Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Robinah Nabbanja amesema Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo na Tanzania hususan kwenye nyanja zinazochochea maendeleo ya wananchi ikiwemo kilimo na biashara.
Mhe. Nabbanja ametoa kauli hiyo alipotembelea Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited kilichopo eneo la Nala jijini Dodoma, Januari 29, 2025 ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati kwa niaba ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni uliomalizika jijini Dar es Salaam, Januari 28, 2025.
Mhe. Nabbanja ambaye aliwasili jijini Dodoma kwa kutumia usafiri wa Treni ya SGR amesema kuwa, uwekezaji wa kiwanda hicho cha mbolea ni mkombozi kwa wakulima wote wa Afrika Mashariki ambao sasa wanatakiwa kuzalisha mazao yao kwa kutumia mbolea hiyo asilia ambayo inazalishwa kwa utaalam na ubora wa hali ya juu ili kuongeza uzalishaji wa kibiashara.
Pia amesisitiza umuhimu wa Serikali hizi mbili kuendelea kuwekeza kwenye masuala ya kilimo cha umwagiliaji, udhibiti wa magonjwa na wadudu, utafutaji wa mitaji na masoko kwa wakulima, elimu kwa wakulima ya matumizi bora ya mbolea pamoja na kuingia ubia na wadau mbalimbali hususan kwenye masuala ya teknolojia ya kilimo.
“Tanzania na Uganda zimebarikiwa kuwa na ardhi nzuri ya kilimo. Naamini Mwenyezi Mungu alijua ipo siku tutailisha dunia. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunawawezesha wakulima wetu ili walime kwa tija ikiwemo kuwahimiza kutumia mbolea kwa uzalishaji mkubwa wa kibiashara kwa faida zaidi” alisema Mhe. Nabbanja.
Aidha, Mhe. Nabbanja aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na sera nzuri inayowawezesha watanzania kuajiriwa kwa wingi kwenye viwanda vya wawekezaji kutoka nje kama ilivyofanyika katika kiwanda hicho cha mbolea ambapo zaidi ya watanzania 800 wameajiriwa kiwandani hapo.
Mhe. Nabbanja alitumia nafasi hiyo pia kuelezea furaha yake ya kusafiri kwa kutumia Treni ya Reli ya Kisasa ya SGR na kuahidi kurudi tena Tanzania wakati mwingine ili kufurahia maendeleo makubwa ya miundombinu yanayokamilishwa hapa nchini.
“Nimefurahia kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa SGR. Naiushukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzanua kwa hatua hii. Na sisi tayari Mhe. Rais Museveni alizindua mradi huo na tupo katika hatua za mwisho kukamilisha njia ya SGR,” alifafanua Mhe. Nabbanja.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo amemshukuru Mhe. Nabbanja kwa kutembelea kiwanda hicho ili kujionea uwekezaji mkubwa unaofanywa hapa Tanzania na kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuja nchini kwa manufaa ya watanzania.
Pia ameongeza kusema, Mhe. Nabbanja kama kiongozi wa juu wa Uganda amenonesha nia ya nchi yake kutumia mbolea inayozalishwa kiwandani hapo na kuitaja hatua hiyo kama chachu ya kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda kupitia makubaliano chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na yale ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Nduwimana Nazaire ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha miundombinu muhimu kwa uendeshaji wa kiwanda hicho ikiwemo barabara, maji na umeme inakuwepo na inafanya kazi wakati wote na kwa uhakika.
Akitoa neno la shukrani, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Meja Jenerali Paul Simuli ameishukuru Serikali ya Uganda kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata katika kutekeelza majukumu yao nchini humo na kumshukuru Mhe. Nabbanja kwa kutenga muda na kukitembelea kiwanda hicho ili kujionea uzalishaji mkubwa unaofanywa kiwandani hapo.
Mbali na Mhe. Jafo, Viongozi wengine wa Serikali walioshiriki ziara hiyo ni pamoja Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.Mhe. Rosemary Senyamule.
Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited kilianza uzalishaji rasmi mwaka 2022 ikiwa ni matokeo ya ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi. Kiwanda hicho hadi kufikia mwezi Juni 2025, kina lengo la kuzalisha Tani milioni moja za mbolea huku kikiajiri zaidi ya Watanzania 800.
![]() |
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo mara baada ya kuwasili jijini Dodoma |
![]() |
Mhe. Nabbanja akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho |
![]() |
Mhe. Nabbanja akihutubia |
![]() | |
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo akizungumza |
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza |
![]() | |
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Paul Simuli akizungumza |
![]() |
Mhe. Nabbanja akiwa ameongozana na Mhe. Londo mara baada ya kupokelewa |
![]() |
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited, Bw. Nduwimana
Nazaire |
![]() |
Kikundi cha burudani wakati wa mapokezi ya Waziri Mkuu wa Uganda jijini Dodoma |
![]() |
Mhe. Nabbanja akiteta jambo na Viongozi wa Seriklai waliofika kumpokea alipowasili Dodoma akiwemo Mhe. Londo (wa pili kushoto) |
![]() |
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited, Mhe. John Chiligati |
![]() |
Afisa Mambo ya Nje Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Seif Kamtunda akishiriki ziara ya Mhe. Nabbanja |
![]() |
Shehena ya mbolea |
![]() | |
|
![]() | |
|
![]() |
Mhe. Nabbanjana wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited |
![]() |
Mhe. Nabbanja akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Fredrick Sumaye walipokutana katika Stesheni za SGR jijini Dodoma mara baada ya Mhe. Nabbanja kuwasili |
![]() |
Mhe. Nabbanja akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Dodoma. Aliyesimama pembeni ni Mhe. Londo |
![]() |
Mhe. Nabbanja akipokelewa baada ya kuwasili Dodoma kwa Treni ya SGR |
![]() |
Wageni waalikwa wakishiriki Mkutano wa Mhe. Nabbanja na Viongozi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilzer Limited |
![]() |
Mhe. Nabbanja akizungumza wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited |