Friday, January 27, 2017

India yaadhimisha miaka 68 ya Uhuru kwa kuzindua Jengo jipya la Ubalozi nchini

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India. Maadhimisho hayo yaliyoenda sambamba na ufunguzi wa Jengo la Ubalozi mpya wa India yalifanyika kwenye Jengo hilo lililopo Mtaa wa Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Januari,
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Ausralasia, Bibi Justa Nyange wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India


Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Balozi wa India nchini, Mhe. Sandeep Arya nae akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Sehemu nyingine ya wageni waalikwa wakisikiliza hotuba ya Balozi wa India (hayupo nchini)

Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Naibu Balozi wa China, Bw. Gou Haudong na Bi. Sun kutoka Ubalozi wa China wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa China.
Wageni waalikwa
Wanafunzi wakiimba nyimbo za mataifa ya Tanzania na India wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Kikundi cha Burudani kikitumbuiza wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Makamu wa Rais, Mhe. Suluhu katika picha ya pamoja
==================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

India yaadhimisha miaka 68 ya Uhuru

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ameipongeza India kwa kuadhimisha miaka 68 ya Uhuru wa nchi hiyo. Pongezi hizo alizitoa jana wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Uhuru wa nchi hiyo ambayo ilienda sanjari na ufunguzi wa jengo jipya la Ubalozi lililopo Mtaa wa Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam.

Mama Samia Suluhu aliipongeza India kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyopata katika nyanja mbalimbali tokea ilipopata uhuru kutoka kwa Mwingereza ambaye pia aliitawala Tanzania.

Makamu wa Rais aliitaja India kuwa sio tu ni rafiki mkubwa wa Tanzania bali ni ndugu wa karibu wanaounganishwa na bahari ya Hindi ambayo imekuwa kiunganishi kikubwa cha wafanyabiashara hata kabla ya uhuru.
Alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na India ni wa kuridhisha na umeimarika zaidi kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi iliyofanyika nchini mwezi Julai 2016. “Wakati wa ziara hiyo mikataba mbalimbali ilisainiwa kati ya nchi hizi mbili ambayo inalenga uedelezaji wa sekta tofauti kwa faida ya pande zote mbili”. 

Mama Samia aliendelea kueleza kuwa ushirika wa Tanzania na India ni wa kimaendeleo ambapo Tanzania imekuwa ikifaidika na misaada mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na msaada wa kuendeleza miundombimu ya maji katika mikoa ya Dar es Salaan na Pwani pamoja na Zanzibar; msaada wa kituo cha TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela mkoani Arusha na uimarishaji wa vyuo vya ufundi.

Mhe. Samia Suluhu alitumia fursa hiyo pia kuishukuru India kwa msaada iliyotoa wa zaidi ya Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la Kagera lililotokea mwezi Septemba 2016. 

Kwa upande wake, Balozi wa India, Mhe. Sandeep Arya aliridhishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na India na kubainisha kuwa ziara ya Mhe. Modi mwezi Julai 2016 imeboresha na kuimarisha zaidi mahusiano hayo. Aliahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali kama ilivyokuwa inafanya siku za nyuma. 

Alisema mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ni makubwa na kwamba nchi yake imeisaidia Tanzania katika maeneo mengi ikiwemo mikopo ya masharti nafuu, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, mafunzo ya ufundi, ujenzi wa vituo vya TEHAMA, na vifaa vya matibabu. 

Alizungumzia pia mahusiano ya asasi za kiraia za Tanzania na India, ushirikiano katika masuala ya utamaduni, ziara za Watanzania kwenda India kwa ajili ya matibabu na michezo ambapo aliitolea mfano wa ziara ya timu ya Taifa ya Serengeti Boys nchini India mwaka jana. 

Mhe. Balozi alihitimisha hotuba yake kwa kusifu uamuzi wa Tanzania na India kufuta viza kwa watu wenye Hati za Kusafiria za Kidiplomasia na zile za Serikali.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Januari 2017.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.