Friday, November 1, 2024

Wagonjwa wa Moyo kutoka Malawi Kutibiwa JKCI

Serikali ya Jamhuri ya Malawi imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili wagonjwa wa moyo waliopo nchini humo hasa watoto kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda alipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Mhe. waziri Chiponda ambaye pia kitaaluma ni mfamasia alisema ameridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwani ameona vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo, amekutana na wataalamu wabobezi ambao wanatibu moyo na kuipongeza JKCI kwa kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo.

 “Nimefurahi sana kufika hapa nimeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yenu pamoja na huduma inayotolewa ni jambo la kufurahi na kushangaa kuona huduma hii inapatikana Afrika tena katika nchi jirani ya Tanzania, tukirudi nyumbani tutaona namna ya kuwa na makubaliano na taasisi hii ili wagonjwa wetu waje kutibiwa hapa hasa watoto”.

“Ninawashukuru wataalamu wa taasisi hii kwani mmekuwa mkiwahudumia wagonjwa kutoka nchini Malawi ninawaomba mzidi kuwahudumia kwani tunahitaji msaada wenu tunafurahi kuona baada ya kupata matibabu wagonjwa wanarudi nyumbani wakiwa na furaha. Pia ninawaomba mje nchini kwetu japo kwa wiki mbili kufanya kambi za matibabu ili kuwasaidia watu wenye matatizo ya moyo”, alisema waziri Chiponda.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo Dkt. Angela Muhozya alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea JKCI na kusema kuwa watahakikisha wanatoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi wenye matatizo hayo.

Dkt. Angela alisema mwaka jana wataalamu wa taasisi hiyo walikwenda nchini Malawi katika hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo katika nchi hiyo kufanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo ambapo waliona watu 724 kati ya hao waliokuwa na matatizo ya moyo walikuwa 537.  

“Taasisi yetu imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika hasa zile tunazopakana nazo mipaka ikiwemo ya Malawi hadi sasa tumeona wagonjwa 33 kutoka nchini hiyo ambapo watu wazima walikuwa 22 na watoto 11”.

“Licha ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo taasisi yetu pia inatoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa afya, ninawaomba muwatume madaktari na wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba vya moyo waje kujifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo pamoja na kutumia vifaa hivyo”, alisema Dkt.Angela.

Kwa upande wake balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola alisema wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kutangaza diplomasia ya uchumi inayojumuisha mipango ya kuinufaisha nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

“Wenzetu kutoka nchini Malawi wamekuja Tanzania kuhudhuria mkutano wa MERCK Foundation nasi tukaona tutumie nafasi hii kuwaleta JKCI ili waone huduma za matibabu ya moyo tunazozitoa, wamefika hapa wameziona na kuzitambua hii itasaidia kuwashawishi wamalawi kuja kutibiwa moyo nchini kwetu”, alisema Mhe. Balozi Agnes.

Mhe. Balozi Agnes alisema Tanzania imepiga hatua katika sekta ya afya kwani wananchi wanapata kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu wao kama ubalozi wataendelea kuwashawishi wamalawi kuja kutumia huduma za matibabu ya zilizopo nchini. 



AICC NI MUHIMILI WA SEKTA YA UTALII NCHINI


Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kimeelezwa kuwa ni moja ya muhimili muhimu katika kufanikisha agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya utalii nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 31, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo alipokutana na uongozi wa kituo hicho chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe.

Mhe. Londo alisema kuwa Rais Samia amelipa umuhimu mkubwa suala la utalii ndiyo maana amecheza filamu ya Tanzania: The Royal Tour, na manufaa yake yameaanza kupatikana kwa kuongezeka kwa watalii na fedha za kigeni nchini.

 "Utalii una maeneo mengi na moja kati ya hayo maeneo ni utalii wa mikutano. Hivyo, kwa  Tanzania hakuna taasisi nyingine inayotegemewa na Serikali kulitekeleza kwa ufanisi eneo hili na kulitolea  miongozo isipokuwa AICC pekee", Waziri Londo alisema.

Mhe. Londo aliongeza kuwa AICC ndiyo sura na kioo cha nchi na ni moja ya kituvu cha diplomasia ya Tanzania, hivyo,  endapo watumishi wa kituo hicho watajituma kwa kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa, basi watakuwa wamelitangaza vyema jina la Tanzania. 

"Mnapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi, wanaokuja kushiriki mikutano. Wageni hawa, wengi wao huwa hawapati fursa ya kwenda sehemu yoyote zaidi ya AICC kutokana na ratiba za mikutano, maana yake wakiridhika na huduma zenu, mtakuwa mmelitangaza jina la Tanzania na kinyume chake mtakuwa mnalibomoa jina la Tanzania" Mhe. Londo alitahadharisha.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Mwakatobe ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, amesema kuwa malengo yake ni kukifanya kituo hicho kuwa taasisi namba moja nchini, Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau ili aweze kufanikisha lengo hilo.

Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazokikabili kituo hicho kama vile uchakavu wa miundombinu, kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi, ameanza kuchukua hatua ya kufanya maboresho ya majengo na ununuzi wa vifaa vya kisasa kama vile vifaa vya ukalimani, vyoo na vipoza joto.

Aidha, amesema  kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao, Kituo kimeanza kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili shughuli zote ziweze kufanyika kidigitali kwa lengo la kuongeza mapato na kuleta ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja. 

Amemalizia kwa kusema kuwa mapato ya kituo hicho yameongezeka kwa kupata faida ghafi ya bilioni 6.5 mwaka 2023/2024 ukilinganisha na faida ya bilioni 1.7 mwaka 2022/2023.

Mhe. Naibu Waziri Londo kabla ya kufanya kikao na menejimenti ya AICC alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na kituo hicho. Maeneo hayo ni pamoja na Kijenge site D 1 lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 21, Kijenge site E lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48 na Soweto ambapo pia kuna makazi na ukubwa wa ekari zaidi ya 50. 

Mhe. Naibu Waziri baada ya kuona maeneo hayo ambayo yote yapo katikati ya jiji la Arusha, amesema kuwa AICC ina uwezo wa kulibadilisha jiji hilo endapo rasilimali hizo zitatumiwa ipasavyo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akizungumza na Menejimenti ya Kituo  cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Aliyesimama ni Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe akiwasilisha taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya AICC.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akisisitiza jambo alipozuru eneo Kijenge lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48. Eneo hilo inamilikiwa na linapatikana katikati ya jiji la Arusha.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe kabla ya Mhe. Naibu Waziri hajaanza ziara ya kukagua miradi ya kituo hicho jijini Arusha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo (kulia) akiwa katika eneo lingine la makazi linalomilikiwa na AICC ambalo pia lipo Kijnege. eneo hili lina ukubwa wa ekari 21 pia linapatikana katikati ya jiji la Arusha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo (kulia) akiwa katika moja ya maeneo ya AICC. Anayetoa maelezo kwa Mhe. Naibu Waziri ni Afisa Mwandamizi wa Kituo hicho, Bw. Assah Mwambene. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili AICC kwa ajili ya kufahamu shgughuli za kituo hicho. Anayemwangalia ni Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe