Wednesday, February 26, 2025

WAZIRI KOMBO AWASILI MALAWI KUHUDHURIA MKUTANO WA SITA WA JPCC.

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb)


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amewasili jijini Lilongwe, Malawi, kushiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi. 

Mkutano huo wa ngazi ya mawaziri utafanyika tarehe 26 Februari 2025, ukiwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kiuchumi kati ya Tanzania na Malawi. 

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Banda jijini Lilongwe Mhe. Kombo amepokewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Patricia Nangozo Kainga (Mb), na Balozi wa Tanzania Malawi, Mhe. Agnes Kayola. 

Mkutano wa Sita wa JPCC utajadili masuala muhimu ya kuendelea kuimarisha Ushirikiano kupitia sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, elimu, afya, ulinzi na usalama, pamoja na fursa zinazopatikana kwenye maeneo ya ushirikiano katika sekta za kipaumbele.

Mkutano huo pia, utafanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto mbalimbali.

Viongozi wa pande zote mbili wanatarajiwa kusaini makubaliano mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya Mataifa yote mawili.

 

 




                          Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Patricia Nangozo Kainga.

Tuesday, February 25, 2025

MKUTANO WA JPCC KUJADILI USHIRIKIANO KATIKA NYANJA ZA KIMKAKATI WAANZA NCHINI MALAWI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa JPCC kwenye ngazi ya Maafisa Waandamizi.

 

Maafisa waandamizi wa Tanzania na Malawi wamekutana jijini Lilongwe, Malawi, katika kikao cha sita cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC), kujadili masuala ya kimkakati yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kijamii na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Kikao hicho, kilichoongozwa na wenyeviti wenza, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Said Shaib Mussa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Malawi, Balozi Mwayiwayo Polepole, ni hatua muhimu katika kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita na kuibua fursa mpya za ushirikiano.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi Mussa alipongeza jitihada za pande zote mbili katika kudumisha ushirikiano wa muda mrefu na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiusalama kwa maendeleo ya kikanda.

Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kujadili kwa kina sekta muhimu zinazogusa maendeleo na ustawi wa Mataifa haya mawili na kikanda kwa ujumla. Maeneo hayo ameyataja kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara hasa za mipakani, uendelezaji wa miundombinu ya usafiri, ushirikiano katika sekta ya nishati na kuimarisha mwingiliano wa watu.

"Ni muhimu tushiriki majadiliano haya kwa mtazamo chanya na ari ya ushirikiano, kwani maendeleo ya kiuchumi, usalama wa kikanda, na ustawi wa jamii yanaweza kupatikana tu kupitia mshikamano wa kweli.” Alisema Balozi Mussa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho na Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi, Balozi Polepole alisema kuwa kikao hicho kinatoa fursa adhimu ya kujadili masuala muhimu ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pamoja na masuala mengine, kikao hicho kimeangazia nyanja za diplomasia na siasa, ulinzi na usalama, masuala ya uchumi, miundombinu na mawasiliano, pamoja na masuala ya kijamii na kibinadamu.

Kikao hichi ni maandalizi ya Mkutano wa Sita wa Tume ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na Jamhuri ya Malawi ngazi ya Mawaziri, unaotarajiwa kufanyika Februari 26, 2025.

 

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa

                Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Malawi, Balozi Mwayiwayo Mclloyd Polepole

 

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (kushoto) na
                Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Malawi, Balozi Mwayiwayo Mclloyd Polepole (kulia)
 
 

 
 

 




 










                                                                 Picha ya pamoja.

Monday, February 24, 2025

BALOZI MUSSA AKAGUA MAJENGO YA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI.

       Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya miradi wa wizara, Balozi Said Shaib Mussa akiwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Balozi Agnes Richard Kayola wakikagua kiwanja cha ubalozi huo.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya miradi ya Wizara, Balozi Said Shaib Mussa, ametembelea majengo ya Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi na kukagua kiwanja cha Ubalozi huo jijini Lilongwe.

