Naibu Katibu Mkuu awatembelea
Watanzania wanaoshikiliwa nchini Malawi
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi
amewasihi Watanzaniawananewanaoshikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini
Malawi kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa
Kayerekera kuwa wavumilivu wakati
Serikali ikitafutaufumbuzi wa suala lao.
Balozi Mwinyi aliyasema hayo alipowatembelea
gerezani ambapo katika ziara hiyo alifuatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa
Ruvuma, Bw. Hassan Bendeyeko pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo
ya Nje na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi.
Balozi Mwinyi aliwaeleza
Watanzania hao kuwa mazungumzo katika ngazi mbalimbali kati ya Tanzania na Malawi
yanaendelea na kuna matumaini makubwa kuwa hivi karibuni ufumbuzi wa suala lao
unaweza kupatikana.
Balozi Mwinyi aliendekea kuekeza
kuwa yeye na wenzake wamekuja Lilongwe kushiriki kikao cha Tume ya Pamoja ya
Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi, lakini wameamua kusafari takriban kilomita 400 kutoka Lilongwe hadi Mzuzu kuja kuwaona na kuwafikishia
ujumbe kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kuwa suala hili linapatiwa
ufumbuzi kwa haraka.
"Nikufahamisheni kuwa
jitihada katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lenu
zinaendelea na hata Mhe. Rais Dkt. John
Pombe Magufuli alipokutana na Rais wa Malawi, Mhe. Prof. Peter Mutharika
pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia jambo
lenu lilikuwa moja ya masuala
waliyoyajadili.
Naibu Katibu Mkuu alisema kuwa
alifarijika kuwakuta watu hao wote wapo salama na wenye afya nzuri na
kuwajulisha kuwa ziara hiyo ya kuwatembelea na nyingine zilizofanyika siku za
nyuma ni ushahidi dhahiri kwao na kwa Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya Rais Dkt. Magufuli imedhamiria kuwahudumia Watanzania wote wa kada
mbalimbali popote pale wanapoishi.
Watanzania hao wanane walikamatwa
mwishoni mwa mwezi Desemba, 2016 na hadi sasa wanashikiliwa katika gereza kuu
la Mzuzu. Watanzania hao ambao kati yao wawili ni wanawake wamejitambulisha ni wakulima na wachimbaji
wadogo wa madini wanatoka katika mkoa wa Ruvuma na walikwenda Malawi chini ya
Taasisi ya CARiTAS kujifunza athari za migodi ya urani katika jamii.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe 05
Februari 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.