Monday, August 23, 2021

WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA KENYA KWA MAZUNGUMZO YA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula leo tarehe 23 Agosti 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Raychelle Omamo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili nchini humo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Katika mazungumzo hayo ambayo yamefanyika kwenye Hoteli ya Movenpick jijini Nairobi, Mhe. Balozi Mulamula amemshukuru Mwenyeji wake kwa mwaliko na kumweleza kwamba mwaliko huo umekuja wakati muafaka ili kuwawezesha kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza maagizo ya Viongozi Wakuu wa Nchi hizi mbili waliyoyatoa wakati wa ziara ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Aliongeza kuwa, hadi sasa yapo masuala mbalimbali ambayo yameendelea kutekelezwa na nchi hizi mbili kufuatia maagizo hayo ikiwa ni pamoja kufanyika kwa mkutano wa Mawaziri wa Biashara wa nchi hizi mbili mwezi Julai 2021 ambapo kwa pamoja waliweza kujadili na kutatua changamoto kadhaa za ufanyaji biashara ikiwemo kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 30 kati ya 60 vilivyokuwa vinazikabili nchini hizi mbili. Masuala mengine yanayotekelezwa yanagusa sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, mifugo na uvuvi.

Kadhalika, alisema kuwa nchi hizi mbili zina mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mmoja hivyo uangaliwe utaratibu mzuri wa kuwezesha ubadilishanaji wa program mbalimbali za elimu na mafunzo zitakazowahusisha vijana ili kuwajengea uwezo kwenye maeneo mbalimbali ya utaalam ikiwemo nyanja za diplomasia. 

Kuhusu ufanyaji biashara, Mhe. Balozi Mulamula alishukuru kwamba urari wa biashara kati ya Tanzania na Kenya sasa unakwenda vizuri na alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Kenya kuendelea kuweka mazingira ambayo yatawawezesha watanzania wengi zaidi kuwekeza nchini humo kama ilivyo kwa kampuni nyingi za Kenya ambazo zimewekeza Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Balozi Omamo alimshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kukubali mwaliko wake na kwamba kitendo hicho ni heshima kubwa kwao na kusisitiza kuwa ushirikiano huo wa kihistoria uendelee kwa kuanzisha mikutano ya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili masuala muhimu yenye manufaa kwa nchi hizi mbili. 

Pia alipongeza ukuaji wa biashara unaoendelea kati ya nchi hizi mbili na kueleza kuwa Tanzania na Kenya zina fursa nyingi za kushirikiana na kinachotakiwa ni kuendelea kutekeleza kikamilifu masuala yote ambayo tayari yamekubalika kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili. 

Wakati huohuo, Mhe. Balozi Mulamula amezungumza na Maafisa Mambo ya Nje Wanawake Vijana wa Kenya kupitia Mpango wa Azizi ambapo amewataka Maafisa hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu kazi na mamlaka, kuwa wavumilivu na kufuata misingi ya kazi ili kufikia malengo ya juu ya kazi zao kwa manufaa yao ya baadaye na nchi kwa ujumla. 

“Ili kufikia malengo ya juu ya kazi yako kuna mambo mengi ya kutekeleza. Uvumilivu, heshima, kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na wengine na umaridadi ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatia ili kufikia malengo hayo” alisisitiza Waziri Mulamula.

Waziri Mulamula alitumia nafasi hiyo kuwaeleza Maafisa hao hatua mbalimbali alizopitia hadi kufikia nafasi hiyo ikiwemo kuajiriwa kama Afisa Mambo ya Nje Daraja la Tatu, kuwa Katibu Mtendaji wa Kwanza wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki hadi kuteuliwa katika wadhifa wa Waziri mwaka 2021.

Katika hatua nyingine, Mhe. Balozi Mulamula amekitembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya na kutoa mhadhara wenye mada isemayo “Mtazamo wa Tanzania kwenye Agenda ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama” kwa Washiriki 62 kutoka Nchi 15 za Afrika, Ulaya na Asia waliohudhuria mhadhara huo.

Katika maelezo yake, Mhe. Balozi Mulamula ambaye amewahi kukitembelea Chuo hicho miaka 10 iliyopita alisema wanawake wana nafasi na umuhimu mkubwa wa kushirikishwa katika masuala ya amani na usalama tangu ngazi ya familia hadi kimataifa kwani wao ndio walezi wakuu wa familia hususan pale amani inapotoweka.

