Saturday, February 4, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


JPCC kati ya Tanzania na Malawi ni chachu ya kuimarisha mahusiano

Wajumbe wanaoshiriki katika Kikao cha 4 cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya  Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi kilichofunguliwa leo jijini Lilongwe, Malawi wamehimizwa katika majadiliano yao ya  siku tatu  kubuni mkakati utakaowezesha kutatua changamoto zinazojitokeza kutokana na muingiliano mkubwa wa ngazi mbalimbali za ushirikiano baina ya wananchi  wa  mataifa hayo mawili.

 Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Wataalam, Balozi Ramadhan Mwinyi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa anasoma hotuba ya ufunguzi.

"Kama mnavyofahamu kunapokuwa na maingiliano makubwa ya wananchi wa nchi mbili kama zilivyo nchi zetu, changamoto haziwezi kukosa kujitokeza. Hivyo ni jukumu letu sisi wataalamu kubuni mkakati wa kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinashughulikiwa haraka iwezekanavyo".

Balozi Mwinyi alieleza kuwa kikao hicho ni fursa nzuri kwa Serikali za Tanzania na Malawi kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi zao katika maeneo tofauti ikiwemo uchumi, uwekezaji, biashara, kutunza mazingira, elimu, Tehama, kilimo, uhamiaji, uchukuzi na masuala ya ulinzi na usalama, Hivyo alihimiza wajumbe wa pande zote mbili kuwa wabunifu katika majadiliano yao ili watoke na mipango inayotekelezeka kwa kuwa wananchi wanachohitaji ni maendeleo na sio mikakati inayoishia katika makabrasha.

Aidha, Balozi Mwinyi aliekeza kuwa watu wengi walistaajabu kusikia ujumbe wa Tanzania unakuja Malawi kushiriki kikao hiki kama walivyostaajabu kuona Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya mazungumzo hivi karibuni na Rais wa Malawi, Mhe. Prof. Peter Mutharika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia. Alisema hakuna cha kustaajabisha hapo, isipokuwa ifahamike lengo kuu la pande zote mbili ni kuona uhusiano kati ya Tanzania na Malawi unaimarishwa na kwamba mkutano huo ni ushahidi kuwa nchi hizi mbili zipo karibu zaidi kuliko hapo awali.

Naibu Katibu Mkuu aliihakikishia Serikali ya Malawi kuwa Serikali ya Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi hiyo katika kuboresha mahusiano ya kidiplomasia, uchumi na kijamii, hivyo alisisitiza umuhimu wa yale yote yatakayoafikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa katika muda uliopangwa.

Alishauri iundwe timu ya ngazi ya Makatibu Wakuu ambayo itakuwa inakutana kila baada ya miezi sita kutathmini utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi, Dkt. Dalitso Kabambe alisisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuweka mikakati itakayorahisisha wananchi kufanya biashara bila vikwazo. "Bisahara ni jambo muhimu lazima tuhakikishe kuwa Serikali zetu zinaweka mazingira mazuri ili wananchi wafanye biashara kwa wepesi".

Kikao hicho kinatarajiwa kufungwa rasmi na Mawaziri wa Mambo ya Nje siku ya Jumapili tarehe 05 Februari 2017 ambapo Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anatarajiwa kuwasili Malawi tarehe 04 Februari 2017. Mawaziri hao pia wataweka saini Mikataba mitatu ya ushirikiano katika mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia, usafiri wa anga na utalii.

Wajumbe wa Tanzania katika kikao hicho wanatoka katika sekta mbalimbali wakiwemo wajumbe kutoka mikoa miwili ya Mbeya na  Ruvuma inayopakana na Malawi ambao wanaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla.



Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe  03 Februari 2017


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi na Mwenyekiti Mwenza wa Kikao cha JPCC kati ya Tanzania na Malawi, Dkt. Kalitso Kabambe akisoma hotuba ya iufunguzi na ukaribisho.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akisoma houtuba ya ufunguzi wa kikao cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi, Dkt. Dalitso Kabambe. Kikao hicho kinafanyika Lilongwe, Malawi kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 03 Februari 2017.


Wajumbe wa Tanzania wakisikiliza hotuba za Makatibu Wakuu. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Suleiman Salehe na Kaimu Mkurugenzi kutoka Mamlka ya Viwanja vya Ndege.


Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Ali Ubwa na mjumbe mwingine ambaye jina lake halikupatikana.


Bw. Kalitso Kabambe akiwa na Balozi wa Malawi nchini Tanzania.


Sehemu  ya ujumbe wa Malawi ukifuatilia hotuba za ufunguzi

Wajumbe wa pande zote mbili wakiwa katika kikao cha JPCC

Naibu Katibu Mkuu, Balozi Mwinyi akihojiwa na Mwandishi wa TBC, Bw. Hosea Cheo

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Victoria Mwakasege akihojiwa na Mwandishi wa TBC

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla akifanya mahojiano na Mwandishi wa TBC

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.