Thursday, August 24, 2017

Diaspora ni rasilimali muhimu katika kuimarisha uchumi wa Afrika, Makamba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Issa Haji Ussi Gavu, akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) kuzungumza na Watanzania waishio ughaibuni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Kongamano la Nne la Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora), linalofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff Mjini Zanznibar.
Baadhi ya Watanzania waishio Ughaibuni wakisikiliza Hotuba ya ufunguzi.
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nao wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi
Sehemu nyingine ya wageni waliohudhuria mkutano wa nne wa Diaspora unaoendelea mjini Zanzibar
Mhe. Makamba akiendelea kuzungumza na Watanzania waishio ughaibuni.


Watanzania waishio ughaibuni wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi
Watanzania waishio ughaibuni wakiingia kwenye meli ya MV Mapinduzi 2 tayari kuzunguka na kujionea mandhari ya visiwa vya Tumbatu na Nugwi kwa madhumuni ya kutambua  fursa za uwekezaji.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Severa Kazaura (wa kwanza kulia), akiwa katika chumba cha manahodha ambapo alimshuhudia Nahodha wakike akiiongoza meli MV Mapinduzi.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya uendelezaji Biashara Tanzania(TanTrade) Bw Edwin Rutageruka (kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mh William Erio na Mkuu wa Kitengo na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Bi. Mindi Kasiga wakiwa katika safari ya Kuzunguka na meli ya MV Mapinduzi pamoja na Watanzania waishio Ughaibuni. 
Watanzania waishio Ughaibuni wakipata burdani kwenye meli ya MV Mapinduzi waliyoitumia kuzunguka nayo kujionea Mandhari ya Visiwa vya Tumbatu na Nungwi.


Taarifa kwa Vyombo vya Habari 
Serikali imeahidi itaendelea kuboresha mazingira  wezeshi ili wanadiaspora   wengi zaidi waweze kuwekeza nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Januari Makamba (Mb) ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Diaspora unaofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mjini Zanzibar.

Mhe. Makamba alibainisha kuwa mwaka jana pekee, Bara la Afrika lilipokea kiasi cha Dola za Marekani bilioni 33 kutoka kwa Diaspora, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko misaada ambayo bara hilo inapokea kutoka nchi wahisani. 

Alisema hiyo inadhihirisha kuwa endapo nchi zitaweka mazingira mazuri ya kuvutia wanadiaspora watakuwa na mchango mkubwa wa kuinua uchumi wa nchi zao.


"Nchi nyingi duniani zinatumia diaspora yao kuendeleza mipango ya maendeleo na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza kama vile uhaba fedha za kigeni" Waziri Makamba alisema



Alitolea mfano wa Zimbabwe ambayo mwaka jana ilipokea kiasi cha Dola milioni 750 kutoka Diaspora ya nchi tatu ambazo ni Afrika Kusini, Marekani na Uingereza na kufanikiwa kupunguza tatizo la uhaba wa fedha za kigeni.


Akionesha zaidi umuhimu wa diaspora katika uchumi wa nchi, Mhe. Makamba alisema nchi ya Kenya kwa mwaka jana pekee, iliingiza Dola bilioni 1.7 kupitia diaspora, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko ilichopata kupitia sekta ya utalii na kilimo cha maua ambazo ndio sekta zinazoingiza fedha nyingi kwa nchi hiyo.


Alieleza namna baadhi ya nchi zinavyotumia mbinu mbalimbali kuwawezesha diaspora wao kuwekeza. Baadhi ya mbinu hizo ambazo zinaweza zikatumiwa hata na nchi yetu ni pamoja na kutoa hati fungani maalum kwa ajili ya diaspora. Alisema mbinu hiyo inatumiwa na nchi nyingi duniani kama India na Nigeria kukusanya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ikiwemo ya miundombinu.


Mhe. Makamba aliwahimiza wanadiaspora kuwekeza nchini na kwamba Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika kwa yeyote mwenye dhamira ya dhati ya kuwekeza. Aidha, alieleza kuwa yeyote anayetaka kuwekeza nchini na akakumbana na vikwazo atoe taarifa mapema kwenye mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.


Baadhi ya watoa mada ambao ni pamoja na Geofrey Simbeye wa TPSPF; Joseph Simbakalia wa EPZA; Geofrey Mwambe wa TIC na Edwin Rutagerura wa TANTRADE waliwashauri wanadiaspora kuunda kampuni ya uwekezaji katika maeneo yao wanayoishi. Kampuni hiyo itakuwa ni fursa kwa kila mwanadiaspora kuchangia mtaji angalau wa Dola 200 kila mwezi ili fedha hizo zitumike kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini.


Wabobezi hao wa masuala ya uchumi na biashara walishauri pia wanadiaspora wawekeze katika miradi isiyohitaji mitaji mikubwa kama vile miradi ya kuzalisha bidhaa zinazotumia ngozi kama viatu, mabegi na mipira.


Mwisho wanadiaspora wanaoshiriki mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo "Mtu kwao ndio Ngao" walielezwa kuwa hali ya kisiasa nchini ni tulivu, hivyo wasiwe na shaka yeyote wawekeze kwa wingi miradi yao itakuwa salama.


