Monday, October 24, 2016

Mfalme wa Morocco aendelea na ziara nchini

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 



Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
             11466 DAR  ES SALAAM, 
                                    Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MFALME WA MOROCCO AENDELEA NA ZIARA NCHINI

Mfalme wa Morocco, Mtukufu Mohammed VI aliyewasili jana kwa ziara ya kitaifa, ameendelea na ziara yake nchini ambapo leo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika kuboresha mahusiano ya Tanzania na Morocco katika maeneo mbalimbali ya Kidiplomasia, Siasa, Uchumi, Ulinzi na Ustawi wa Jamii.

Akielezea mahusiano ya Tanzania na Morocco, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alisema kuwa ziara hii ni matokeo ya  Mhe. Rais kuridhia ujio huo wa Mfalme wa Morocco na ujio wake umekuwa ni maalum sana kwa kuwa unakumbushia historia iliyowekwa na mgeni wa kwanza kutoka Morocco, Bw. Iban Batutu aliyetembelea Tanzania eneo la Kilwa Mwaka 1631.

Baada ya mazungumzo,  Mhe. Rais Magufuli na Mgeni wake, Mtukufu Mfalme wa Morocco walishuhudia uwekaji saini wa Mikataba 22 ambayo inalenga kuendeleza sekta mbalimbali kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco.

Baadhi ya Mikataba hiyo ni Makubaliano baina ya Benki ya Kilimo ya Tanzania na Benki ya Kilimo ya Morocco  ili kuwawezesha wakulima wetu kusindika mazao yao na kuyasafarisha nje yakiwa yamekamilika, Makubaliano baina ya Kampuni ya Mbolea ya Morocco na ya Tanzania ambapo kwa pamoja zitabadilishana uzoefu na utaalamu kwa lengo la kuiwezesha kampuni ya Tanzania kuzalisha mbolea ya kutosha kulingana na mahitaji, Makubaliano katika Sekta ya Anga ambapo katika siku za usoni Shirika la Ndege la Morocco litaanzisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Rabat hadi Dar es Salaam.

 Makubaliano mengine ni pamoja na kusaidia wakulima wadogo wadogo, kuendeleza Sekta ya Utalii ya Tanzania hususan katika fukwe za Zanzibar na hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro, makubaliano  baina ya Shirika la reli la Tanzania na lile la Morocco ambapo watashirikiana  kuboresha usafiri  wa reli kwa madhumuni ya kupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kuendeleza reli ya Mtwara-Mchuchuma/Liganga.

Viongozi hao pia walishuhudia uwekaji saini ya Mkataba baina ya Kampuni ya chai ya Tanzania na ile ya Morocco kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kutengeneza chai yenye ubora wa hali ya juu ili iweze kupata soko nchini Morocco na nchi nyingine.

Aidha, akiongea katika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Bw. Salahddine Mezouar amesema wakati sasa umefika nchi hizi kupeleka mbele mahusiano yao na hii ndio sababu kubwa iliyopelekea nchi hizi mbili kukubaliana kusaini jumla ya mikataba 22, amesema nchi ya Morocco imefurahishwa na utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuri.

Mtukufu Mfalme atahitimisha ratiba yake kwa siku ya leo kwa kushiriki dhifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli  Ikulu, Dar es Salaam.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 24 Septemba 2016

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.