Friday, April 16, 2021

KATIBU MKUU BALOZI BRIGEDIA JENERALI IBUGE ARIDHISHWA NA UENDESHWAJI WA MIRADI MWANZA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge ameeleza kuridhishwa kwake na ubunifu na uendeshwaji wa miradi mbalimbali ya maji na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa Victoria. Miradi hiyo inatekelezwa chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC). 

Balozi Ibuge kwenye ziara hiyo akiwa ameambatana na wataalamu kutoka Sekta ya Maji, Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Wataalumu kutoka LVBC, amebainisha kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutambua maendeleo ya Miradi inayotekelezwa katika ukanda wa Ziwa Victoria ambayo inawagusa wananchi zaidi ya milioni 40 kutoka Nchi Tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kubaini changamoto zilizopo ili kutoa suluhisho linalofaa. 

Akizungumza wakati akihitimisha ziara hiyo Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameongeza kueleza kuwa asilimia kubwa ya Ziwa Victoria ipo Tanzania (kwa 51%) hivyo, Serikali ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania inayapa kipaumbele kinachostahili masuala yote ya maendeleo yanayoendelea katika Ziwa hilo sambamba na masuala ya kiusalama. “Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kutengeneza meli kubwa za usafirishaji na uvuvi ili kuwezesha maendeleo ya wananchi na kuhakisha usalama wao wakati wote wakiwa wanatekeleza majuku yao” amasema Balozi Ibuge.

Wakati huohuo Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amepokea taarifa ya mpango mkakati wa utelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde la Ziwa Victoria, iliyowasilishwa na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo Dkt. Ally Said Matano. Sambamba na uwasilishaji wa taarifa hiyo Dkt. Matano ametoa rai kwa Serikali ya Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa LVBC katika kutekeleza majukumu yake ambayo yanalenga kuboresha maisha ya wana Afrika Mashariki. 

LVBC ni Taasisi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye Makao Makuu yake Kisumu, Kenya. Taasisi hii ilianzishwa ili kuratibu maendeleo endelevu na usimamizi wa Bonde la Ziwa Victoria katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo nchi hizo zililitaja Bonde hilo kuwa eneo la “maslahi makubwa ya kiuchumi na eneo la ukuaji wa uchumi wa Kikanda litakaloendelezwa kwa pamoja na Nchi wanachama wa Jumuiya

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akifuatilia uwasilishwaji wa mpango mkakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde la Ziwa Victoria uliokuwa ukifanywa na Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo Dkt. Ally Said Matano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge (kulia) akimfuatilia Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Ally Said Matano (kushoto) wakati akiwasilisha mpango mkakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde hilo.
Sehemu ya Wadau kutoka sekta mbalimbali wakifuatilia uwasilishwaji wa mpango mkakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde la Ziwa Victoria uliokuwa ukifanywa na Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo Dkt. Ally Said Matano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisisitiza jambo baada ya uwasilishwaji wa mkakati wa utekelezaji wa mpango miradi katika Bonde la Ziwa Victoria

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.