Alieleza kuwa, pamoja na kuwepo kwa mikataba ya kitaifa, kikanda na kimataifa inayotambua umuhimu wa ushirikishwaji wanawake kwenye masuala ya kulinda amani na utatuzi wa migogoro bado ushirikishwaji huo haujapewa kipaumbele ukilinganisha na ule wa wanaume. 

Akizungumzia nafasi ya Tanzania, alisema kuwa, kwa kiasi fulani Tanzania imepiga hatua kwenye masuala kadhaa ya kuwainua wanawake hususan kwenye agenda ya amani na usalama ambapo tayari mikataba kadhaa inayotambua ushirikishaji wanawake imesainiwa ukiwemo Mkataba wa Beijing. 

Pia alisema kwamba, Tanzania imeendelea kuchangia vikosi vya ulinzi wa amani kwenye nchini mbalimbali duniani ambapo hadi sasa Tanzania ina takribani wanajeshi 1,759 waliopelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya kulinda amani ambapo kati ya hao 149 ni wanawake.

Mhe. Waziri Mulamula ambaye yupo nchini Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili pia anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya utakaofanyika kwa ngazi ya Mawaziri tarehe 24 Agosti 2021. Ujumbe wa Tanzania pia unawahusisha Mawaziri kadhaa pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka sekta mbalimbali.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo yaliyofanyika jijini Nairobi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo jijini Nairobi.

 

Mazunguzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo wakiwa katika picha ya pamoja

Kutoka kushoto; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (Mb) na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwasili katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha nchini Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akivishwa beji maalum na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Mhe. Dkt. Monika Juma, kama ishara ya kutambua mchango wake katika masuala ya amani na usalama  alipotembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha nchini Kenya 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeji wake alipotembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa ameambatana na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Mhe. Dkt. Monika Juma (kushoto) walipowasili katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha nchini Kenya
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akielezea jambo wakati akitoa Mhadhara kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa mhadhara katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeji wake alipotembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa mhadhara kwa Maafisa Mambo ya Nje Wanawake Vijana wa Kenya, jijini Nairobi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo jijini Nairobi wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Mambo ya Nje Wanawake Vijana wa Kenya.

Sunday, August 22, 2021

WAZIRI MULAMULA KUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA NNE WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA KENYA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Commission for Cooperation-JCC) kati ya Tanzania na Kenya unaofanyika jijini Nairobi kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti, 2021.

Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mhe. Balozi Mulamula anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Balozi Raychelle Omamo tarehe 23 Agosti 2021 pamoja na kutembelea Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Kenya ambapo atatoa mhadhara kwa mada isemayo “Mtazamo wa Tanzania kwenye Agenda ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama”. 

Kadhalika wakati wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Hati tatu (3) za Makubaliano zitasainiwa ambazo ni:- Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia baina ya Nchi hizi mbili. Kusainiwa kwa makubaliano haya kutaendeleza na kuimarisha mahusiano mazuri ya kisiasa na kidiplomasia yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya. 

Hati nyingine itakayosainiwa ni kuhusu Uhakiki wa Mpaka kati ya Tanzani na Kenya. Kusainiwa kwa Hati hiyo kutazipa Nchi zote mbili msingi wa kisheria wa kuhakiki mpaka uliowekwa na wakoloni kwa kuuimarisha na kuweka alama zinazoonekana ili kuondoa mwingiliano wa jamii za mpakani na hivyo kupunguza migogoro ya mara kwa mara.

Mwisho ni Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia. Hati hii inalenga kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote katika maeneo ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ili kuleta manufaa kwa nchi zote katika kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa masuala ya elimu ya juu, Sayansi na teknolojia kwa pande zote. 

Mkutano huu ulioanza katika ngazi ya wataalam tarehe 19 hadi 22 Agosti 2021, umeongozwa na Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huku upande wa Kenya ukiongozwa na Balozi George Orina, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Umoja wa Afrika.

Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Wataalam umejadili agenda mbalimbali za ushirikiano ambazo zitawasilishwa kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 23 Agosti 2021 kabla ya Mkutano wa Nne wa Tume ya Ushirikiano kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 24 Agosti 2021. 

Tanzania na Kenya zimeendelea kutekeleza masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, siasa na diplomasia, elimu, uhamiaji, utalii, kazi, afya, usafirishaji, ulinzi na usalama. 

Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ilianzishwa rasmi mwezi Septemba 2009 jijini Arusha, Tanzania na kufuatiwa na Mkutano wa Kwanza wa Tume hiyo uliofanyika jijini hapo mwaka 2009. Mkutano wa Pili wa Tume hiyo ulifanyika jijini Nairobi, Kenya mwezi Septemba 2012 na Mkutano wa Tatu ulifanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016.

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walipokutana wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Balozi Naimi S.H. Azizi, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Wataalam uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Movenpick jijini Nairobi, Kenya.

 

Meza Kuu; Balozi Naimi S.H. Azizi (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Tanzania, na Balozi George Orina Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Umoja wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje Kenya, wakifuatilia Mkutano.

Sehemu ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakijadili jambo kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliokuwa ukiendelea.

Mkutano ukiendelea

Bw. Paul Makelele Afisa Sheria wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichangia jambo kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliokuwa ukiendelea.
Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ukiendelea.

Friday, August 20, 2021

MKUTANO WA NNE WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA KENYA WAFANYIKA NAIROBI, KENYA.


Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya umeanza kufanyika leo tarehe 19 Agosti 2021 Jijini Nairobi, Kenya. Mkutano huu utakaofanyika kwa kipindi cha siku sita kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti, 2021 unalenga kujadili mambo mbalimbali muhimu ya ushirikiano ikiwemo Mahusiano ya Kidiplomasia, Ulinzi na Utawala Bora, Uchumi na Biashara, na Masuala ya Kijamii sambamba na kuibua maeneo mapya ya ushikiano kwa lengo la kuchagiza maendeleo baina ya Tanzania na Kenya. 

Mkutano huu muhimu katika ustawi wa ushirikiano na maendeleo baina ya mataifa haya mawili, unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ziara yake aliyoifanya Nchini Kenya mwezi Mei, 2021, kuwa Nchi hizi mbili zifanye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo katika ngazi ya Wataalamu, Balozi Naimi S.H. Azizi, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amebainisha kuwa mkutano huo umetoa fursa hadhimu kwa pande zote mbili kukutana ili kuweka mipango na mikakati ya pamoja itakayoimarisha ushirikiano kwenye utekelezaji wa vipaumbele vya shughuli za maendeleo katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili. “Natambua vyema kuwa tokea Mkutano wa Mwisho wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ulipofanyika, mengi mazuri yamefanyika baina ya Nchi zetu (Tanzania na Kenya) na kwa kupitia miogozo ya Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mathalani nilifarijka sana pale timu yetu ya Wataalamu ya Pamoja ya kudhibiti Mipaka ilipofanya Mkutano wao kwa mafanikio Juni 2021, Jijini Mombasa, Kenya. Hili linaendelea kudhihirisha utayari wa Serikali zetu wa kudumisha amani na kuleta maendeleo”. Alisema Balozi Naimi S.H. Azizi. 

Balozi Naimi S.H. Azizi aliongeza kusema kuwa ni muhimu wajumbe wa mkutano wajikite katika kujadili masuala muhimu yenye maslahi kwa pande zote mbili ili kukidhi matarajio ya Wakuu wa Nchi hizi mbili, ya kuona Wataalamu katika Serikali wanazoziongoza wanaendelea kuwajibika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo wananchi. 

Mkutano huu umejumuisha Viongozi, Watendaji na Maafisa mbalimbali wa Serikali kutoka Tanzania na Kenya. 

Balozi Naimi S.H. Azizi (kulia) Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya   Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliokuwa ukiendela katika Hoteli ya Movenpick Jijini Nairobi, Kenya. 
Balozi Naimi S.H. Azizi Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya unofanyika Jijini Nairobi Kenya
Balozi wa Tanzania Nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene akifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliokuwa ukiendela katika Hoteli ya Movenpic Jijini Nairobi, Kenya.
Meza Kuu wakifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliokuwa ukiendela katika Hoteli ya Movenpick Jijini Nairobi, Kenya
Sehemu ya Wajumbe kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliokuwa ukiendela katika Hoteli ya Movenpick Jijini Nairobi, Kenya

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ukiendelea.

Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya unaendelea Jijini Nairobi, Kenya wakiwa katika picha ya pamoja.
Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ukiendelea.
Mhe. Ababu Namwamba, Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya unofanyika Jijini Nairobi Kenya