Wednesday, April 21, 2021

MKUTANO WA KAWAIDA WA 20 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA AFYA UNAENDELEA KUFANYIKA JIJINI ARUSHA, TANZANIA.

Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya umeendelea kufanyika kwa siku ya tatu leo, katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania. 

Mkutano huu ambao utafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Aprili 2021,una lenga kufanya mapitio ya hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na la Kisekta. Vilevile mkutano huu ataangazia masuala mengine muhimu katika Sekta ya Afya ndani ya Jumuiya. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu katika ngazi ya wataalamu Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashukuru wataalamu wa Sekta ya Afya kwa juhudi zao za kutatua changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo na ushauri wa kitaalamu kwa ngazi za maamuzi ambayo yamepelekea utekelezaji wa mipango ya ubunifu katika sekta ya Afya na kuunganisha vipaumbele vya uwekezaji kwenye sekta hiyo katika Jumuiya. 

Katika ngazi ya Wataalamu mkutano huu unafuatilia na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya kama ilivyoelekezwa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri na la Kisekta, ikiwemo; maendeleo ya utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Korona (UVIKO-19), usalama wa dawa na chakula, masuala ya afya ya uzazi, Watoto na Lishe na hali ya utekelezaji wa miongozo na taratibu za taaluma na huduma za afya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano katika ngazi ya wataalamu Dkt. Leonard Subi Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto ameeleza kuwa; Tanzania imeendelea kuongeza mikakati ya kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19 tangu lilipozuka katikati ya Machi 2020. Ameongeza kusema kuwa UVIKO-19 ni ugonjwa mpya wa aina yake kwani tumeshuhudia tishio la ukuaji wa uchumi wa ulimwengu na umegharimu maisha ya watu wengi sehemu mbalimbali duniani, hivyo mshikamano ni muhimu ili kuukabili. “Tanzania tunadhamini juhudi zinazofanywa na Wanasayansi mbalimbali ulimwenguni katika kupata suluhisho la kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na mshikamano ulioonyeshwa na WHO, GAVI na Taasisi zingine zinazounga mkono jitihada hizo. Tanzania haikatai chanjo ya UVIKO-19, isopokuwa tunafanya tathmini thabiti kabla ya kukubali matumizi ya chanjo nchini. Mathalani, Tanzania nyakati zote imekuwa na rekodi za juu kwenye matumizi ya chanjo kwa watoto wachanga walio chini ya miaka 5 hivyo tutaendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa wadau wa ndani na Wakimataifa katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.” Ameeleza Dkt.Subi

Mkutano huu unaofanyika kwa njia mbili ya ana kwa ana na video, umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Aprili 22, 2021 watakutana Makatibu Wakuu na Aprili 23, 2021 watakutana Mawaziri wanaosimamia masuala ya Afya kutoka nchi Wanachama.

Kaimu Mkurugezi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota akichangia jambo kwenye Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt.Leonard Subi akifuatilia mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt.Leonard Subi akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

 

Ujumbe kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano
Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.