Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mikutano ya Kamati ya Wataalam uliofuatiwa na Kamati ya Uratibu ya Makatibu Wakuu na Mkutano wa 46 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, pamoja na mambo mengine umemteua Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Novemba 2024 hadi Novemba 2025 akisaidiana na Rais wa Somalia, Mhe. Hassan Sheikh Mohamud.
Aidha, Mkutano huo mbali na kuridhia Lugha za Kiswahili na Kifaransa kuwa Lugha rasmi za EAC zikienda sambamba na Kiingereza pia umezitaka nchi wanachama za Tanzania, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Somalia kukamilisha mashauriano ya kitaifa kuhusu katiba ya shirikisho la kisiasa la EAC ifikapo Juni 30, 2025.
Vilevile, Wakuu hao wa Nchi wameridhia utezi wa Jaji Richard Wejuli Wabwire kutoka Uganda kuwa Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kuanzia mwezi Novemba 2024.
Katika hatua nyingine, wakuu hao wa nchi waliwapongeza wananchi wote wa Nchi wanachama wa EAC kwa kuadhimisha miaka 25 ya Mtangamano wa Kikandana kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika biashara, kudumisha amani na usalama, kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi, kuzalisha bidhaa kibiashara na kulinda mazingira kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuzingatia mageuzi ya kidigiti kama kichocheo muhimu katika kukuza Mtangamano.
Akizungumza, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyeji wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono agenda ya Mtangamano wa Kikanda wa EAC kwani Tanzania inaamini katika Umoja kuliko utengano.
Amesema EAC inasherehekea kutimiza miaka 25, Tanzania itaendelea kuenzi maono ya viongozi waanzilishi wa EAC akiwemo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuhakikisha umoja na undugu unaoziunganisha nchi hizi unadumishwa kwa maslahi ya wananchi wan chi hizo.
Tangu tupate uhuru hadi Muungano neno Umoja ni tunu hapa Tanzania. Hivyo tutaendelea kudumiasha umoja wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwaenzi waanzilishi wa maono haya akiwemo Hayati Mwalimu Nyerere”, alisema Mhe. Rais Samia.
Pia alimpongeza Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni ambaye naye ni mwanzilishi wa Jumuiya hiyo kwa kuendelea kusimamia misingi ya umoja, amani na mshikamano katika Jumuiya ambapo pia alimtakia afya njema na maisha marefu.
“Tunamshukuru Rais Museveni ambaye amekuwa Mwalimu kwetu, msuluhishi na kwa kifupi tunamwita Dean yaani kiongozi wetu katika Jumuiya ambapo kila tunapotaka kuengeuka anaturejesha” alisisitiza Rais Samia.
Mbali na Mhe. Rais Samia, Mhe. Rais Ruto na Mhe. Rais Mohamud, Mkutano huo pia ulimshirikisha Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame na Makamu wa Rais wa Burundi Mhe. Prosper Bazombaza.
Aidha, Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mhe. Veronica Nduva ambaye alishiriki kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo.
Viongozi wengine walioshiriki ni Mawaziri kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji-Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Selemani Jafo na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda-Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban.
Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni akifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha tarehe 30 Novemba 2024 |
Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamesimama kama ishara ya heshima wakati wimbo wa Taifa la Tanzania kama mwenyeji wa mkutano na wibo wa Afrika Mashariki zikiimbwa |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha Novemba 30, 2024 |
Wageni waalikwa wakati wa Mkutano |