Thursday, October 24, 2024

MHE. PINDA AZUNGUMZA NA VIONGOZI WA SIASA NA VYA KIRAIA BOTSWANA


Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe wake (kulia) wamekutana na Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya African Trust ya jijini Gaborone Bw. Monametsi Sokwe na kusikiliza maoni na mtazamo wake juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu yanavyokwenda nchini humo.



     













 
    




 
 

 

 

 

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe wake wamekutana na Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya African Trust ya jijini Gaborone Bw. Monametsi Sokwe na kusikiliza maoni na mtazamo wake juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu yanavyokwenda nchini humo.

Bw. Sokwe ameshukuru kukutana na SEOM na kusema kuwa vyama vingi ni vichanga na havina nguvu za kifedha kuendesha shughuli zao za kisiasa hasa za kampeni wakati huu wa uchaguzi.

Mhe. Pinda amemuomba Bw. Sokwe na washirika wake kuhakikisha wanaongeza na kuwashirikisha kwa wingi wanawake na vijana katika shughuli za siasa kwani kufanya hivyo ndivyo kunachochea ukuaji wa demokrasia nchini humo.

Katika tukio jingine Mhe. Pinda na ujumbe wake mazungumzo kwa njia ya mtandao na Kiongozi  wa Chama Kipya cha Siasa cha Botswana Republican Party (BRP) Bw. Biggie Butale ambacho kimesimamisha wagombea 10 katika nafasi ya viti vya Bunge la nchi hiyo.

Mhe. Pinda alieleza dhamira ya ujumbe wake kuzungumza na kiongozi huyo kuwa ni kutaka kusikia maoni na mawazo yake kuhusu namna kampeni za vyama vya siasa zinavyoendeshwa na kama mazingira ni mazuri na yanaridhisha kwa nyakati husika.

Bw. Biggie alielezea kuridhishwa kwake na namna shughuli za kuelekea uchaguzi mkuu zinavyoendeshwa na kwamba mazingira yamekuwa salama ila alielezea kutokuridhishwa kwake na wazo la kutoa fedha za uchaguzi kwa vyama vya siasa baada ya uchaguzi na kuongeza kuwa hatua hiyo haitoi nafasi kwa vyama vya siasa kuwa sawa na hivyo kuwapa manufaa vyama vikongwe na vikubwa na kuviacha vyama vichanga njiani.

Tarehe 30 Oktoba, 2024 Wananchi wa Botswana watapiga kura katika Uchaguzi mkuu kuchagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza ya Mitaa ambpo Viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa.

SEOM imepeleka waangalizi wake wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji yote nchini Botswana.


Wednesday, October 23, 2024

BALOZI SHELUKINDO AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA BUNGE LA MAREKANI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Bi. Heather Flynn, Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge (Senate) la Marekani na ujumbe wao wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, leo tarehe 23 Oktoba 2024, amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Bunge la Marekani wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. 

Kupitia mazungumzo hayo wamejadili masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, utalii, demokrasia na utawala bora na ulinzi na usalama. 

Balozi Shelukindo akizungumza na ujumbe huo ulioongozwa na Bi. Heather Flynn, Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge (Senate) la Marekani amewaeleza kuwa hali ya kisiasa nchini ni salama na tulivu. Katibu Mkuu Balozi Shelukindo alisisitiza kuwa hali hiyo inachagizwa na juhudi zinazofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Falsafa ya R4, ambazo ni Maridhiano, Mageuzi, Ustahimilivu na Kujenga upya.

Kwa upande wake Bi. Heather Flynn ameeleza kuridhishwa kwake na mageuzi mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo ameeleza kuwa ni muhimu katika ustawi wa siasa, jamii na uchumi wa Taifa.

Ujumbe wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Marekani ipo nchini kwa ziara ya kikazi, ambapo watakutana na kufanya mazungumzo na watendaji na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Bi. Heather Flynn, Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge (Senate) la Marekani na ujumbe wakifurahia jambo walipokuwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaa.

NAIBU WAZIRI CHUMI AFANYA MAZUNGUMZO NA WABUNGE WA BUNGE LA AFRIKA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Wabunge wa Bunge la Afrika (PAP) katika Ofisi ya Wizara jijini Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2024.

