Wednesday, January 29, 2025

UGANDA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Robinah Nabbanja amesema Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo na Tanzania hususan kwenye nyanja zinazochochea maendeleo ya wananchi ikiwemo kilimo na biashara.

 

Mhe. Nabbanja ametoa kauli hiyo alipotembelea Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited kilichopo eneo la Nala jijini Dodoma, Januari 29, 2025 ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati kwa niaba ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni uliomalizika jijini Dar es Salaam, Januari 28, 2025.

 

Mhe. Nabbanja ambaye aliwasili jijini Dodoma kwa kutumia usafiri wa Treni ya SGR amesema kuwa, uwekezaji wa kiwanda hicho cha mbolea ni mkombozi kwa wakulima wote wa Afrika Mashariki ambao sasa wanatakiwa kuzalisha mazao yao kwa kutumia mbolea hiyo asilia ambayo inazalishwa kwa utaalam na ubora wa hali ya juu  ili kuongeza uzalishaji wa kibiashara.

 

Pia amesisitiza umuhimu wa Serikali hizi mbili kuendelea kuwekeza kwenye masuala ya kilimo cha umwagiliaji, udhibiti wa magonjwa na wadudu, utafutaji wa mitaji na masoko kwa wakulima, elimu kwa wakulima ya matumizi bora ya mbolea  pamoja na kuingia ubia na wadau mbalimbali hususan kwenye masuala ya teknolojia ya kilimo.

 

“Tanzania na Uganda zimebarikiwa kuwa na ardhi nzuri ya kilimo. Naamini Mwenyezi Mungu alijua ipo siku tutailisha dunia. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunawawezesha wakulima wetu ili walime kwa tija ikiwemo kuwahimiza kutumia mbolea kwa uzalishaji mkubwa wa kibiashara kwa faida zaidi” alisema Mhe. Nabbanja.

 

Aidha, Mhe. Nabbanja aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na sera nzuri inayowawezesha watanzania kuajiriwa kwa wingi kwenye viwanda vya wawekezaji kutoka nje kama ilivyofanyika katika kiwanda hicho cha mbolea ambapo zaidi ya watanzania 800 wameajiriwa kiwandani hapo.

 

Mhe. Nabbanja alitumia nafasi hiyo pia kuelezea furaha yake ya kusafiri kwa kutumia Treni ya Reli ya Kisasa ya SGR na kuahidi kurudi tena Tanzania wakati mwingine ili kufurahia maendeleo makubwa ya miundombinu yanayokamilishwa hapa nchini.

 

“Nimefurahia kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa SGR. Naiushukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzanua kwa hatua hii. Na sisi tayari Mhe. Rais Museveni alizindua mradi huo na tupo katika hatua za mwisho kukamilisha njia ya SGR,” alifafanua Mhe. Nabbanja.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo amemshukuru Mhe. Nabbanja kwa kutembelea kiwanda hicho ili kujionea uwekezaji mkubwa unaofanywa hapa Tanzania na kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuja nchini kwa manufaa ya watanzania.

 

Pia ameongeza kusema,  Mhe. Nabbanja kama kiongozi wa juu wa Uganda  amenonesha nia ya nchi yake kutumia mbolea inayozalishwa kiwandani hapo na kuitaja hatua hiyo kama chachu ya kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda kupitia makubaliano chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na yale ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji  wa Kiwanda hicho, Bw. Nduwimana Nazaire ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha miundombinu muhimu kwa uendeshaji wa kiwanda hicho ikiwemo barabara, maji na umeme inakuwepo na inafanya kazi wakati wote na kwa uhakika.

 

Akitoa neno la shukrani, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Meja Jenerali Paul Simuli ameishukuru Serikali ya Uganda kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata katika kutekeelza majukumu yao nchini humo na kumshukuru Mhe. Nabbanja kwa kutenga muda na kukitembelea kiwanda hicho ili kujionea uzalishaji mkubwa unaofanywa kiwandani hapo.

 

Mbali na Mhe. Jafo, Viongozi wengine wa Serikali walioshiriki ziara hiyo ni pamoja Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.Mhe. Rosemary Senyamule.

