Wednesday, October 3, 2012

VIFO VYA AKINA MAMA HAVIVUMILIKI-JK‏



Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa katika picha ya pamoja na  Bw. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mjini New York, nchini Marekani.  Rais Kikwete alikutana na Bw. Ki-moon kwa ajili ya mazungumzo ya namna kuendeleza ushirikiano, hususan katika masuala ya Mama na Watoto.


Mhe. Rais Kikwete akisaini kitabu cha wageni. 


Mhe. Rais Kikwete (wa tatu kushoto), akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon.  Wengine ni wajumbe kutoka pande zote mbili, Tanzania ikiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Y. Sefue (wa nne kushoto), Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa kwanza kushoto), Afisa Mwandamizi wa Rais Kikwete (masuala ya diplomasia), Mhe. Balozi Tuvako Manongi (wa pili kushoto), Mwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Ndugu Prosper Mbena (wa tano kushoto), Msaidizi wa Rais Kikwete.  Wengineo ni Wajumbe kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon, mara baada ya mazungumzo yao mjini New York.




VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI HAVIKUBALIKI- JK

Na MAURA MWINGIRA, New York
2 Oktoba, 2012
Rais Jakaya Mrisho Kikwete  amesema,  vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo wakati  wakujifungua havipaswi kutokea na havikubaliki.
Na kwa sababu hiyo, anasema juhudi zaidi zinahitajika katika kubabiliana na hali hiyo na hasa ikizingatia kwamba   sababu zinazosabisha kutokea kwa vifo hivyo zinazuilika.

“ Vifo vya wanawake wajawazito havikubaliki” akasema na kuongeza “ na ndiyo kwasababu tunahitaji kuongeza  juhudi zaidi kuokoa maisha ya wanawake, kwa sababu si haki na si jambo jema kwa mwanamke kufa wakati wa kujifungua , si haki afe wakati akimleta kiumbe mwingine duniani, na cha kusikitisha zaidi wanakufa kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika”, akasisitiza Rais Kikwete.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa  awamu ya pili ya mpango wa ubunifu wa uboreshaji wa huduma ya  afya ya mama na mtoto katika maeneo ambayo huduma hiyo haipatikani kwa urahisi nchini Tanzania.

Uzinduzi wa mpango huo umefanyika mbele ya waandishi wa habari siku ya  jumanne  hapa  Makao Uakuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki  Moon, Rais Jakaya kikwete na wafadhili wakuu wa mpango huo ambao ni Meya wa Jiji la New  York  na philanthropist Michael Bloomberg na Dkt. Helen Agerup, Mkuu  wa Mfuko wa  H&B Agerup.

Wafadhili hao wawili wametoa dola za kimarekani  milioni 15 kufadhili huduma za uboreshaji wa vituo vya afya,  na mafunzo ya huduma za upasuaji wa dhararu kwa  waganga,  wakunga na manesi lengo likiwa ni kuokoa maisha ya wanawake wanapojifungua na kupunguza umbali wa  kuifuata huduma hiyo.

Rais Kikwete amesema kwamba, uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto na afya kwa ujumla  ni moja ya vipa umbele  vyake muhimu na ni jambo lililo ndani ya moyo wake.

“Tumefanya mengi na tunaendelea kufanya, lakini tunahitaji kuongeza kasi ya juhudi hizi,  uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto ni kupaumbele changu ni jambo lililo moyoni mwangu na tunapopata wafadhilli kama nyinyi kuchangia juhudi zetu tunafarijika zaidi na kutiwa moyo na tunawashukuru” akasema Rais.

Naye  katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kupigania nakutetea  haki za wanawake na watoto, amesisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi kuokoa maisha ya wanawake na watoto kwa kuboresha huduma zao.

“Tunahitaji marais, mameya, wanaharakatiwa   kuboresha huduma za afya na wafanyakazi wa afya hadi ngazi ya chini kabisa. Leo tunashuhudia matokeo ya ushirikiano huu ambapo kwa ushirikiano wa viongozi watatu tumeweza katika kipindi cha miaka miwili  kupunguza kwa  asilimia kubwa vifo vya wanawake wajawazito katika  maeneo ya mikoa ya Kigoma,  Morogoro na Pwani ambako mpango huu wa ubunifu umekuwa ukitekelezwa” akabainisha Ban ki Moon.

Aidha  Ban Ki Moon amemuelezea  Rais Jakaya kikwete kama  mmoja wa viongozi  wa kwanza duniani kuungua mkono mkakati wa Kimataifa kuhusu Afya ya mama wajawazito na watoto, mpango uliozinduliwa mwaka 2010 ambapo kiasi cha  dola milioni 400 zitaelekezwa katika  uboreshaiji wa huduma hizo. Na ni   mpango unaokwenda sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo  Millenia ( MDGs).

Kwa upande wake Meya na philanthropies Michael Bloomberg  akizungumza  kwenye uzinduzi huo anasema aliamua kuichagua Tanzania  kufadhili  uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto kutokana na kuvutiwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kukabiliana na  vifo vitokanavyo na uzazi.

