Monday, October 24, 2016

Waziri Mahiga ahimiza umuhimu wa somo la Umoja wa Mataifa

WAZIRI MAHIGA AHIMIZA UMUHIMU WA SOMO LA UMOJA WA MATAIFA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine mahiga amependekeza ni vema somo la Umoja wa Mataifa likaingizwa katika mitaala ya masomo, ameeleza hayo alipokuwa akihutubia  katika kilele cha Maadhimisho ya 71 ya Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo Waziri Mahiga alisema “Maadhimisho haya ni muhimu  kwa historia ya nchi yetu kwakua yanawezesha vizazi vyetu kuelewa historia ya nchi yetu na Shirika la Umoja wa Mataifa tangu kupatikana kwa Uhuru hivyo ni vyema Walimu na Wadau wote katika Sekta ya Elimu wakatilia mkazo umuhimu wa somo la Umoja wa Mataifa katika shule zetu za Msingi na Sekondari.”

Vilevile ameeleza umuhimu na mchango wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa Tanzania na  kwa nchi wanachama wengine wa Umoja huo ni pamoja na kutengeneza agenda ya kimataifa ya maendeleo; kuleta amani hususan baada ya vita ya kwanza na  ya pili ya Dunia; vilevile Shirika hilo limekuwa likiendelea kuhakikisha amani na Ulinzi inapatikana katika mataifa yenye migogoro ambapo Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekuwa zikishiriki katika masuala ya ulinzi wa amani katika baadhi ya mataifa kama Lebanon, Sudan Kusini (Dafur) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Pamoja na hayo ameeleza kuwa kupitia shirika la umoja wa Mataifa Tanzania imefanikiwa kuwa na  wawakilishi wa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa ambao pamoja na shughuli nyingine za mashirika hayo yamekuwa yakifadhili na kushiriki katika shughuli za maendeleo ambapo wastani wa bilioni za fedha za miradi ya maendeleo zimekuwa zikitolewa kwaajili ya miradi ya maendeleo. Vilevile Mahakama ya Umoja wa mataifa ya mauaji ya kimbari iliamuriwa kujengwa nchini Tanzania ambapo makao makuu yake yapo Jijini Arusha licha ya kumalizika kwa kesi majengo pamoja na nyaraka zote zilizokuwa zikitumika zimeendelea kubaki nchini kama kumbukumbu za marejeo.

Naye Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez alieleza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs), umuhimu wa kutunza amani na kuheshimu haki za binadamu sambamba na usawa wa jinsia.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa yanayowakilisha nchi zao hapa nchini. Wengine ni wadau wa maendeleo kutoka Sekta binafsi na taasisi za Serikali. 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.