Wabunge hao wa Bunge la Afrika wa Kamati ya Biashara, Forodha na Uhamiaji wapo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku nane (8) yenye lengo la kujionea hatua iliyopigwa na Tanzania katika utekelezaji wa muongozo wa awali wa kufanya Biashara (Guided Trade Initiatives - GTI) wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Akizungumza na wabunge hao naibu Waziri Chumi ameeleza Tanzania imekuwa ikifanya shughuli nyingi za kibiashara ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla kupitia AfCFTA ambapo Tanzania ilichaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 8 za mfano katika utekelezaji wa awali wa kufanya biashara. Nchi nyingine ni Rwanda, Ghana, Egypt, Mauritius,Cameroon na Tunisia.

AfCFTA ni sehemu ya utekelezaji wa Agenda 2063 iliyosainiwa Rwanda mwaka 2018 na Wakuu wa Nchi na Serikali ya Afrika ikiwa na matarajio ya kuwa na mtangamano wa kikanda wenye amani na ustawi.
 Aidha, amefafanua kuwa uratibu wa wafanyabiashara unafanywa na taasisi za biashara mfano taasisi ya sekta binafsi Tanzania, Chama cha wafanya biashara wenye viwanda na wakulima, Chama cha wafanyabiashara wanawake Tanzania na nyingine ambazo zimekuwa zikiratibu na kuwaunganisha na Serikali katika kuwezesha shughuli za kibiashara na kujenga uelewa wa masuala mbalimbali kwa wafanyabishara.

“Elimu kwa umma bado inahitajika katika kujenga uelewa kwa wafanyabiashara ili waweze kutumia fursa za masoko na biashara zinazopatika barani Afrika, hivyo Tanzania inaendelea kujenga uwezo katika hilo ili kuongeza fursa za mazao ya kibishara na taratibu za kufanya biashara” alisema Mhe. Chumi.

Naye, Mkuu wa ujumbe huo wa Wabunge hao na Mbunge wa Kenya, Mhe. Prof. Margaret Kamar  ameeleza kuwa Bunge la Afrika hushirikiana katika utendaji wake na Mawaziri wa Mambo ya Nje barani Afrika katika kuhakikisha malengo na mipango mbalimbali yenye maslahi ya kikanda inafikiwa.

Pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa kufanikiwa kufanya maboresho na mageuzi ya kibiashara hususan katika kuhakikisha inakua na barabara nzuri inayowezesha shughuli za kibiashara baina yake na nchi jirani na bara la Afrika kwa ujumla.

“ Miongoni mwa mikoa tuliyotembelea kabla ya kuja huku Dododma ni mkoa wa Arusha, tumejionea dhahiri namna barabara zilivyoboreshwa na kutuwezesha kutembelea kwa urahisi kila
sehemu tuliyohitaji kutembelea” Mhe. Kamar alisema.

Pia alibainisha kuwa huo ni ushahidi tosha kwa nchi nyingine za Afrika kuona kuwa inawezekana kuiunganisha Afrika kibiashara endapo hatua madhubuti za kufanikisha hilo litapewa mkazo.

Vilevile ameeleza kuwa hatua hizo zilizopigwa zinaonesha kuwa Tanzania ina uwezo wa kupiga hatua zaidi kibiashara na kuzipita kanda nyingine kwakuwa ina nafasi na fursa za kutosha hususan kupitia uwingi wa rasilimali za kibiashara.

Msisitizo mwingine uliotolewa na Wabunge hao wa PAP ni pamoja na suala la uhuru wa watu kutembea baina ya nchi na nchi ambalo kwa upande mwingine linahitaji muongozo kwakuwa kwasasa bado halijielezi vizuri mipaka ya uhuru huo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi ameeleza kuwa Tanzania katika jitihada zake za kuwaunganisha Watanzania kibiashara barani Afrika, imefanikiwa kufanya yafuatayo; uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika, Ujenzi wa miundombinu hususan barabara, reli ya kisasa, kuimarisha shirika la ndege la Tanzania kwa kuongeza ndege ikiwemo ndege za mizigo zenye uwezo kusafiri popote duniani.

Pia Balozi Mbundi ameeleza kuwa GTI imewezesha usafirishaji wa bidhaa za biashara zilizoongezwa thamani ambapo kwa upande wa Tanzania ilianza kuuza bidhaa kama mkonge, kahawa, viungo na karanga.

