Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi Ubalozini.
Akizungumza Ubalozini hapo Mhe. Makamba amewapongeza watumishi hao kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kuiwakilisha vyema Tanzania.
Aidha, amewasihi watumishi hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuchapa kazi na kutimiza azma ya kuanzishwa Ubalozi huo na kufikia matarajio ya serikali kutoka kwao.
“Nyinyi ni wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Indonesia mna wajibu wa kuchapa kazi , kushirikiana na kuwa wamoja katika kushirikiana na Indonesia na kufanya mambo yaende”, na kuongeza “mnatakiwa msiende kinyume na matarajio ambayo nchi inayo, nyinyi ni wawakilishi wa nchi kwa hiyo hulka, maneno, muonekano na vitendo vyenu lazima viakisi nchi yenu, na mhakikishe mnalilinda hilo,” alisisitiza Mhe. Waziri Makamba.
Alisema Tanzania inawategemea watumishi hao kuleta manufaa nyumbani kwa kuvutia biashara na wawekezaji na wadau wengine ambao watasaidia juhudi za kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Amesema ziara ya Mhe. Rais nchini Indonesia ni bahati kubwa kwa ubalozi huo kwakuwa mwaka jana ulimleta Rais wa Indonesia Tanzania na safari hiii umemleta Mhe. Rais Indonesia, “wenzenu wanamaliza muda wao bila kupata nafasi kama hii, hili ni jambo la kujivunia na mjipongeze kwa kazi nzuri.
Akiwa Ubalozini hapo Waziri Makamba amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ubalozini hapo.
“Tunajivunia sana uwezo wako Jakarta, uendelee kuchapa kazi na hatutachoka kukusaidia itakapobidi kufanya hivyo,” alisema
Amesema ziara hizo za wakuu wa nchi ni jitihada za kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Indonesia ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
Ameongeza kuwa ziara hiyo pia inalenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika maeneo ya kımkakati ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, uchumi wa buluu na kilimo na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa faida ya pande zote mbili.
Mhe. Makamba yuko nchini Indonesia kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika nchini humo tarehe 24-26 Januari, 2024.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.