Rais Yoweri Kaguta Museveni pamoja na Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakizungumza jambo.
===================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Uganda sio
nchi rafiki tu bali ni ndugu wa kweli lakini Kiwango cha biashara kati ya nchi
hizo hakitafsri ipasavyo ukubwa wa udugu na urafiki uliopo kati ya yao.
Hayo yalibainishwa leo na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
Ikulu jijini Dar es Salaam akiwa na Mgeni wake Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri
Kaguta Museveni.
Rais Museveni yupo nchini
Tanzania kwa ziara ya Kiserikali ya Siku mbili kuanzia tarehe 25 hadi 26
Februari 2017.
“Tanzania iliuza bidhaa
zenye thamani ya Shilingi bilioni 126.744 mwaka 2016 ikilinganishwa na bidhaa
zenye thamani ya Shilingi bilioni 99.882 zilizouzwa mwaka 2015”. “Hiki ni
kiwango kidogo sana ukilinganisha na udugu mkubwa tulionao kati ya nchi zetu
mbili”alisema Dkt. Magufuli.
Rais Magufuli alieleza
kuwa ili kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili, Serikali yake
imeanza mkakati wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli
ya kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam-Mwanza-Isaka hadi Burundi na
Rwanda. Rais Magufuli alisema pia kuwa Serikali itajenga Bandari Kavu jijini
Mwanza ili kuwarahisishia wafanyabiashara wa Uganda kuchukulia bidhaa zao
Mwanza badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.
Sanjari na hayo Serikali
itaboresha bandari ya Bell na itapunguza vizuizi vya barabarani na kubaki
vitatu ili kupunguza muda mwingi unaopotezwa na malori ya mizigo kwenye vizuizi
hivyo.
Kuhusu ujenzi wa bomba la
kusafirisha mafuta kutoka Hoima hadi Bandari ya Tanga, Rais Magufuli alisema
Serikali yake ilishafanyia kazi vikwazo vyote saba vilivyowasilishwa ikiwemo
kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kutoa mwito kwa mwekezaji kuanza ujenzi wa
bomba hilo haraka kwani hakuna kisingizio kingine. Rais Magufuli alisisitiza
umuhimu wa kupanga tarehe ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba hilo na kwamba yupo tayari kusafiri kwenda nchini
Uganda kama itakubalika jiwe hilo kuwekwa nchini humo.
Aidha, Rais Magufuli
alizungumzia jitihada za Serikali yake kufufua Shirika la Ndege la ATCL kwa
kununua ndege sita kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga nchini na nchi
jirani. Alimuomba Rais Museveni muda utakapofika ndege hizo ziweze kwenda
Uganda jambo ambalo liliafikiwa.
Akizungumzia Mkataba wa
Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Umoja
wa Ulaya (EPA), Rais Magufuli aliuona mkataba huo kama kikwazo katika juhudi za
Serikali za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020. Hivyo alimuomba
Rais Museveni kumuunga mkono kuepuka mkataba huo kwa manufaa ya wananchi wa
EAC.
“Rais Museveni alibebwa na
Tanzania wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo namuomba
Rais Museveni naye anibebe katika suala hili la EPA kwa manufaa ya wananchi wa nchi
zetu na Jumuiya yetu” alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Rais
Museveni alibainisha kuwa, hadi leo tatizo kubwa kwa Bara la Afrika lililopelekea
hadi kutawaliwa na wakoloni huko nyuma ni ukosefu wa umoja na msimamo wa pamoja.
Alisema amekuja Tanzania kujadiliana na
Rais Magufuli ili kupata msimamo wa pamoja kuhusu Mkataba wa EPA wenye manufaa
kwa wananchi kwani undugu na umoja
uliopo kati ya nchi hizi mbili ni zaidi ya mkataba huo.
Kuhusu mpango wa Tanzania
kujenga reli ya kiwango cha kimataifa, Rais Museveni aliupongeza mpango huu na
kuutaja kama mchango wa pili wa Tanzania katika ukombozi wa Uganda. Alisema
reli hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa uchumi wa Uganda kwa kuwa utakuwa ni usafiri
wa haraka na gharama nafuu.
Rais Museveni kabla ya
kuondoka nchini kesho tarehe 26 Februari 2017 atatembelea kiwanda cha AZAM kilichopo
Vingunguti jijini Dar es Salaam. AZAM pia imefanya uwekezaji nchini Uganda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dar es Salaam, 25 Februari, 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.