Katika ziara hiyo, Balozi Mussa aliwaambia Watumishi wa Ubalozi huo kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na miundombinu bora katika ofisi zake za uwakilishi  nje ya nchi na kufafanua kuwa licha ya changamoto ya ufinyu wa bajeti, Serikali ina dhamira ya dhati ya kukarabati na kuimarisha majengo hayo ili yawe katika viwango vinavyostahili.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa ubalozi na kuhakikisha mali zake zinatumika kwa tija.  

Aidha, Balozi Mussa alitembelea pia kiwanja kinachomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Malawi na kutoa wito wa kukitumia kiwanja hicho kwa njia inayoweza kuleta manufaa kwa Taifa.

Alibainisha kuwa kuna fursa ya kukiendeleza kiwanja hicho kwa kujenga miundombinu ikiwemo majengo ya biashara au makazi ya kupangisha, jambo ambalo litaongeza mapato ya serikali na kunufaisha Tanzania kwa ujumla.  

Balozi Mussa amempongeza  Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola  na watumishi wa Ubalozi huo kwa kazi  kubwa wanayofanya ya kuiwakilisha nchi na kusimamia maslahi ya Watanzania wanaoishi na kufanya shughuli zao nchini humo.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa tija na ufanisi.  

Balozi Mussa yupo nchini Malawi kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi utakaofanyika Februari 25, 2025 katika ngazi ya Maafisa Waandamizi, na Mkutano ngazi ya Mawaziri  unatarajiwa kufanyika Februari 26, 2025.





 

UJUMBE WA TANZANIA NCHINI MALAWI WASISITIZWA KUTUMIA JUKWAA LA JPCC KUIBUA MAENEO YENYE TIJA YA USHIRIKIANO.



           Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akizungumza na ujumbe wa Tanzania nchini Malawi.

 

Ujumbe wa Tanzania utakaoshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi wamesisitizwa kutumia Mkutano huo kuibua na kuendeleza maeneo muhimu ya Ushirikiano yenye manufaa kwa mataifa hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, alipowasili jijini Lilongwe, Malawi na kuzungumza na ujumbe wa Tanzania katika kikao kilichofanyika katika makazi ya balozi wa Tanzania nchini humo.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mussa alisisitiza kuwa Mkutano huo ni fursa muhimu ya kuboresha uhusiano wa pande zote mbili kwa faida ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.

Aliwasihi wajumbe wa Tanzania kuwa mstari wa mbele kuwasilisha hoja zenye manufaa kwa Tanzania.

"Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kutambua malengo ya safari hii na kuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya nchi kwa kuzingatia maeneo muhimu hususan biashara, miundombinu, amani na usalama, kilimo, viwanda, nishati na gesi hivyo ni kuhakikisha hoja hizi zinazingatiwa," alisema Balozi Mussa.

Aidha, amefafanua kuwa mkutano huo pia utatoa fursa kwa pande zote mbili kupitia makubaliano yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita na kutathmini utekelezaji wake, pamoja na kuweka mikakati mipya ya ushirikiano kwa kuzingatia kipaumbele maalum kwenye maeneo mbalimbali hususan diplomasia, Siasa, uchumi, miundombinu na mawasiliano, masuala ya kijamii na kibinadamu, ulinzi na usalama pamoja na utatuzi wa changamoto za kikanda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Malawi kuanzia tarehe 25 ambapo atashiriki mkutano ngazi ya Mawaziri wa Sita wa Tume ya kudumu ya pamoja ya ushrikiano kati ya Tanzania na Malawi utakaofanyika tarehe 26 Februari 2025. Mkutano huo utatanguliwa na vikao vya Maafisa Waandamizi vitakavyofanyika tarehe 24 na 25 Februari 2025.

 

 




Balozi wa Tanzania nchini Malawi ,Mhe. Agness Richard Kayola akitoa hoja katika kikao hicho.

 


                     Mkurugenzi wa idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki Balozi Ali Sakila Bujiku akichangia mada.











.