“Mwaka 2006 niliamua kuwekeza Tanzania kwa kubuni mpango huu wa kuboresha huduma ya dharura ya uzazi  hasa katika maeneo  ambayo hayafikiki na hakuna huduma za afya. Niliamua hivi kwa sababu nilivutiwa sana na juhudi za Rais Kikwete, ni kiongozi makini, imara na  ambaye amekuwa mstari wa mbele katika suala hili, Tanzania inabahati ya kuwa na kiongozi kama huyo” akasisitiza.

Na kuongeza kwamba mpango wake huo ambao amesema ni wa aina yake na wa kwanza kufanyika na  umeanza katika maeneo machache kwa lengo la kuona maendeleo na mafaniko yake  ili baadaye uweze kusambazwa katika maeneo mengine ya nchi.
Naye Dkt. Helen Agerup, yeye amesema ameamua kuugana na Meya Bloomberg kufadhili mpango huo  kutokana  kuvutiwa na  kazi nzuri inayofanywa na Meya na kubwa zaidi baada ya kujionea kwa macho yake kile ambacho kimekuwa kikifanyika nchini Tanzania.

“Nilikwenda Tanzania  mimi na binti yangu na mume wangu, tukajionea kazi nzuri ya  ubunifu huu na namna ilivyoweza kuokoka maisha ya wanawake wajawazito. Tumeamua kuwekeza kwa sababu kile tulichokiona Tanzania kimekidhi malengo ya mfuko wetu, kwa sababu tunahitaji kufanya jambo ambalo matokeo yanapimika,  yanaonekana na yanazaa matunda na haya yote tumeyashuhudia Tanzania”, akabainisha Dkt. Hellen.

Uzinduzi wa mpango huo ulikwenda sambamba na onesho la video fupi iliyoonyesha  kile kilichokuwa kikifanyika nchini Tanzania, kwa maana ya uokoaji wa vifo vya wanawake wajawazito kwa utoaji wa huduma za dharura za upasuaji baada ya waganga na wakunga kupewa mafunzo ya upasuaji wa dharura.

Aidha video hiyo imeonyesha wanawake wakipoteza maisha aidha kutokana na kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua au kupata maambukizo wakati wa kijifungua. Lakini imeonyesha pia jinsi ya wataalamu hao wakitoa huduma hiyo kwa uhodari na uadilifu mkubwa na nyuso zao zikiwa zimejaa faraja hasa baada ya kupewa mafunzo kupitia mpango huo.






Tuesday, October 2, 2012

Press Conference: UN Secretary General, President Kikwete and NYC Mayor Bloomberg unveil results of Innovative Maternal Health Program in Tanzania




H.E. Jakaya Mrisho Kikwete (3rd right), President of the United Republic of Tanzania in a press conference held today in New York to unveil results of Innovative Maternal Health Program in Tanzaina.  Others are the United Nations Secretary General Ban Ki-moon (2nd left), New York City Mayor Bloomberg (left) and Ms. Helen Agerup (2nd right) of the H&B Agerup Foundation and Mr. Martin Nesirky (right), Spokesperson for the Secretary-General, in the Dag Hammarskjöld Library at the United Nations Headquarter in New York, USA.


President Kikwete reading his Statement before members of media.  Listening are UN's Secretary General Ban Ki-moon (center) and New York City Mayor Michael Bloomberg (left).



Tanzania Delegation which consisted of Chief Secretary H.E. Ambassador Ombeni Y. Sefue (5th left), Ambassador Liberata Mulamula, Senior Advisor to President Kikwete, Ambassador Mwanaidi Sinare Maajar (3rd left), Ambassador of the United Republic of Tanzania to the United States of America, H.E. Ambassador Tuvako Manongi (left), Permanent Representative of Tanzaia to the United Nations.  Others are Deputy Ambassador Ramadhan Muombwa Mwinyi (4th left), Deputy Permanent Representative of the United Republic of Tanzania to the United Nations, Mr. Prosper Mbena (6th left), Assistant to President Kikwete and Mr. Salva Rweyemamu, Director of Communications to the Tanzania State House.     



President Kikwete (right), UN's Secretary General Ban Ki-moon (center) listening to New York City Mayor Michael Bloomberg during the press conference.   The Bloomberg Philanthropies have been supporting Tanzania since 2006, with investment of over USD 7.5 million towards projects aim to prevent maternal and newborn deaths.


Ms. Helen Agerup of H&B Agerup Foundation gives her remarks during the press conference which was held today in the Dag Hammarskjöld Library at the United Nations Headquarter in New York, USA.  Bloomberg Philanthropies in collaboration with H&B Agerup Foundation will cost-share the second phase to support Tanzania for a combined commitment of USD 8 million.  The first phase which started since 2006 cost USD 7.5 million where over 9 health centres had been upgraded in Kigoma, Morogoro and Pwani Regions.  The project aims at exploring opportunties to incentivize and promote retention of trained health care workers.   In the photo also is Mr. Martin Nesirky (1st right), Spokesperson for the UN's Secretary-General.



A short video on the work of Bloomberg Philanthropies in Tanzania is playing in the background.