Kadhalika, ujenzi wa Vituo vya Huduma za Pamoja Mipakani umewezesha kuondoa changamoto nyingi zilizokuwa kikwazo katika biashara na nchi nyingine. Vituo hivyo vimewezesha kuokoa muda kwa wasafirishaji wa bidhaa na wasafiri na kupunguza muda wa kupitisha bidhaa mipakani ambapo maboresho hayo yameenda sambamba na maboresho ya mizani ya kupima mizigo inayotoka bandarini na kuelekea katika nchi jirani.

Hata hivyo, Tanzania ipo katika hatua za mapitio za kutathimini bidhaa nyingine ambazo zitafaa kuingia katika utekelezaji wa Muongozo wa Awali wa kufanya Biashara ili kuona namna gani
inanufaika na soko la AfCFTA.

“Nchi zetu za Afrika zinazalisha bidhaa zinazofanana hivyo ni lazima tathimini yetu ifanyike kwa kina ili kupata bidhaa zenye upekee, tofauti na bidhaa za nchi nyingine na kuleta tija katika maendeleo ya biashara nchini’’ alisisitiza Balozi Mbundi.




Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akizungumza na wabunge wa Bunge la Afrika walipomtembea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 22october 2024.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akichangia mada wakati wa mazunguzo.


Naibu Waziri Mh. Cosato David Chumi akizungumza na sehemu ya wabunge waliokuja nchini kwa ziara ya siku nane.



Picha ya pamoja


Tuesday, October 22, 2024

MHE. PINDA AZINDUA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA JUMUIYA YA MAENDELEO YA KUSINI MWA AFRIKA (SEOM) JIJINI GABORONE

 







 

 

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOM) katika Uchaguzi Mkuu wa Botswana, Mhe. Mizengo Pinda, amezindua misheni hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la SADC la Siasa, Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jijini Gaborone, Botswana.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Pinda aliwasihi wapiga kura wa Botswana kujitokeza kwa kwa wingi kupiga kura tarehe 30 Oktoba 2024, kufanya mamuzi sahihi, kuheshimu mitazamo tofauti ya kisiasa na kuwajibikaji katika kipindi cha baada ya uchaguzi, bila kujali chama au mgombea anayependwa na atakayechaguliwa na wananchi wengi.

 

“Katika siku zilizobaki kuelekea siku hii muhimu kwenu, SADC inawasihi wote kujitokeza kwa wingi, kufanya maamuzi sahihi, kuheshimu mitazamo tofauti ya kisiasa, na kuwajibika katika kipindi cha baada ya uchaguzi, bila kujali chama au mgombea anayependwa atakayechaguliwa na wananchi,” alisema Mhe. Pinda.

 

Alisema SEOM inatekeleza jukumu la uangalizi wa uchaguzi katika nchi wanachama, kwa kuzingatia misingi na miongozo ya SADC ya uchaguzi wa Kidemokrasia, ambayo Nchi Wanachama wa SADC waliridhia kutekeleza.

 

Mhe. Pinda alisema misingi na miongozo hiyo inatoa mbinu za kisayansi na za kimantiki za kuangalia uchaguzi ili kuchangia katika kuimarisha demokrasia katika ukanda huo kwa kuboresha mbinu bora za uchaguzi na kushughulikia kasoro zozote za uchaguzi na kuongeza kuwa misingi na miongozo hiyo pia inategemea nyaraka muhimu za Umoja wa Afrika (AU), kama vile Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi, na Utawala wa mwaka 2007, pamoja na Mikataba husika ya Umoja wa Mataifa (UN).

 

Alifafanua kuwa kwa kufuata masharti ya misingi na miongozo ya SADC inayohusiana na uchaguzi wa kidemokrasia ya mwaka 2021 na mifumo, kanuni, na taratibu za SEAC, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC (SEAC) lilifanya tathmini ya awali ya uwezo wa uchaguzi nchini Botswana tarehe 22 hadi 29 Aprili 2024.

