Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali za uwekezaji.
Alitoa wito huo katika kongamano kubwa la biashara
na uwekezaji (Tanzania India Trade Conference) lililofanyika katika jiji la Chennai, India tarehe 11 na 12 Aprili
2022.
Kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini India na Taasisi ya Uchumi na Biashara ya India (Indian Economic Trade Organization) lilitoa fursa kwa taasisi mbalimbali
zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara ikiwepo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE),
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwasilisha mada
kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Balozi Mbega alisema licha
ya India kuwekeza nchini mtaji wa kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 3.7 na
kuifanya nchi hiyo kuwa ya tano kwa uwekezaji, lakini bado nchi hiyo ina fursa kubwa
ya kuongeza uwekezaji wake nchini.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wafanyabiashara na wawekezaji takribani 110 ambapo
waliweza kufahamishwa fursa za biashara kwa bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na fursa za uwekezaji katika
sekta za Miundombinu, Madini, Ujenzi wa majumba, viwanda vya madawa, mitambo ya
viwandani, nguo, Elimu na Afya.
Kutokana na kongamano hilo,
tayari wawekezaji mbalimbali wa India wameonesha nia ya kuwekeza nchini
Tanzania ambapo kundi la kwanza la wawekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa viwanda
vya madawa ya binadamu na vifaa tiba kutoka India, linatarajiwa kutembelea
Tanzania kuanzia tarehe 19 Aprili 2022 ili kukutana na wadau na kuanza taratibu
za kuwekeza Tanzania.
Wafanyabiashara wengine
walioshiriki Kongamano hilo wameonesha nia ya kushiriki maonesho ya 46 ya biashara
ya kimataifa ya Dar es Salaam ambayo yataanza
tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2022. Ushiriki huo utawawezesha kukutana na wafanyabiashara
na kuona bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania.
Kupitia kongamano hilo, wazalishaji
wa bidhaa za Ngozi na korosho wa Tanzania wameunganishwa na wafanyabiashara wa
India ambapo watapata fursa ya kuuza bidhaa hizo katika soko la India.
Sambamba na kongamano hilo, Ubalozi pia ulishiriki
katika hafla ya uzinduzi wa ofisi ya uhamasishaji na uratibu wa biashara na uwekezaji inayojulikana kwa jina la INDIA TANZANIA TRADE COMMISSION (ITTC) iliyopo katika jengo laJJ Diamonds Mart No. 85,
Barabara ya Gopathi Narayanas wani Chetty Chennai katika eneo la Thyagaraya Nagar ambalo ni kitovu cha biashara jijini Chennai. Ofisi hiyo itaongozwa na kusimamiwa na Dkt. J. Shrenik Naharkama Kamishna wabiashara wa
ITTC.
Uwepo wa ITTC utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa
haraka wa taarifa sahihi za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kwa kuwa ITTC itakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na taasisi
zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji za nchini Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akifungua Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India Jijini Chennai, India. |
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya
Tanzania na India wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa kongamano hilo. |
Balozi
wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega akikata utepe na kuwasha mshumaa kuashiria
uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wabiashara na uwekezaji ITTC.
|
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na India katika hafla ya uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wabiashara na uwekezaji ITTC |