Dr. Peter Mfisi (left) of the President Kikwete's office and Ms. Ellen Maduhu (2nd left), main organizer of the event and Foreign Service Officer at the Tanzania Mission to the United Nations. Others in the photo are official personnels from the Bloomberg Foundation.


A news reporter from CBS Channel of Americans asks few questions to President Kikwete.   Third left is Mr. Modest Jonathan Mero, Minister Plenipotentiary of the Permanent Mission of the United Republic of Tanzania to the UN. 


President Kikwete answering few questions from the reporters (not in the photo).


Ms. Ramla Khamis, Second Secretary in the Ministry of Foreign Affairs and International Co-operation listening to the press conference.



All photos by Tagie Daisy Mwakawago 



President Kikwete, Mr. Ban Ki-moon, Mayor Bloomberg and Ms. Agerup meet to discuss maternal and newborn deaths



President Kikwete (left) in official talks with New York City Mayor Michael Bloomberg.  (This photo is a courtesy of Bloomberg Philanthropies/Jin Lee).


New York City Mayor Michael Bloomberg (right), and Ms. Helen Agerup (center), President of H&B Agerup Foundation, listening to President Jakaya Mrisho Kikwete of Tanzania as talks about the maternal health and newborn deaths in Tanzania. The Bloomberg Philanthropies have supported Tanzania since 2006 and has invested USD 7.5 million toards the project aimed to prevent maternal and newborn deaths.  To this date, there are over 9 upgraded health centres in Kigoma, Morogoro and Pwani Region which have benefited through the Bloomberg Philanthropies project.   (This photo is a courtesy of Bloomberg Philanthropies/Jin Lee).



H.E. Jakaya Mrisho Kikwete (left), President of the United Republic of Tanzania listens Mr. Ban Ki-Moon, Secretary General of the United Nations prior to the press conference of the Maternal Health Program in Tanzania funded by Bloomberg Philanthropies. Second right is Mr. Michael Bloomberg, Mayor of the New York City and Ms. Helen Agerup (2nd left), President of H&B Agerup Foundation.  (Photo by Tagie Daisy Mwakawago of the Ministry of Foreign Affairs and International Co-operation)




President Kikwete explains the much needed training for non-physician clincians in health facilities throughout the regions in Tanzania.   (Photo by Tagie Daisy Mwakawago of the Ministry of Foreign Affairs and International Co-operation)



H.E. Jakaya Mrisho Kikwete (left), President of the United Republic of Tanzania discusses briefly with New York City Mayor Michael Bloomberg (right) about his country's gratitude towards the Bloomberg Philanthropies initiative which resulted in an increase of over 1,000 delivery health facilities in Kigoma, Morogoro and Pwani Regions in Tanzania.  Others in the photo are Ambassador Tuvako Manongi (2nd left), Permanent Representative of the United REpublic of Tanzania to the United Nations and Ms. Helen Agerup (2nd right), President of H&B Agerup Foundation.  (Photo by Tagie Daisy Mwakawago of the Ministry of Foreign Affairs and International Co-operation)



United Nations Secretary General Ban Ki-moon (right), listens to New York City Mayor Michael Bloomberg prior to the press conference of the Maternal Health Program in Tanzania funded by Bloomberg Philanthropies held today in the Dag Hammarskjöld Library at the Nations Headquarters in New York, USA.   (Photo by Tagie Daisy Mwakawago of the Ministry of Foreign Affairs and International Co-operation)



President Kikwete (left), in a group photo with Mr. Michael Bloomberg (2nd right), New York City Mayor, Mr. Ban Ki-moon (right), United Nations Secretary General and Ms. Helen Agerup (2nd left), President of H&B Agerup Foundation.  (Photo by Tagie Daisy Mwakawago of the Ministry of Foreign Affairs and International Co-operation).


Hotuba ya Rais Kikwete ya mwisho wa mwezi Septemba 2012





HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA WANANCHI, TAREHE 30 SEPTEMBA, 2012

Utangulizi

Ndugu wananchi;
Kama ilivyo ada, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana tena leo kupitia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi. Leo nina mambo matatu ninayopenda kuzumgumza nanyi.

TATIZO LA MPAKA WA ZIWA NYASA

Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni kuhusu Ziwa Nyasa.  Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi uliopita nilielezea kuwa katika kushughulikia utata wa mpaka wetu na nchi ya  Malawi katika Ziwa Nyasa, Tume yetu ya pamoja ingekutana tarehe 10 mpaka 15 Septemba, 2012.  Mkutano huo haukufanyika kwa maombi ya ndugu zetu wa Malawi.  Waliomba mkutano huo uahirishwe mpaka watakapotutaarifu.  Tumekubali, hivyo bado tunasubiri.  Wahenga walisema “subira yavuta heri”.  Lakini kwa upande wetu tunaendelea na matayarisho husika iwapo tutaamua kwenda kwenye Mahakama ya Kimataifa (ICJ) huko Uholanzi. 

