Thursday, December 5, 2013

Korea Kusini kuwekeza katika mradi wa umeme nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya  Mambo ya Nje ya Korea Kusini, Bw. Moon Duk-ho walipokutana kwa mazungumzo Jijini Soul, Kore Kusini hivi karibuni. Balozi Mbelwa yupo nchini Korea Kusini kwa ziara ya kikazi.


Balozi Mbelwa (kulia) akimsikiliza Bw. Moon Duk-ho wakati wa mazungumzo yao. Pembeni kwa Balozi Mbelwa ni Bw. Francis Mosongo, Afisa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Japan.

Picha ya pamoja kati ya Balozi Mbelwa (wa tatu kutoka kulia) na Bw. Moon Duk-ho (wa tatu kutoka kushoto) pamoja na Wajumbe waliofutana nao.



---------------------------------------------------------------------------------------------
 

Kampuni kubwa za Korea Kusini kuwekeza katika mradi wa uzalishaji wa umeme nchini


Kampuni ya Daewoo ya nchini Korea Kusini, imetangaza kuwekeza katika mradi wa kufua umeme kwa kutumia maji, Mkoani Iringa. Taarifa ya uwekezaji huo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea ya Kusini, Bwana Moon Duk-ho, wakati alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Asia na Australasia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki, jijini Seoul, Jumatatu 3 Desemba, 2013.

Akifafanua kuhusu mradi huo wa umeme unaojulikana kama (Iringa Hydro-Power Project), Bwana Moon Duk-ho alisema kuwa tayari Kampuni ya Daewoo kwa kushirikiana na Taasisi ya Serikali ya Korea ya Kusimamia Rasilimali Maji, wamekwisha anza kazi ya upembuzi yakinifu na kwamba utekelezaji wa mradi huo utaanza mara tu kazi hiyo itakapamalizika mwanzoni mwa mwaka 2014.

Mradi huo utaokagharimu mamilioni ya Dola za Kimarekani unatarajiwa kuwanufanisha zaidi ya wakazi 2000 kutoka vijiji mbalimbali mkoani Iringa na mikoa ya jirani ya Njombe, Songea na Mbeya.

Upatikanaji wa nishati ya umeme ni moja ya changamoto kubwa kabisa inayoikabili Tanzania, kwani kati ya Watanzania kumi, ni wawili tu ndio wanaopata nishati hii muhimu.

Sambamba na uwekezaji huo, Serikali   ya Korea imedhamiria kuanzisha ushirikiano na Tanzania katika masuala ya nishati ambapo mwakani mwezi Februari 2014, Timu ya Wataalam wa Nishati kutoka Korea watatembelea Tanzania kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini.

Akitoa salamu za shukrani, kwa niaba ya serikali ya Tanzania, Balozi Mbelwa Kairuki alisema,“mradi huu wa Daewoo unakuja wakati muafaka ambapo Serikali ya Tanzania chini ya dira ya Taifa (Vision 2025) imedhamiria kuongeza huduma ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwa Watanzania kutoka asilimia 18.4 hadi 30 kwa ngazi ya taifa, na kutoka asilimia 6.5 hadi 15  kwa maeneo ya vijijini, ifikapo mwaka 2025.”

Aidha Balozi Kairuki, alitumia fursa hiyo pia kukaribisha wawekezaji zaidi kutoka Korea Kusini kuwekeza kwenye Sekta ya Viwanda na Utalii ili kutengeneza fursa za ajira.

Korea  Kusini ni miongoni mwa nchi marafiki wa karibu wa Tanzania na kwa zaidi ya miongo minne, Serikali za Tanzania na Korea Kusini zimeshirikiana na kusaidiana kwenye masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Ujio wa kampuni kubwa kama ya Daewoo unaonesha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili.

Mbali na ushiriikiano katika kuendeleza sekta ya nishati, Serikali ya Korea ya Kusini pia imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia mradi wa kuanzisha vijiji vya mfano vitakavyowezeshwa kwa kupatiwa teknolojia za kilimo na miundombinu ya maji, umeme na barabara.  Tayari Korea imeanzisha vijiji vya aina hiyo huko Pangawe, Morogoro na Zanzibar.

Aidha, Korea Kusini, imeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza elimu ya juu kwa kuongeza fursa za masomo kwa Watanzania hususan kwenye sekta ya gesi na mafuta.

-Mwisho-

 












 

Tuesday, December 3, 2013

Balozi Chabaka Kilumanga awasilisha Hati za Utambulisho nchini Comoro


Mhe. Dkt. Ikililou Dhoinine, Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro akisoma Hati za Utambulisho za Mhe. Balozi Chabaka Kilumanga, katika Ikulu ya Beit Salaam, Moroni.



Mhe. Dkt. Ikililou Dhoinine wa Muungano wa Visiwa vya Comoro akiwa katika mazungumzo na Mhe. Balozi Chabaka Kilumanga mara baada ya kupokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi huyo. 















Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Visiwani Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga, leo tarehe 3 Desemba 2013 amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Dkt. Ikililou Dhoinine, Rais wa Muungano wa Visiwa vya Muungano wa Comoro.


Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ikulu ya Beit Salaam, Mhe. Balozi Kilumanga na Mhe. Rais Dhoinine walipata fursa ya kuzungumza machache katika muktadha wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya Tanzania na Comoro kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Comoro pamoja na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania mjini Moroni.

Kamati ya Bunge ya Biashara na Uchumi yatembelea Ubalozi Mdogo - Dubai


Bw. Omary Mjenga (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Bunge ya Biashara na Uchumi ilipotembelea Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Dubai hivi karibuni.


Uteuzi wa Dr. Asha-Rose Migiro