-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Zanzibar, 23 Agosti 2017








Wednesday, August 23, 2017

Waziri Mahiga ampokea Waziri wa Nchi wa Uingereza ambaye yupo ziarani nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Mhe. Stewart Rory alipofika Wizarani tarehe 22 Agosti, 2017 kwa ajili ya mazungumzo rasmi na Waziri Mahiga. Katika mazungumzo yao walisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Uingereza. Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lale la Kimataifa la Maendeleo (DFID) inaisadia Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Maji, Elimu, Nishati Mbadala na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya. Mhe. Stewart yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili tarehe 22 na 23 Agosti, 2017.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Mhe. Stewart. Kulia ni Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Sarah Cooke, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID), Bi. Beth Arthy na Afisa kutoka Ubalozini.
Sehemu ya ujumbe wa Wizara wakati wa mazungumzo kati ya Waziri Mahiga na Waziri Stewart kutoka Uingereza (hawapo pichani). Kushoto ni Bw. Salvatory Mbilinyi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Bw. Joseph Kapinga, Afisa Mambo ya Nje.
Waziri Mahiga akiagana na mgeni wake Mhe. Stewart mara baada ya kumaliza mazungumzo yao
Picha ya pamoja
Waziri Mahiga kwa pamoja na Mhe. Stewart wakizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu lengo la ziara ya Mhe. Stewart nchini.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea

Joint Communique issued by His Excellency Dr. John Pombe Joseph Magufuli President of United Republic of Tanzania and His Excellency Abdel Fattah Al Sisi, President of The Arab Republic Of Egypt , 14th -15th, August,2017 - Dar es Salaam.






Tuesday, August 22, 2017

Warsha kuunganisha Mipango ya APRM na Mipango ya Serikali kufanyika Zanzibar



                                                                                          


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Warsha kuunganisha Mipango ya APRM na Mipango ya Serikali kufanyika Zanzibar


Tunapenda  kuwafahamisha kuwa warsha ya APRM itafanyika tarehe 24 – 25 Agosti 2017, kwenye hoteli ya “Golden Tulip Boutique”, Zanzibar. Warsha hiyo itahudhuriwa na Wakurugenzi na maafisa waandamizi toka idara za Mipango na Sera za Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wapatao 50. Na pia itakuwa na watoa mada toka nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar yenyewe, Afrika ya Kusini, Ghana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.


Warsha hiyo inalenga kujenga uwezo wa Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), katika kuoanisha (kuunganisha) Mpango Kazi wa APRM na mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, hasa Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kuleta Maendeleo Na. III. 


Na itajadili masuala yafuatayo: Namna ya kuunganisha Mipango ya Maendeleo ya nchi, Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Malengo Endelevu ya Milenia pamoja na Mpango Kazi wa APRM; Uzoefu wa nchi nyingine za Kiafrika katika kuunganisha Mipango yao ya Maendeleo na Mpango Kazi wa APRM na Mkakati wa Tathmini na Ufuatiliaji.


Warsha hiyo inagharamiwa kwa pamoja baina ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Uchumi Barani Afrika pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.


Mwishoni inatarajiwa kuwa washiriki wataweza kuunganisha  Mpango Kazi wa APRM na kuonda changamoto za Utawala Bora pamoja na Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar kwa lengo la kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kujenga uhusiano kati ya Mipango hiyo pamoja na kukuza uwezo wa kitaasisi.


Hatua hiyo ni muhimu sana kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha Taarifa ya kuondoa changamoto za Utawala Bora zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Nchi. Na hatimaye nchi yetu itaweza kuwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto hizo kwenye kikao cha Wakuu wa nchi wanaoshiriki mchakato wa APRM.


Inatarajiwa kuwa, kwa kutatua changamoto za utawala bora nchi itaweza kuendelea kuwa na amani na utulivu, kukuza uchumi, kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kuharakisha Muungano wa Kikanda, na hatimaye kuwaondolea wananchi umaskini.


Tanzania ni mojawapo kati ya nchi 36 za Afrika zinazoshiriki mchakato wa APRM, nayo imeshawasilisha Ripoti yake ya kwanza kwa Wakuu Wenza wanaoshiriki mchakato huu mwaka 2013. Hivi sasa ipo katika hatua ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Utawala Bora.


Imetolewa na APRM Tanzania
22 Agosti 2017


Monday, August 21, 2017

Waziri wa Nchi anayeshugulikia Masuala ya Afrika wa Uingereza kuzuru Tanzania


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Waziri wa Nchi anayeshugulikia Masuala ya Afrika wa Uingereza kuzuru Tanzania tarehe 22 na 23 Agosti 2017


Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Mhe. Stewart Rory atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Agosti 2017. 


Mhe. Rory anakuja nchini kwa madhumuni ya kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (Department for International Development – DFID).


Aidha, wakati wa ziara hiyo, Mhe. Waziri Rory amepangiwa miadi ya kuonana na Viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).

Baadhi ya miradi ambayo, Mhe. Waziri ataitembelea ni upanuzi wa Bandari ya Dar Es Salaam, Shule ya Msingi Mkoani, Bonde la Mto Msimbazi, Kiwanda cha Nguo cha Tooku kilichopo katika Eneo la Viwanda la Benjamin Mkapa, Mabibo jijini Dar es Salaam na kampuni ya Songas. 


Waziri Rory pia anatarajiwa kushiriki chakula cha mchana na vijana wa Kitanzania katika moja ya migahawa `ya kawaida katika mitaa ya jiji la Dar Es Salaam


Baada ya kukamilisha ziara yake, Waziri Rory ataondoka nchini tarehe 23 Agosti 2017 kurejea London.



-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 21 Agosti 2017