Mkutano wa AGRA
Ndugu wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mkutano wa AGRA. Tarehe 26 mpaka 28 Septemba, 2012, katika Hoteli ya Ngurdoto nje kidogo ya Jiji la Arusha kulifanyika Mkutano Mkuu wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika, the Alliance for Green Revolution in Afrika kwa Kiingereza.  Kwa kifupi shirika hilo hujulikana kama AGRA.  Huu ulikuwa mkutano wake wa pili, wa kwanza ulifanyika Accra, Ghana, mwaka 2010.

          Narudia kutoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Kofi Annan, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AGRA kwa uamuzi wao wa kufanyia mkutano wao hapa nchini.  Wameitendea nchi yetu jambo jema na kuiletea sifa na heshima kubwa. 

Kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru sana Mheshimiwa Christopher Chiza, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na viongozi, watumishi na watu wote waliohusika kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya maandalizi ya mkutano huu. Vilevile nawashukuru wananchi wenzetu wa Mkoa wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwaangalia vyema wageni wetu.  Mkutano ulikwenda vizuri sana na wageni wameondoka wakiwa wamefurahi na kuridhika.  Nchi yetu imepata heshima kubwa.

Ndugu Wananchi; 
Sina budi kutoa pongezi na shukrani maalum kwa uongozi wa Hoteli ya Ngurdoto kwa kututoa kimasomaso.  Ndugu zetu wa AGRA walitarajia kuwa washiriki wangekuwa 600 ambao wangeenea kwenye ukumbi wa mikutano unaotumika sasa pale hotelini.  Kwa mvuto na heshima ya nchi yetu wakajitokeza watu 1,200, hivyo kukawa na mgogoro wa mahali pa kufanyia mkutano.  Kwa ubunifu wa uongozi wa hoteli mahali palipokidhi mahitaji palipatikana na waandaji na washiriki wakaridhika.  Nawapongeza sana kwa juhudi za ziada walizofanya na kuepusha matatizo ya wingi wa washiriki kugeuka kua kikwazo. 

Ndugu Wananchi;
Shirika la AGRA lilianzishwa mwaka 2006 kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali duniani kwa lengo la kuhimiza na kuleta mapinduzi ya kilimo katika nchi za Afrika.  Shabaha kubwa ni kuliwezesha Bara letu kujitosheleza kwa chakula na kuondoa umaskini unaowakabili watu wengi hasa wale waishio vijijini.  Ni ukweli ulio wazi kuwa kilimo ni sekta muhimu sana barani Afrika.  Kati ya asilimia 70 – 80 ya watu katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo.  Sekta ya kilimo ndicho chanzo kikuu cha ajira kwa watu waishio vijijini.  Kilimo hutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa la nchi nyingi na ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni na malighafi za viwandani.  Kutokana na umuhimu wake huo, kilimo kisipostawi vizuri Barani Afrika hali za watu wengi zinakuwa duni, uchumi wa nchi kudorora na maendeleo yanadumaa.

Ndugu Wananchi;
Juhudi nyingi zimekuwa zinafanyika katika nchi zote za Afrika kuboresha kilimo na mafanikio yanaonekana.  Hata hivyo, bado hali ya maendeleo ya kilimo na wakulima hairidhishi.  Kwa ajili hiyo, juhudi zaidi hazina budi kufanyika.  Hayo ndiyo madhumuni ya AGRA na hivyo ndiyo ilikuwa agenda kuu ya Mkutano wa Arusha wa AGRA, yaani “Kuongeza Uwekezaji na Maarifa ya Kisasa katika Kilimo”.
Kilimo chetu kinategemea mvua ambazo siku hizi haziaminiki sana. Lazima tuongeze uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji.  Wakulima wengi wanatumia jembe la mkono ambalo huleta tija ndogo na mavuno kidogo.  Lazima hatua za makusudi zichukuliwe kuwawezesha wakulima kutumia zana bora na za kisasa za kilimo.  Bado wakulima wengi hawana elimu ya kutosha na hasa ya maarifa ya kilimo bora.  Lazima tuongeze maafisa ugani wa kuwafundisha na kuwaelekeza wakulima maarifa bora na ukulima wa kisasa.  Bado matumizi ya pembejeo za kisasa ni madogo.  Hatuna budi kuongeza uwekezaji na uwezeshaji ili wakulima wapate na kutumia mbegu bora, mbolea na madawa ya kuua wadudu waharibifu na kuzuia maradhi ya mazao ya kilimo. Suala la uwekezaji mdogo katika shughuli za utafiti katika nchi za Afrika nalo lilizungumzwa.  Ilisisitizwa kuwa lazima nchi zetu ziongeze uwekezaji katika utafiti kwani mapinduzi ya kilimo yanaanzia na kuletwa na utafiti unao fanyika ndani ya nchi husika.  Hali kadhalika, suala la kuwepo kwa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima lilisisitizwa.  Hayo mambo mawili ni kichocheo kikubwa kwa wakulima kuongeza uzalishaji na pia kuwawezesha kupunguza umaskini kupitia kilimo. 


