Wednesday, January 11, 2017

Waziri Mahiga aipongeza Cuba kwa kuchangia maendeleo nchini


                               Waziri Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipeana mkono na Balozi wa Cuba nchini    anayemaliza muda wake, Mhe. Jorge Luis Lopes Tormo wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika Jijini Dar es Salaam
===================================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, ameipongeza Serikali ya Cuba kwa mchango wake wa maendeleo hapa nchini hususan katika sekta za elimu, afya na kilimo.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mahiga wakati wa hafla fupi ya kumuaga  Balozi wa Cuba aliyemaliza muda wake wa kazi nchini, Mhe.  Jorge Luis Lopes Tormo.

Katika hotuba yake Mhe. Mahiga alisema kuwa, nchi ya Cuba imekuwa ikichangia na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika sekta ya afya, elimu, kilimo na michezo  ikiwa ni jitihada za nchi hiyo za kukuza na kudumisha uhusiano mzuri na wa muda mrefu wa kidiplomasia uliojengeka baina ya nchi hizi mbili.

Mhe. Mahiga alieleza kuwa, takwimu zinaonesha  katika sekta ya elimu, kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi 2014 jumla ya wanafunzi 64 kwa ngazi ya elimu ya juu walipata nafasi za kwenda kusoma nchini Cuba katika tasnia mbalimbali.

Aidha alisema kwamba, Serikali ya Cuba inaendelea kufadhili mradi wa elimu kwa watu wazima unaojulikana kama “NDIO NAWEZA” (“Yes I CAN”), ulioanzishwa kwa pamoja baina ya  Serikali ya Tanzania na Cuba mwaka 2011 chini ya wataalamu kutoka Wizara ya Elimu ya Tanzania na Cuba na kuzinduliwa mwaka 2014. 

Mradi huu unaotekelezwa nchini kwa awamu, sasa unatelezwa katika miji 7 ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Manispaa ya Dodoma, Manispaa ya Songea  Mwanga, Bagamoyo na Mkuranga. Mpaka sasa jumla ya vijana na wazee 2670 wamenufaika na mradi, na inategemewa kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017 mradi utakuwa umewanufaisha jumla ya vijana na wazee 3,321,840.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Jorge Luis Lopes Tormo aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri aliopewa wakati wa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka takrbani mitano aliyokuwepo nchini.

Pia alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kusimamia vyema raslimali za taifa kwa maendeleo ya watu wote. 

Vilevile Balozi Tormo alitumia fursa hiyo kuihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa Cuba itaendelea kuwa mshirika mzuri wa shughuli za maendeleo ikiwemo kuangalia maeneo mbalimbali na fusra ambazo Cuba inaweza kuwekeza nchini, kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana, pato la taifa na kuongeza kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba ulianzishwa mwaka 1962 ukiasisiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castro.

-Mwisho-






No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.