utaratibu unaofuatwa na waajiri katika nchi zote za mashariki ya kati ambapo
katika kipindi chote cha mkataba hati ya kusafiria huwekwa chini ya uangalizi
wa mwajiri, utaratibu hufanyika kwa waajiri wa aina zote kwa maana ya taasisi (
Wizara, Idara, mashirika binafsi ) na watu binafsi, hivyo tunaomba ieleweke
kuwa ni suala la utaratibu
Ndugu wanahabari
Katika kupambana na changamoto hizi serikali imejipanga
kuimarisha udhibiti wa utekelezaji wa utaratibu huu kupitia vikao mbalimbali
vya wadau. Vikao hivyo viliazimia Kuandaa mtaala wa kuongeza stadi na ujuzi kwa wanaokusudia
kufanya kazi za Housemaid
Kuanza kutumia
mawakala rasmi wa ajira walioandikishwa na mamlaka husika
Kuwepo mkataba wa
ajira unaotambuliwa na Mamlaka za Nchi unayotaka kwenda. Kwa hapa nyumbani
mamlaka zinazoweza kusaidia ni pamoja na Ofisi za Ubalozi za Nchi husika,
Wakala wa Ajira Tanzania - TAESA (Tanzania Bara) au Kamisheni ya Kazi
(Zanzibar); Mtanzania asikubali kuanza safari bila kupata
mkataba na Kibali kutoka TAESA au Kamisheni ya Kazi.
kila Ubalozi katika nchi za Mashariki ya Kati
uandae mikataba ya kazi kutokana na muongozo uliokubaliwa na wadau
wote.
Vilevile, kupitia kwenu wanahabari, tunatoa wito
kwa watanzania wote, tuwe makini pale tunapopata fursa za kazi nje ya
nchi. Kama nilivyosema hapo awali, ni muhimu kujiridhisha kwamba mambo
yote ya msingi yanayohusiana na ajira hizo yamekaa sawa ikiwa ni pamoja na:
Kuzingatia na kufuata utaratibu
uliowekwa na serikali, na wala mtanzania asikubali kuambiwa kuwa mktaba ataukuta huko anakokwenda au kusafiri kupitia
nchi jirani kwenda kuanza kazi nje ya nchi,
wito kwa Taasisi zote zinazoratibu safari za
Nje katika viwanja vya ndege au vituo vya mipakani kuhakikisha hawamruhusu mtu
kusafiri nje kwa nia ya kufanya kazi bila kuwa na vibali husika.
Kutafuta msaada wa
kupata uthibitisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki au Wizara ya Kazi kama kweli kazi uliyoahidiwa ipo- Wizara yetu
itaweza kutumia Balozi zetu kuthibitisha;
Na pale unapokwenda
Nje, ni muhimu kuhakikisha kwamba unajisajili kweye ofisi za Ubalozi wa Tanzania
uliopo katika nchi hizo au ubalozi wa Uingereza mahali ambapo hakuna Ubalozi wa
Tanzania.
Kutokubali
kuweka hati yako ya kusaifiria kama rehani kwasababu yoyote ile;
Katika kupata suluhisho la kudumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia
Watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi, Wizara kwa kushirikiana na wadau
husika inaendelea na jitihada za kusaini Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta
ya Ajira na Kazi baina ya Serikali ya Tanzania na nchi hizo kama ule wa
Tanzania na Qatar. Kusainiwa kwa mikataba hiyo sio tu kutasaidia kupata fursa
za ajira katika nchi hizo bali kutailazimu Serikali ya nchi hizo kushirikiana
na Wizara pindi raia wao watapokwenda kinyume na mikataba ya ajira iliyopo.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
05 Oktoba 2016.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.