TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU RAIA WA TANZANIA NCHINI OMAN
Kuna kipande cha video kinasambaa
mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa Tanzania wanaoishi nchini Oman
wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na
mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande hicho cha video iliwasiliana
na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni ya kujua usahihi wa jambo
hilo.
Ubalozi ulitoa ufafanuzi kuwa
uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na ulipangwa kufanyika
katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat tarehe 23 Machi 2018. Matangazo ya
mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda kushiriki wajisajili kabla ya siku
ya mkutano. Watanzania takriban 200 walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi
ya ukumbi, vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden
Tulip.
Siku ya mkutano ilipowadia,
Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na kusababisha ugumu wa kuendelea na
mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa yalilenga watu 300.
Kamati ya maandalizi ilipoona ukumbi
umejaa na watu walio nje ni weng mara mbili zaidi ya watu waliokuwemo ndani ya
ukumbi iliamua kufunga milango na kuwaomba waliochelewa warejee nyumbani.
Uamuzi huo haukuwafurahisha watu
waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye ukumbi wa mkutano, kitendo
ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu kubwa.
Kutokana na uhalisia huo, Kamati ya
maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini humo
ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe na maandalizi yaanze upya
kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya
watu.
Kutokana na ufafanuzi huo, Wizara
inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa kipande hicho cha video
kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye ukumbi wa mkutano
na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa Tanzania kushinikiza
kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso wanayoyapata.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Machi,
2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.