 

Alisema lengo la misheni hiyo lilikuwa kutathmini kama mazingira ya kisiasa na usalama nchini Botswana yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi kwa kufuata kanuni na miongozo, mfumo wa kisheria unaoshughulikia uchaguzi uko katika nafasi, mipaka ya majimbo ilitekelezwa kwa mujibu wa sheria ya nchi, na kama Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ya Botswana iko tayari kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.

 

Aliongeza kuwa wakati huo, misheni hiyo ilifanya mazungumzo na wadau kutoka katika sehemu mbalimbali nchini Botswana, ikiwemo vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, wataalamu wa uchaguzi, mashirika ya dini, na jumuiya ya kidiplomasia.

 

Alisema jukumu la SEOM ni kuangalia kama Nchi Wanachama wanafanya uchaguzi kwa kuzingatia Misingi na Miongozo ya SADC iliyorekebishwa mwaka 2021.

“Tupo hapa kusaidiana kuboresha ubora wa chaguzi zetu na ubora wa harakati zetu za muda mrefu kwa ajili ya uhuru na demokrasia.”

 

Mhe. Pinda alisema SEOM itatoa taarifa yake ya awali kuhusu uchaguzi wa Botswana tarehe Mosi Novemba 2024, na ripoti ya mwisho itawasilishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Botswana siku 30 baada ya uchaguzi.

 

Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi, alisema ndoto ya kubadilisha kanda ya SADC kuwa kanda iliyoungana kikamilifu yenye kuhifadhi ustawi kwa wote inategemea uwezo wake wa kudumisha demokrasia, utawala bora, amani na utulivu na ndoto hiyo itakamilika pale Nchi Wanachama zitakapozingatia na kutekeleza mapendekezo ya SEOM kikamilifu.

 

“Uzingatiaji wa Misingi na Miongozo ya SADC unatarajiwa kuziinua Nchi Mwanachama wa SADC na utafanya kanda hii kufikia Mpango wa Maendeleo wa Kistratejia wa Kanda (RISDP), Dira ya SADC 2050 na Ajenda pana ya Umoja wa Afrika ya 2063 kuhusu Afrika tunayotaka, bila kuacha Nchi Mwanachama au mtu yeyote nyuma,” alisisitiza.

 

Alisema SADC inaendelea kuzihimiza Nchi Wanachama kufikiria utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na misheni mbalimbali za uchaguzi (SEOMs) na kuongeza kuwa SEOM hutoa mapendekezo yake baada ya kuzingatia ripoti za waangalizi wake na mitazamo ya wadau mbalimbali wanaoshirikiana nao katika nchi zinazofanya chaguzi.

 

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya SEOM utachangia na kukuza demokrasia kwa Nchi Wanachama, kuhakikisha utawala bora na kuimarisha imani ya wananchi na wadau wa nje na kusisitiza kuwa uangalizi wa uchaguzi, ambao una gharama kubwa, unafaida na ni kitu cha thamani, na si kitu tu cha kutimiza wajibu na safari rahisi kwa waangalizi.

 

Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa na Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, Wawakilishi wa Serikali ya Botswana, Jumuiya ya wanadiplomasia waliyopo Botswana, Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana (IEC), vyama vya kisiasa, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya Habari na wanahabari, waangalizi wa uchaguzi wa ndani, waangalizi wa kimataifa, vyama vya kiraia na waangalizi wa SADC.

 

SEOM inajumuisha wajumbe 72, kutoka nchi wanachama wa Troika na SEAC, Wajumbe wa Sekretarieti ya SADC, waangalizi wa SEOM ambao wametoka katika Nchi 10 Wanachama wa SADC za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Falme ya Eswatini, Falme ya Lesotho, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri  ya Namibia, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Zambia na Jamhuri ya Zimbabwe ambao watakwenda katika wilaya zote, miji, na majiji makubwa ya Jamhuri ya Botswana.

 

 

 

 


MHESHIMIWA PINDA AKUTANA NA KATIBU MTENDAJI WA SADC JIJINI GABORONE

 

 

Mkuu wa Missoni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Africa (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda (kulia)  akisalimiana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi walipokutana jijini Gaborone, Botswana, kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa.

