Monday, January 23, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Rais wa Uturuki nchini Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayip Erdogan kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea katika mpango wake wa kuzitembelea nchi za Afrika. Kauli hiyo imetolewa leo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa anaongea na waandishi wa habari pamoja na mgeni wake huyo.

Rais Magufuli alimuhakikishia, Rais Erdogan kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uturuki na ana matumaini kuwa kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo kutakuza mahusiano zaidi ya kibiashara ambapo kwa takwimu zilizopo zinaonesha kuwa biashara kati ya nchi hizi mbili imekua kutoka Dola za Marekani milioni 66 mwaka 2011 na kufikia Dola milioni 190 mwaka 2016.

Aidha, Rais alielezea matumaini yake kuwa ziara ya Rais Erdogan nchini, itaongeza uwekezaji kutoka Uturuki ambapo kwa sasa takribani makampuni 30 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 305 ambayo yameajiri watu 2,959 yapo nchini.

Rais Magufuli na Mgeni wake walishuhudia uwekaji saini wa Mikataba 9 ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika maeneo mbalimbali kama vile, viwanda, utalii, usafiri wa anga, utangazaji, elimu, utafiti, ulinzi na afya. Uwekaji saini wa mikataba hiyo utaimarisha ushirikiano na utasaidia pia kufikia azma ya Serikali ya kuifanya kuwa nchi ya viwanda kutokana na teknolojia kubwa iliyofikiwa na Uturuki.

Rais Magufuli alieleza kuwa mojawapo ya kampuni zilizoomba zabuni ya kujenga reli ya kati ni kampuni kutoka Uturuki hivyo, amemuomba Rais Erdogan kuwa endapo kampuni hiyo itashinda zabuni, Benki ya Exim ya Uturuki  itoe mkopo kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya reli hiyo ambayo ina urefu wa zaidi ya kilomita 400.

Kwa upande wake, Rais wa Uturuki aliahidi kushirikiana na Tanzania kukuza uwekezaji na biashara ambapo alisisitiza umuhimu wa kukuza kiwango cha biashara angalau kifikie Dola milioni 500 kwa mwaka.

Aidha, Rais Erdogan alielezea tukio la jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali yake lililofanywa na kikundi cha Fethulla tarehe 15 Julai 2016 ambalo lilisababisha vifo vya watu 240 na maelfu ya majeruhi nchini humo. Alisema wafuasi wa kikundi hicho kilichopanga jaribio hilo wamesambaa hadi katika nchi za Afrika, hivyo, aliomba viongozi wa nchi za Afrika kushirikiana naye katika kukabiliana nao  ili kujihakikishia amani kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Rais wa Uturuki alihitimisha mazungumzo yake kwa kumuomba Rais Magufuli azuru nchini Uturuki wakati wa ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo ambapo Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Januari 2017.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.