Balozi wa Tanzania Visiwani Komoro Mhe. Sylvester Mabumba alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi mpya wa Diaspora ya Watanzania waishio Komoro (TADICO) tarehe 23 Julai 2018. Viongozi hao wapya walifika ofisi za Ubalozi kwa ajili ya kujitambulisha ambapo miongoni mwa mambo waliyojadili ni pamoja na kutoa ahadi ya kuinua Diaspora ya Watanzania waishio Comoro ambapo kwa muda mrefu Diaspora hiyo imeonekana kuwa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na Diaspora za nchi nyingine.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mabumba alichukua fursa hiyo kuwapongeza viongozi hao wapya waliochaguliwa pamoja na kuwatakia kila la kheri katika nafasi zao hizo mpya walizoaminiwa na Watanzania wenzao. Aidha, Mhe. Mabumba alisisitiza juu ya umuhimu wa wanachama kulipa michango ya uanachama na vilevile kuwaomba viongozi kuwa wasimamizi wazuri wa matumizi ya fedha za wanachama hao.
Katika hatua za kuhuisha chama hicho wajumbe walishauriwa pia kuwa wabunifu katika mikakati yao na vilevile waangalie njia gani bora za kuibua vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea michango ya wanachama pekee. Pia Balozi Mabumba aliwahimiza viongozi hao kutosahau kuwekeza nyumbani na vilevile kuchangamkia fursa za biashara ambazo zinapatikana Tanzania na kuzitangaza Visiwani humo.
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.