Ndugu wananchi;
Katika mkutano wa Arusha tulikubaliana kwa pamoja kuwa bila kuongeza uwekezaji na matumizi ya maarifa mapya katika kilimo chetu, uzalishaji hautaongezeka Afrika. Tatizo la upungufu wa chakula na njaa litaendelea na watu wengi hasa wa vijijini watabakia kuwa maskini.  Hivi sasa watu wapatao 239 milioni Barani Afrika wanaishi bila ya uhakika wa chakula. Hiki kimekuwa chanzo kimojawapo kikubwa cha utapiamlo na vifo vya akina mama wajawazito na watoto katika nchi za Afrika. Pia, ndiyo maana takriban zaidi ya nusu ya watu wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wana kipato cha chini ya dola mbili kwa siku, hivyo wanaishi kwenye umaskini uliopindukia. 

Hali ya umaskini na njaa kwa watu hawa inaweza kubadilika endapo kilimo chao kitafanyiwa mageuzi makubwa na ya haraka:  endapo watawezeshwa kupata na kutumia zana bora za kilimo; iwapo watawezeshwa kutumia mbegu bora, mbolea na madawa ya mimea yao;  na, endapo wakulima  watapewa elimu ya ukulima wa kisasa, huduma za kifedha na masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao yao.  Pia, kama miundombinu muhimu ya umwagiliaji, barabara na umeme vitapatikana kwa uhakika na urahisi kwa wakulima vijijini.

Ndugu Wananchi;
Dhima ya Mkutano wa AGRA wa mwaka huu  inahimiza kuongeza uwekezaji na ubunifu wa kuwezesha mambo yote hayo kupatikana ili kuchochea kasi ya mapinduzi ya kilimo na ukuaji wake.  Katika majadiliano, sote tumeelewana kuwa, kimsingi kufanya hayo ni jukumu la Serikali na wakulima Barani Afrika.  Lakini, kwa kutambua ukweli kuwa Serikali zetu ni za nchi maskini na wakulima walio wengi ni wale wa kujikimu na sehemu kubwa hawana elimu ya kutosha, uwezo wa kufanya hayo peke yao ni mdogo.  Kwa ajili hiyo, wajibu wa sekta binafsi katika nchi za Afrika na jumuiya ya kimataifa hususan Serikali za nchi za Afrika na mashirika ya kimataifa ya kiserikali na yasiyokuwa ya kiserikali ulisisitizwa.  Lengo hapa likiwa ni kuongezea nguvu pale ambapo  nguvu za Serikali na wananchi wa Afrika zimeishia.

Maazimio ya Mkutano
Ndugu Wananchi;
Katika mkutano huo wito ulikuwa kwa wabia wetu wa maendeleo kuchukua hatua za makusudi kuongeza misaada kwa maendeleo ya sekta ya kilimo Afrika.  Misaada hiyo imepungua kutoka dola 18 bilioni miaka 20 iliyopita hadi dola 3 bilioni miaka mitatu iliyopita.  Hivi sasa imepanda kidogo na kuwa dola 6 bilioni, pengine kufuatia kuongezeka kwa kelele za baadhi yetu katika majukwaa ya kimataifa.  Pia, ni kutokana na baadhi ya viongozi katika mataifa kuwa na mtazamo tofauti na wenzao waliotangulia kuhusu kilimo.  Tunaamini kabisa mataifa tajiri na mashirika ya kimataifa yanaweza kuongeza zaidi ya kiasi hicho.  Kinachotakiwa ni kuongeza utashi wa kisiasa ambao tunaaza kuuona kama ilivyodhiria katika Mkutano uliopita wa G8 kule Camp David, Marekani mwezi Mei, 2012.  Tunaamini hivyo kwa sababu miaka 20 iliyopita waliweza kutoa zaidi ya ilivyo sasa.  Pia, kuongezeka kwa watu wanaoamini kuwa kufanya hivyo ni sahihi kiuchumi na kibinadamu.  (It makes economic and humanitarian sense).  Afrika ndilo bara pekee lenye asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kuzalisha chakula duniani ambayo bado haijatumika.  Hivyo mapinduzi ya kilimo yakifanikiwa yataihakikishia dunia chakula cha kutosha kwa watu waliopo sasa na wale bilioni 9 wanaotarajiwa kuwepo mwaka 2050.  Kibinadamu yatawaondolea adha ya njaa na umaskini mamia ya mamilioni ya watu wanaoteseka Barani Afrika. 

Ndugu Wananchi;
Pamoja na kusisitiza wajibu wa mataifa tajiri na mashriika ya kimataifa kuongeza misaada kwa Serikali na wakulima wadogo Afrika, mkutano wa Arusha pia ulitambua nafasi na mchango ambao sekta binafsi inaweza kutoa kwa maendeleo ya kilimo Afrika.  Mkutano ulitoa wito kwa sekta binafsi kujitokeza kuwekeza katika maendeleo ya sekta ya kilimo na kuzitaka Serikali za nchi za Afrika kutengeneza mazingira mazuri yatakayowezesha sekta binafsi kushirikishwa na kushiriki. Ilikuwa jambo la faraja kuona kuwa dhana ya nchi yetu ya kushirikisha sekta binafsi kama ilivyo katika Tamko la Kilimo Kwanza na Mpango wa Kuendeleza Kilimo Katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) vimetambuliwa katika Mkutano wa Arusha kuwa ni mfano bora unaoleta matumaini ya kuleta mapinduzi ya kijani yanayokusudiwa kwa kushirikisha Serikali, wafadhili, wakulima wadogo, sekta binafsi na wadau wengine. 

