Monday, February 20, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Comoro aagwa kwa kutunikiwa Tuzo na Rais

Balozi wa Tanzania kwenye Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga akitunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Azali Assoumani hivi karibuni.

Nishani hiyo imetolewa na Mhe Azali  kwa kutambua mchango wa Balozi Kilumanga katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya Comoro kwa ajili ya kumuaga Balozi Kilumanga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini humo

Mhe. Rais Azali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Kilumanga na Mkewe




Balozi Kilumanga akipongezwa na Mkuu wa Utawala Ubalozini, Bw. Mudrick Soragha mara baada ya kutunikiwa nishani na Rais wa Comoro
============================================

BALOZI WA TANZANIA VISIWANI COMORO ATUNUKIWA MEDANI YA JUU YA HESHIMA NA MHE. AZALI ASSOUMANI, RAIS WA MUUNGANO WA VISIWA VYA COMORO TAREHE 16 FEBRUARI 2017

Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Chabaka Kilumanga ametunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo Mhe. Azali Assoumani. Mhe. Balozi ambaye aliongozana na Mkewe Bi Irene Kilumanga walishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika Bait Salam, Ikulu ya Comoro tarehe 16, Februari 2017. Wageni waalikwa walioshuhudia  hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro,  Mhe. Baccar Dossar na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Comoro Mhe. Yousef Mohamed Yousef.

Hafla hiyo ilifanyika ikiwa ni sehemu ya sherehe ya kumuaga Balozi huyo ambaye amemaliza muda wake wa kazi Visiwani Comoro na kuelekea kustaaafu ifikapo tarehe 17 Machi, 2017. Mhe. Chabaka Kilumanga anakuwa ndio Balozi wa mwanzo kutunukiwa nishani hiyo miongoni mwa mabalozi wenzake wanao tumikia nchi zao Visiwani Comoro. Wakati akimtunuku medani hiyo, Mhe Azali alieleza kutambua mchango mkubwa aliofanya Balozi huyo katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Kwa upande wake Mhe. Balozi alieleza kufarijika sana kwa kutunukiwa Nishahi hiyo ambayo imekuwa ni heshima kubwa kwake. Aidha, Balozi Kilumanga alipongeza juhudi za Serikali ya Mhe. Azali kwa hatua inazochukua katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Comoro. Pia alipendekeza kwa Serikali hiyo kuanza kufanya taratibu za kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro.

Kutunukiwa kwa nishani hiyo kulikuwa ni kwa kushtukiza kwani Mhe. Balozi hakutarajia kabisa kutunukiwa nishani hiyo ambayo kwa kawaida hupewa raia wa Comoro ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa lao. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mhe. Balozi bali pia kwa Tanzania. 

Wakati wakiagana na Mhe. Rais, Mhe. Balozi na Mkewe Bi Irene Kilumanga walieleza kuwa kamwe hawatasahau upole na ukarimu wa Wacomoro na kwamba Comoro itaendelea kuwa mioyoni mwao daima.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.