Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi.
Mkutano huo ambao unafanyika kwa njia ya mseto (Video na ana kwa ana) pamoja na masuala mengine unatarajiwa kupitia ripoti mbalimbali kama vile; ripoti ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa na Mkutano wa 41 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya, ripoti ya ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ambayo itajumuisha taarifa za Ukaguzi wa Fedha, ripoti ya Mipango na Miundombinu na ripoti ya Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii.
Mkutano huo utakaofanyika kwa kipindi cha siku nne, umeanza katika ngazi ya Maafisa Waandamizi tarehe 8 na 9 Juni 2022, utafuatiwa na Makatibu Wakuu tarehe 10 Juni 2022 na hatimaye tarehe 11 Juni 2022 kuhitimishwa na Mawaziri.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi unaongozwa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi Stephen P. Mbundi, wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kila mwaka, Baraza la Mawaziri la Jumuiya hukutana mara mbili ambapo mkutano mmoja kati ya hiyo hufanyika kabla ya mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya. Miongoni mwa malengo ya Mikutano ya Baraza la Mawazi ni kuhusianisha maamuzi yanayofikiwa kwenye Mikutano ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya na majukumu ya utendaji wa kila siku ya Jumuiya.
Mkutano ukiendelea |
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoendelea jijini Arusha |
Mkutano ukiendelea |