Ndugu Wananchi;
Katika mkutano huo pia, nafasi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika kutoa mchango muhimu wa kuleta mapinduzi ya kilimo Afrika umetambuliwa.  Mashirika kama vile AGRA, Bill and Melinda Gates Foundation na Rockefeller Foundation ni miongoni mwa mifano halisi.  Mashirika hayo yamekuwa yanatoa mchango wa namna hiyo katika nchi mbalimbali za Afrika pamoja na hapa kwetu Tanzania.

Ndugu Wananchi;
Shirika la AGRA, kwa mfano, tangu kuanza shughuli zake miaka mitatu iliyopita hapa nchini limechangia shilingi 37.2 bilioni kuendeleza shughuli za kilimo.  Hususan yafuatayo yamefanyika au yanafanyika nchini kwa msaada AGRA. Chini ya Programu ya Mbegu AGRA imesaidia gharama za kusomesha wanasayansi 7 wa Digrii ya Uzamivu (Ph.D) na 8 wa Digrii ya Uzamili (MSc).  AGRA imeiwezesha Idara ya Utafiti na Maendeleo ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kufanya kazi na wakulima katika kutafiti na kuchagua aina za mbegu za mazao zenye uwezo mkubwa wa kuzaa na kustahimili wadudu na magonjwa. AGRA pia imechangia kuidhinishwa kwa aina 3 za mbegu za maharage, 16 za muhogo, 4 za mahindi, 1 ya soya na 2 za viazi vitamu.  AGRA vile vile imesaidia kampuni za wazawa zipatazo 10 kuzalisha mbegu zilizohakikiwa na kuzisambaza kwa wakulima na imewezesha kuwapa mafunzo  ya uendeshaji wa shughuli za uwakala mawakala 2,843 katika wilaya 53.

Kupitia Programu ya Kuboresha Afya ya Udongo AGRA inasaidia miradi saba katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini Mashariki na Kanda ya Ziwa.  Programu hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa wakulima wadogo kwa kuongeza matumizi ya mbolea za viwandani na za asili, kuboresha hifadhi ya udongo na maji ardhini na kuweka mazingira wezeshi ya wakulima kufuata mbinu zinazohusika za kutunza rutuba ya udongo,
AGRA pia inasaidia Programu ya Masoko yenye lengo la kuboresha mfumo wa masoko ya mazao ya wakulima wadogo, kupunguza upotevu wa mazao, kuongeza usindikaji na matumizi  mbadala ya mazao na kuboresha mazingira ya biashara ya vyakula vikuu ndani ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki. Programu hii tayari imesaidia miradi minne ya wakulima wadogo kupunguza upotevu wa mazao kutoka asilimia 30 hadi asilimia 15 na kupunguza gharama za biashara ya mpunga/mchele katika wilaya ya Kilombero.

Misaada mingine ya AGRA ilielekezwa katika Programu ya Kuboresha Sera na Mpango wa Ghala la Chakula (Bread basket) ambao unalenga kuongeza uhakika wa chakula na lishe, kuongeza uzalishaji katika kilimo na kuongeza ushindani wa nchi katika uuzaji wa bidhaa za mazao yaliyosindikwa nje ya nchi.  Mpango huu pia unalenga kuboresha upatikanaji wa masoko kwa kuhimiza kilimo cha mkataba, kuimarisha miundombinu na kuboresha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.

Ndugu Wananchi; Shirika la Bill and Melinda Gates Foundation nalo linafanya shughuli kadhaa za kuendeleza kilimo nchini ukiacha kuwa ni mmoja wa wawezeshaji wakubwa wa AGRA.  Miongoni mwa shughuli zinazofanywa nchini kwa msaada wa Mfuko huo ni hizi zifuatazo: Kuongeza uwezo wa utafiti katika baioteknolojia na maradhi ya mihogo na mbegu za mahindi zinazostahilimi ukame; kuongeza ubora wa lishe itokanayo na mihogo na viazi vitamu; kuongeza uzalishaji wa mbegu za mahindi yanayostahimili ukame na maharage yanayozaa sana na kustahimili maradhi, na kuboresha afya ya udongo kwa kushirikiana na AGRA. 

Ndugu Wananchi; Mkutano wa AGRA umemalizika kwa mafanikio makubwa. Nafurahi kuwa tumepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wabia wetu wa maendeleo ya kilimo.  Wote wametuhakikishia utayari wao wa kuendeleza ushirikiano nasi na hata kuongeza zaidi ya ilivyo sasa.  Wito wangu kwa Watanzania wenzangu ni kujipanga vizuri kutumia fursa zilizotokana na mkutano huo kufanyika hapa nchini.