Mkuu wa Missoni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Africa (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi katika mazungumzo walipokutana jijini Gaborone, Botswana

Mkuu wa Missoni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Africa (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi katika picha walipokutana jijini Gaborone, Botswana

Mkuu wa Missoni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Africa (SADC-SEOM) Mheshimiwa Mizengo Pinda, amekutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi jijini Gaborone , Botswana








MHE. PINDA AKUTANA NA VIONGOZI WA SERIKALI YA BOTSWANA JIJINI GABORONE

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng  alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone.
Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (kulia) akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Mhe. Dkt. Lemongang Kwape hawapo pichani alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Mhe. Dkt. Lemongang Kwape (kulia) akizungumza na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (wa pili kulia)  alipoembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Mhe. Dkt. Lemongang Kwape (wa pili kushoto) na ujumbe wao wakizungumza na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (kulia) na ujumbe wake hawapo pichani alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone


ujumbe wa SEOM ukifuatilia mazungumzo

Mazungumzo yakiendelea
 



Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Mhe. Dkt. Lemongang Kwape alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone.

Mhe. Pinda amekutana na viongozi hao kwa lengo la kujitambulisha kama Mkuu wa Misheni ya SADC na kuwatambulisha wajumbe wa misheni hiyo ambao wako nchini Botswana kwa ajili ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.

Mhe.Pinda aliambatana na  Sekretarieti ya SADC, wajumbe wa SADC Organ TROIKA, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, na Waangalizi wa SADC.

Mhe. Pinda aliwaambia wenyeji wake kwamba SEOM ipo Botswana tayari kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

Mhe. Pinda aliisifu Botswana kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi pamoja na amani na usalama vilivyopo nchini humo, ambavyo vinaifanya Botswana kuwa bora zaidi.

Pia aliwapongeza kwa kuwa wazalishaji wakubwa wa  madini ya almasi na kusaidia watu kutumia madini hayo halisi badala ya almasi bandia.

Kadhalika, aliwaambia wafikirie kuanzisha uzalishaji wa asali na bidhaa zake, kwani wana misitu katika nchi yao ambayo wanaweza kuitumia kama biashara kwa wakulima wao ili wapate kipato.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe. Kabo Morwaeng, aliikaribisha SEOM nchini Botswana na kumhakikishia kwamba Serikali ya Botswana iko tayari kufanya kazi nao na imejipanga vizuri  kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu

“Karibuni Botswana, hii ni nchi ya amani, na tumejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa huru na wa haki kwa kila anayeshiriki,” alisisitiza.

Alisema Serikali ya Botswana imejiandaa kwa uchaguzi mkuu na kwamba wako tayari kwa uchaguzi na kuihakikishia SEOM kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki na kuendelea kudumisha amani na usalama katika nchi yao.

Akizungumza kwenye mkutano, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana, Dkt. Lemongang Kwape, aliahidi kwamba Botswana itafanya Uchaguzi wake kwa amani na itaendelea kushirikiana na wanachama wengine wa SADC kwa manufaa ya wote.

MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI UCHAGUZI YA SADC AKUTANA NA UONGOZI WA JESHI LA POLISI BOTSWANA


Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe wake wakizungumza na Uongozi wa Jeshi la Polisi  nchini Botswana walipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Gaborone kwa ajili ya kujitambulisha .

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda (katikati) akimsikiliza Kiongozi wa Jeshi la Polisi nchini Botswana alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Gaborone kwa ajili ya kujitambulisha .

 

Kamishna wa Polisi nchini Botswana bi. Dinah Marathe (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe wake walipotembelea Makao Makuu ya Polisi  jijini Gaborone kwa ajili ya kujitambulisha .


Maafisa wa Polisi wa Botswana wakimsikiliza Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe (hawako katika picha)

 

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na kuzungumza na uongozi wa Jeshi la Polisi nchini Botswana alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Gaborone.


Mhe. Pinda a
likwenda katika ofisi hizo kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na ujumbe wake ambako alikutana na kuzungumza na Kamishna wa Polisi wa Botswana Bi. Dinah Marathe.

 

Mhe. Pinda na ujumbe wake walitembelea Ofisi za Jeshi la Polisi kwa lengo la kujitambulisha kama Mkuu wa Misheni ya uangalizi ya SADC na ujumbe wa misheni hiyo ambao wako nchini Botswana kwa ajili ya kazi ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu  uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.

Mhe.Pinda aliambatana na Sekretarieti ya SADC, wajumbe wa SADC Organ TROIKA, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, na Waangalizi wa SADC.

