Tanzania
na Burundi zimejipanga kuutumia Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kama
njia mojawapo ya kuhamasisha wananchi wa pande zote mbili kuchangamkia fursa
mbalimbali za uchumi zinazopatikana katika nchi hizi ili kunufaika nazo.
Kauli
hiyo imetolewa kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge na
mwenzake kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba walipokutana na Waandishi wa Habari
leo mjini Kigoma kwa ajili ya kuwajulisha kuhusu mkutano huo utakaofanyika
mjini humo kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.
Balozi
Ibuge alieleza kuwa, Tanzania na Burundi zimeendelea kuwa na ushirikiano wa
kihistoria na kindugu kwa muda mrefu huku kila nchi ikinufaika kwa kiasi kikubwa
na ushirikiano huo. Hata hivyo alieleza kuwa, bado upo umuhimu mkubwa wa
kuendelea kuwahamasisha wananchi wa Tanzania na Burundi kuchangamkia fursa
mbalimbali zinazopatikana kwenye nchi hizo ili ziwanufaishe kiuchumi. Fursa hizo
ni pamoja na biashara na uwekezaji.
“Mikutano
ya Tume za Pamoja za Kudumu pamoja na mambo mengine inaangalia namna ya kuhakikisha
kila mwananchi kutoka nchi husika ananufaika na fursa zilizopo na jukumu letu
ni kuendelea kuwahamasisha kuzichangamkia fursa hizo” alisema Balozi Ibuge.
Akizungumzia
ukuaji wa sekta ya uchumi kati ya Tanzania na Burundi, Balozi Ibuge alisema pamoja
na changamoto mbalimbali, biashara kati
ya Tanzania na Burundi imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kutoa mfano wa kipindi
cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 ambapo Tanzania na Burundi zilifanya biashara zenye
thamani ya shilingi Bilioni 619.9 ukiwa ni
wastani wa Shilingi Bilioni 123.9 kwa mwaka. Katika kiasi hicho, Tanzania iliuza nchini
Burundi bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 604.9 na Burundi iliuza
Tanzania bidhaa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.4.
Aidha,
akizungumzia huduma ya wakimbizi, Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania
imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi huku Serikali ya Burundi
ikiendelea kuwahimiza wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari kutokana na
kuimarika kwa hali ya amani na utulivu nchini humo.
“Tanzania
imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi, hata hivyo kutokana na kuimarika
kwa hali ya amani na usalama nchini kwao Serikali yao imeendelea kuwahimiza
kurejea ili kwenda kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa lao. Itakumbukwa
kuwa, zoezi la kuwawezesha wakimbizi hao kurejea kwa hiari Burundi limeendelea
kuratibiwa na Kamati ya Utatu inayojumuisha Tanzania, Burundi na Shirika la
Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo kati ya mwezi Septemba 2017 na
Februari 2021, jumla ya wakimbizi 113,488 wamerejea nchini Burundi kwa hiari”
alifafanua Balozi Ibuge.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba
alisema tume ya pamoja ya ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kuimarisha
ushirikiano baina ya nchi na nchi kwani hutoa nafasi kwa nchi mbili kutathmini mafanikio
yaliyofikiwa kupitia ushirikiano uliopo, kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali
na kuainisha hatua imara zaidi za kufikia malengo kusudiwa. Alieleza kuwa,
mikutano hii ni fursa nzuri kwa pande zote mbili kujipanga na kuboresha
utendaji kulingana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani na katika nchi yakiwemo
yale ya kisera na kimazingira.
Kadhalika,
alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Tanzania na kuitaja kama nchi ya
kupigiwa mfano katika kuhudumia wakimbizi wakiwemo wale wa kutoka Burundi ambao
wamekuwa wakipokelewa tangu mwaka 1972. Aliongeza kuwa, Burundi inajivunia
mchango wa Tanzania kwenye ustawi wa nchi hiyo na kwamba nchi hiyo inavutiwa na
uongozi imara wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambao unalenga kuwaletea wananchi wote maendeleo.
Mkutano
wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ambao
unafanyika miaka 15 baada ya Mkutano wa Tano uliofanyika jijini Dar es Salaam
mwaka 2006 unalenga kuendeleza, kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano
uliopo kati ya Tanzania na Burundi. Mkutano huu ambao utaanza kwa ngazi ya
wataalam kutoka Tanzania na Burundi tarehe 3 Machi 2021utahitimishwa na Mkutano
wa Mawaziri kutoka nchi hizo tarehe 5 Machi 2021.
=================================================================
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba. |
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Ntirampeba akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Tanzania, Prof. Riziki Shemdoe (katikati) pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji wa Tanzania, Mhandisi Nadhifa Kemikimba wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. |
|
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. |
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba naye akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. |
|
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata naye akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021 |
|
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jily Maleko akifuatilia Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021 |
|
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Frank Mwega akifuatia Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021 |
|
Sehemu ya wadau kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Burundi walioshiriki mkutano kati ya Baloiz Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021 |
|
Sehemuu nyingine ya wadau |
|
Sehemu ya wadau wakifuatilia mkutano |
|
Wadau wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi |
|
Mkutano ukiendelea |