Miaka 20  ya Mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ni kuhusu mfumo wa siasa wa vyama vingi kutimiza miaka ishirini. Mwaka huu nchi yetu imefikisha miaka ishirini tangu ulipoanzishwa Mfumo wa Siasa ya Vyama Vingi nchini, mwaka 1992.  Katika kipindi chote hiki tumeona maendeleo makubwa ya ukomavu wa demokrasia ya vyama vingi unavyozidi kushamiri. Wananchi wa Tanzania wamepata uhuru wa kuanzisha na kujiunga na vyama vya siasa.  Aidha, watu wana uhuru mkubwa zaidi wa kufanya na kushiriki katika shughuli za kisiasa, kufanya maandamano na kuitisha mikutano ya hadhara ya kisiasa, kijamii na mingineyo. Aidha, watu siku hizi wanao uhuru mkubwa wa kutoa maoni yao ama kupitia majukwaa ya mikutano ya siasa au asasi za kiraia ama vyombo vya habari au mitandao ya internet na hata simu za mikononi. 

Utendaji wa Vyama Vya Siasa
Ndugu Wananchi,
Hatua tuliyofikia sasa imetokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya kuleta mageuzi ya kweli ya kupanua demokrasia nchini na kuendeleza haki za binadamu na haki za msingi za raia wa nchi yetu.  Marekebisho kadha ya Katiba na Sheria yamefanyika kwa ajili hiyo.  Mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi ulipoanza kulikuwa na chama kimoja tu cha siasa nacho ni Chama cha Mapinduzi.  Kati ya mwaka huo na mwaka 1995 kulikuwa na vyama 13 vyenye usajili wa kudumu.  Idadi hiyo ya vyama ilibakia hivyo mpaka mwaka 2001.  Ilipofika mwaka 2005 kulikuwa na vyama 18 na mwaka huu 2012 tumefikisha vyama 20 vyenye usajili wa kudumu. Idadi hii ya sasa haijumuishi vyama viwili vya  PONA na TPP ambavyo mwaka 2002 vilifutiwa usajili kwa kushindwa kutimiza masharti yaliyowekwa. 
  
Ndugu Wananchi;
Chini ya mfumo huu mpya, Uchaguzi Mkuu umefanyika mara nne yaani mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010.  Katika chaguzi zote hizo, tumeshuhudia ukomavu mkubwa wa kisiasa, kuvumiliana, ustaarabu wa kuheshimiana pamoja na kuwepo tofauti zetu za mitizamo, itikadi na maoni ya kisiasa.  Watanzania walio wengi, hivi sasa wanaelewa vizuri kwamba mfumo huu wa vyama vingi upo kwa ajili ya kupanua haki za kidemokrasia za raia na kuimarisha utawala bora.  Katu haupo  kuvuruga amani na kuwachonganisha wananchi baina yao wenyewe kwa wenyewe au baina yao na Serikali yao au vyombo vya Serikali. 

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, katika miaka ishirini hii bado zipo changamoto kubwa na ndogo zilizojitokeza.  Baadhi zimepatiwa ufumbuzi na nyingine zinaendelea kushughulikiwa.  Miongoni mwa hayo ni matukio ya uvunjifu wa amani ambayo yameanza kujitokeza kwa kasi katika shughuli za vyama vya siasa katika siku za hivi karibuni. Matukio ya vurugu na hata watu kupoteza maisha yanaelekea kuongezeka.  Japokuwa matukio haya ni machache, lakini yamekuwa na kishindo kikubwa kwani baadhi ya ndugu zetu kadhaa wamepoteza maisha, wengine kupata majeraha ya kudumu  na mali kuharibiwa. 

Ndugu Wananchi;
Siku hizi siyo jambo la ajabu kusikia wafuasi wa chama fulani kufukuzwa au hata kupigwa na kupoteza maisha wanapokwenda kusikiliza mikutano ya hadhara ya Chama kingine kisichokuwa chao.  Jambo hili linastaajabisha kwani mkutano wa hadhara ni wa watu wote si wa wanachama wa Chama kinachofanya huo mkutano peke yao.  Isitoshe shabaha yake ni kuelezea sera za Chama ili kuwashawishi watu wakiunge mkono pamoja na wale ambao ni wanachama wa vyama vingine.  Iweje leo mwanachama wa Chama kingine akihudhuria mkutano huo iwe nongwa na hata kupigwa mpaka apoteze maisha?  Viongozi wenzangu tunataka kuipeleka wapi siasa katika nchi yetu.  Siku hizi taarifa ya malumbano baina ya Polisi na viongozi na wafuasi wa asasi fulani ya kijamii au vyama vya siasa zinaaza kuwa taarifa za kawaida.  Mimi napata hofu na kwa kweli nachelea kwamba huenda vurugu na ubabe vinaweza kugeuka kuwa utamaduni au utaratibu wa kawaida wa kuendesha shughuli za siasa nchini. Hali hiyo inasikitisha sana na kutisha pia. Napenda kuwasihi Watanzania wenzangu na wanasiasa wenzangu kuwa huko tunakoelekea sasa siko, ni kubaya.  Tubadilike ikingali mapema, isije kuwa mazoea yetu.