Mhe. Pinda aliwaambia
maafisa hao wa Polisi kuwa SEOM ipo nchini Botswana kwa ajili ya kutekeleza jukumu la uangalizi katika uchaguzi huo ambalo wamekabidhiwa na SADC ikiwa ni sehemu ya kukuza na kuimarisha demokrasia katika nchi za ukanda huo.


Mhe. Pinda ali
elezea jinsi  SEOM ilivyojipanga kutekeleza jukumu hilo ambapo wametoa mafunzo kwa waangalizi wao ili wajue taratibu na miongozo ya kufuata wakati wa kutekeleza jukumu hilo.

 

ziara hiyo ya Mhe. Pinda pia ililenga kufahamu jinsi Jeshi la Polisi nchini humo lilivyojipanga kuelekea kwenye uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

 

Akizungumza katika kikao hicho Kamishna wa Polisi wa Botswana Bi. Marathe alimkaribisha Mkuu wa Misheni ya SEOM na ujumbe wake nchini Botswana na kumshukuru kwa kwenda kuwatembelea na kuahidi kushirikiana nao katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa Jumuiya na nchi yao kwa ujumla.

 

Amesema Jeshi la Polisi la Botswana limejipanga kikamilifu kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo unafanyika kwa amani na utulivu na nchi kuendelea kuwa na usalama. 

 

Alisema Botswana ni nchi ya amani na kwamba askari wa nchi hiyo hutembea bila silaha na kuongeza kuwa maafisa wa polisi nchini humo wako tayari kutekeleza kikamilifu majukumu yao katika kipindi chote cha uchaguzi kwa kuendelea kulinda amani,  raia na mali zao.

 

MHE. PINDA AKUTANA NA MABALOZI WA SADC WANAOWAKILISHA NCHI ZAO BOTSWANA

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (katikati amekaa) akizungumza katika kikao na  Mabalozi wa SADC wanaoziwakilisha nchi zao nchini Botswana walipokutana jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024.

 

  Mabalozi wa SADC wanaoziwakilisha nci zao nchini Botswana wakimsikiliza Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (katikati amekaa) walipokutana jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024.

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (katikati amekaa) akiwa na  Mabalozi wa SADC wanaoziwakilisha nci zao nchini Botswana walipokutana jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024.




Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (katikati) akiwa na Balozi wa Angola na Kiongozi wa mabalozi wa SADC nchini Botswana Mhe. Beatriz Morais (kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Botswana Mhe. James Bwana (kushoto) alipokutana kuwaarifu juu ya uwepo wa misheni ya uangalizi wa SADC katika uchaguzi Mkuu wa Botswana ,  jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024.

 

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, (katikati amekaa) akiwa na  Mabalozi wa SADC wanaoziwakilisha nci zao nchini Botswana walipokutana jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024.

 

 

 
 

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na Mabalozi kutoka nchi za SADC wanaoziwakilisha nchi zao nchini Botswana katika kikao kilichofanyika jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Pinda amesema amewaarifu Mabalozi hao juu ya uwepo wake kama Mkuu wa misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya SADC Pamoja na waangalizi wengine kutoka nchi wanachama wa SADC.

Ameeleza kuwa amekutana nao ikiwa ni sehemu ya ratiba zake mbalimbali ili kuwasiliana nao moja kwa moja  na hivyo kusaidia waangalizi kupata picha halisi ya jinsi maandalizi ya uchaguzi huo kwa ujumla yanavyokwenda.

Amesema SEOM imejipanga na iko tayari kutekeleza jukumu lake la Uangalizi kwa ukamilifu kama walivyoaminiwa na Jumuiya na kuwatuma kuifanya kwa niaba yao.

Amesema wao kama viongozi wa SEOM watakuwa na mikutano na watu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kusikiliza na kupata maoni ili kuhakikisha kazi yao ya uangalizi inakwenda vizuri

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi hao Mkuu wa Mabalozi wa SADC nchini Botswana Mheshimiwa Beatriz Morais ameshukuru kukutana na uongozi wa SEOM na kuahidi kushirikiana nao ili  kuhakikisha kazi yao ya uangalizi inafanyika kwa mafanikio na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa Jumuiya na nchi inayohusika.