TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU MATOKEO YA AWALI YA NAFASI ZA AJIRA
KATIKA SEKRETARIATI YA SADC ZILIZOTANGAZWA
KWA MWAKA 2018
Sekretarieti ya SADC
ilitangaza nafasi 50 katika kada mbalimbali mwezi wa Mei, 2018. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi ilitangaza
nafasi hizo kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Wizara inapenda kuutangazia
umma kuwa baada ya mchujo wa duru ya kwanza uliofanywa na Kikosi Kazi Maalum,
jumla ya waombaji 141 kati ya waombaji 1,472 wamepita katika uchambuzi wa
awali. Katika muktadha huo, Wizara inaweka orodha ya awali ya mchujo wa
Tanzania ya waombaji waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali pamoja na jedwali lenye
kuonyesha idadi ya waombaji hao.
Wizara inapenda kuutaarifu
umma na waombaji wa nafasi za ajira zilizotangazwa na SADC kuwa taarifa zaidi
itatolewa Sekretarieti ya SADC kwa wale tu watakao kuwa kwenye orodha ya mchujo
wa duru ya pili (shortlisted) utakayofanywa na Sekretarieti ya SADC.
Aidha, tutakumbuka kuwa mwezi wa Mei, 2017 Sekretarieti ya SADC
ilitangaza nafasi 48 ambapo zoezi la usaili wake lilikamilika mwaka huu. Kwenye
nafasi 48, Tanzania imefanikiwa kupata nafasi tano za kimkakati. Nafasi hizo
zinaainishwa kama ifuatazo:
i.
Afisa Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya
Sera na Mikakati ya Maendeleo, (Senior Officer - Policy and Strategy Development);
ii.
Afisa Mwandamizi Mipango anayeshughulikia
masuala ya Viwanda na Ushindani, (Senior Programme Officer - Industrialization and
Competitiveness);
iii.
Afisa Mipango anayeshughulikia masuala ya Ushuru
na Utaratibu, (Programme Officer
Customs and Procedures);
iv.
Afisa anayeshughulikia masuala ya Ufuatiliaji,
Tathmini na utoaji wa Taarifa, (Monitoring, Evaluation and Reporting Officer); na
v.
Afisa anayeshughulikia masuala ya Fedha na
Bajeti, (Finance Officer -
Treasury and Budget )
Tunawapongeza kwa dhati wote waliochaguliwa na
kufanikiwa kuingia kwenye orodha ya mchujo wa awali uliofanyika Tanzania kwa
mwaka 2018.
Aidha, kwa aina ya pekee, tunawapongeza maafisa
waliochaguliwa kwenye nafasi tano (5) zilizotajwa na tunawatakia kila la heri
katika mjukumu yao mapya sambamba na kuwasihi daima kukumbuka kuwa
wanaliwakilisha Taifa letu kwenye nafasi hizo.
Mwisho, Wizara inapenda kutaarifu kuwa
itaendelea kuzitangaza fursa kama hizi zitapojitokeza kupitia SADC na Jumuiya
zingine za Kikanda na Kimataifa ambazo Tanzania ni nchi mwanachama, kwa manufaa
ya watanzania wote. Hivyo, tunawaomba Watanzania wasikate tamaa na wasisite
kuwasilisha maombi ya ajira kama hizi pale fursa zinapojitokeza.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam,
27 Julai, 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.