 

Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited kilianza uzalishaji rasmi mwaka 2022 ikiwa ni matokeo ya ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi. Kiwanda hicho hadi kufikia mwezi Juni 2025, kina lengo la  kuzalisha Tani milioni moja za mbolea huku kikiajiri zaidi ya Watanzania 800.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo akimpokea Waziri Mkuu wa Uganda, Mhe. Robinah Nabbanja alipowasili katika Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited kilichopo eneo la Nala jijini Dodoma kwa ajili ya kujionea shughuli zinazotekelezwa katika Kiwanda hicho.
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo mara baada ya kuwasili jijini Dodoma

Mhe. Nabbanja akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho
Mhe. Nabbanja akihutubia
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo akizungumza 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Paul Simuli akizungumza 
Mhe. Nabbanja akiwa ameongozana na Mhe. Londo mara baada ya kupokelewa
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited, Bw. Nduwimana Nazaire
Kikundi cha burudani wakati wa mapokezi ya Waziri Mkuu wa Uganda jijini Dodoma
Mhe. Nabbanja akiteta jambo na Viongozi wa Seriklai waliofika kumpokea alipowasili Dodoma akiwemo Mhe. Londo (wa pili kushoto)
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Simuli
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited, Mhe. John Chiligati
Afisa Mambo ya Nje Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Seif Kamtunda akishiriki ziara ya Mhe. Nabbanja
Shehena ya mbolea
Mhe. Nabbanjana wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited
Mhe. Nabbanjana akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited

Mhe. Nabbanjana wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Fredrick Sumaye walipokutana katika Stesheni za SGR jijini Dodoma mara baada ya Mhe. Nabbanja kuwasili
Mhe. Nabbanja akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Dodoma. Aliyesimama pembeni ni Mhe. Londo
Mhe. Nabbanja akipokelewa baada ya kuwasili Dodoma kwa Treni ya SGR
Wageni waalikwa wakishiriki Mkutano wa Mhe. Nabbanja na Viongozi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilzer Limited
Mhe. Nabbanja akizungumza wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited
Shehena ya Mbolea ikipakiwa kwenye lori kabla ya  kusafirishwa kwa ajili ya usambazaji nchini









 

Saturday, January 25, 2025

Rais wa Sierra Leone Awasili nchini














Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone, Mheshimiwa Julius Maada Bio, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, unaotarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha  Kimataifa cha Julius Nyerere kuanzia tarehe 27 hadi 28 Januari 2025.


Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mheshimiwa Rais Bio amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo.


Mheshimiwa Rais Bio ni Rais wa kwanza kuwasili nchini kwa ajili ya mkutano huo ambao jumla ya Marais 25 kutoka nchi za Afrika aanatarajiwa kuja nchini kushiriki mkutano huo.


Mkutano huu wa kihistoria unalenga kuimarisha juhudi za pamoja katika kukabiliana na changamoto na fursa za nishati barani Afrika, sambamba na kupitisha Azimio la Dar es Salaam, linalosisitiza dhamira ya Viongozi wa Nchi na Serikali za Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu barani Afrika.







 

RAIS SAMIA AVUNJA RIKODI, MKUTANO WA NISHATI.

Idadi ya Wakuu wa Nchi watakaoshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliopangwa kufanyika nchini Januari 27 na 28, 2025 ni rikodi nyingine kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Wakuu wa Nchi 25 na Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Naibu Mawaziri Wakuu 10 inafanya idadi ya viongozi wa ngazi ya juu 35 ambao Tanzania tokea izaliwe haijawahi kupokea idadi kubwa ya viongozi kama hao katika tukio moja.

“Tulipokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999 na Wakuu wa Nchi 15 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019, mkiangalia idadi ya Wakuu wa Nchi katika mkutano huu ni kubwa ukilinganisha na matukio hayo mawili yaliyopita” Balozi Kombo alisema. 

Alizitaja nchi ambazo Wakuu wa Nchi zao zimethibitisha kushiriki kuwa ni Pamoja na; Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon. 

Makamu wa Rais watakaoshiriki ni kutoka Gambia na Benin. Mawaziri Wakuu kutoka Cote d’Ivoire, Uganda, São Tomé and Príncipe na Equatorial Guinea na Naibu Mawaziri Wakuu ni kutoka Eswatine na Namibia.

Waziri Kombo amesema mkutano huo ni mwendelezo wa matunda ya diplomasia ya Tanzania ambapo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutangazika barani Afrika na duniani kwa ujumla. 

Amesema mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil Novemba 2024 na Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) na kupewa na nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Bara la Afrika ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kuimarika duniani.

Ameendelea kueleza kuwa mikutano hiyo ina faida kubwa kwenye Uchumi wa nchi hususan sekta ya utalii na makundi mbalimbali ya wajasiriamali kama boda boda, hoteli na mama lishe.

Waziri Kombo amemalizia kwa kuwashukuru waandishi wa habari kwa kazi nzuri ya kuelimisha umma na kuwasihi kazi yao hiyo inahitajika zaidi katika mkutano huu mkubwa kuwahi kufanyika nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati utakaofanyika Januari 27-28, 2025.