Sunday, January 14, 2024

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA ANGOLA WAANZA ZANZIBAR

Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola umeanza tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar.

Mkutano huo unafanyika katika ngazi mbili za maafisa waandamizi unaofanyika tarehe 14 — 15 Januari 2024 na ngazi ya mawaziri utafanyika tarehe 16 Januari 2024.

Mkutano huo unalenga kujadili mambo mbalimbali muhimu ya ushirikiano ya siasa, diplomasia, ulinzi, usalama, Sheria, kilimo, uchumi wa buluu, biashara na uwekezaji.

Maeneo mengine ni pamoja na maendeleo ya miundombinu, ujenzi, uchukuzi, nishati, madini, tehama na huduma za kijamii za afya, elimu, sayansi, na teknolojia ya Habari na mawasiliano. Mkutano huo pia unalenga kuibua maeneo mapya ya ushikiano ili  kuchagiza maendeleo kati ya Tanzania na Angola.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa amebainisha kuwa mkutano huo utatoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo uchumi hususan biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, miundombinu na fedha. 

“Katika mkutano wetu tunategemea kujadili masuala ya uchumi hususan msingi wa diplomasia ya uchumi. Mkutano huu utatoa mipango na mikakati ya pamoja itakayoimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili,” Alisema Balozi Mussa.

Balozi Said aliongeza kuwa mkutano huo unajenga na kuendeleza misingi madhubuti ya mashirikiano katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Angola unaendelea kuimarika zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias amesema mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano imekuwa ikitoa fursa mbalimbali za kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano itaendelea kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya ushirikiano katika nyanja za diplomasia, usalama, ulinzi na uboreshaji wa huduma za kijamii,” alisema Balozi Sardinha Dias.  

Mkutano huu umejumuisha Mabalozi, Watendaji Wakuu na Maafisa mbalimbali wa Serikali kutoka Tanzania na Angola.

Mkutano wa kwanza ulifanyika mwezi Oktoba, 1988 Jijini Dar es Salaam. Kufanyika kwa mkutano huu wa Pili kunafuatia kusainiwa kwa Hati mbili za Makubaliano (MoUs) za kuhuisha/kufufua Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola mwezi Februari 2023 Addis Ababa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar

Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias akizungumza katika Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar

Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar

Viongozi wa Meza kuu katika picha ya pamoja wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye kamba ya njano shingoni) , Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto) pamoja na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Sandro de Oliveira (wa kwanza kulia).

Viongozi wa Meza kuu katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.