Ndugu Wananchi; 
Nawaomba sote turejee kwenye misingi mizuri tuliyoanza nayo ya kufanya siasa za kistaarabu.  Tunatofautiana na kukosoana bila kutukanana wala kugombana. Tuendelee   kuvumiliana kwa fofauti zetu za itikadi na mitizamo ya kisiasa bila ya kuchochea chuki baina ya watu na watu au baina ya wafuasi wa vyama tofauti vya siasa au baina ya wananchi na Serikali, au vyombo vya Serikali.  Hayo ni mambo hatari kwa utulivu na ustawi wa nchi yetu. Niwaombe pia viongozi wenzangu na wafuasi wenzangu wa vyama vya siasa tuheshimu sheria za nchi na taratibu za sheria hizo.  Moja ya mambo ambayo yamekuwa yanazua migongano kati ya Polisi na baadhi ya viongozi na wafuasi wa baadhi ya asasi za kijamii na vyama vya siasa inahusu mamlaka ya Polisi kutoa ushauri au hoja pingamizi kwa vikundi vya kijamii au vyama vya siasa kufanya maandamano au mikutano.  Mamlaka hayo yametolewa kwa Polisi kwa nia njema ili kuhakikisha kuwa shughuli za kisiasa zinafanyika katika mazingira ya amani na utulivu bila migongano baina ya makundi au vyama wala bila ya kuathiri shughuli za jamii. 

Ndugu Wananchi;
Mamlaka waliyonayo Polisi hapa nchini hata nchi nyingine duniani iko hivyo hivyo.  Hata hayo mataifa maarufu kidemokrasia duniani hufanya hivyo hivyo.  Hakuna anayefanya mkutano au maandamano bila ya ridhaa ya Polisi.  Aidha, Polisi huelekeza njia za kupita katika maandamano na kuzuia nyingine.  Aidha, huelekeza wapi mikutano ifanyike na wapi isifanyike. Pale wahusika wanapokaidi makubaliano hutokea athari na sote ni mashuhuda wa athari hizo kwa pande zote.   Demokrasia bila ya utaratibu ni fujo.

Ndugu Wananchi;
Madhara yanayosababishwa na matukio haya yangeweza kuepukika endapo taratibu za kushauriana na kuelewana baina ya makundi hayo au vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kabla  ya kufanya mikutano na maandamano zingefuatwa. Narudia kuwasihi wanasiasa wenzangu tuutumie na kuheshimu utaratibu wetu huu mzuri uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zetu. Napenda kusisitiza hata hivyo kwamba pale panapotokea malumbano kati ya Polisi na wafuasi wa kikundi cha kijamii au vyama vya siasa au wananchi, Polisi lazima wahakikishe kuwa hawatumii nguvu kupita kiasi. Wao wenyewe wanatambua vyema maana yake.  Wanapofanya kinyume chake na ikathibitika hivyo nao pia huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Haipendezi mbele ya macho na mioyo ya askari wetu lakini lisilobudi hutendwa.  Imeshafanyika hivyo siku za nyuma na imefanyika hivi karibuni kufuatia tukio la kusikitisha la kuuawa marehemu Daudi Mwangosi, aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Channel 10 kule Nyololo, Mufindi.  Jambo la msingi ninalotaka kusisitiza ni Polisi na kutendewa haki.  Asiwajibishwe asiye husika. 

Hitimisho
Ndugu wananchi,
Nchi yetu imekuwa na amani kwa takriban miongo mitano sasa.  Ni kisiwa cha amani.  Ukweli huu tunauona hapa ndani na wenzetu pia wanaukubali. Wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunaidumisha amani hii.  Msingi mkubwa wa kuhakikisha tunafanya hivyo ni kuheshimu misingi yetu ya Katiba, kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria na tuendelee kuheshimiana na kuvumiliana kwa tofauti zetu. Natoa wito kwa viongozi na wananchi wenzangu tuione tunu hii ya amani tuliyonayo kuwa ni ya kutunzwa kama mboni ya macho yetu.  Tuitunze kwa hali na mali na siyo ya kuibomoa.  Wako wenzetu wanaitafuta hawaipati.  Naomba tuelewe pia kwamba amani ikitupotea si rahisi kuipata.  Na hata ikirudi madhara yake mtaishi nayo miaka mingi au hata kudumu daima.  Ni rahisi sana kubomoa nyumba iliyojengwa kwa siku nyingi kwa uzembe wa siku moja tu, lakini kuijenga upya itachukua muda. 

Watanzania wenzangu hatuna sababu ya kushabikia kauli na matendo ya wenzetu wachache ambao hawaoni umuhimu wa kuendelea kuienzi tunu ya amani tuliyonayo.  Tusione fahari kufanya vitendo vya uvunjaji amani, kutokuheshimu sheria na taratibu tulizojiwekea. Viongozi tunao wajibu wa kuwaongoza watu wanaotuamini na kutusikiliza kwa kutenda mema, kwani hiyo ndiyo dhamana ya uongozi. Tusiwaongoze wafuasi wetu kwenye njia ambazo zitasababisha maangamizi yao na ya wengine wasiohusika. 
Tunayo kazi kubwa ya kulilea taifa letu kuelekea kwenye umoja zaidi, mshikamano zaidi, kupendana zaidi, kuaminiana zaidi na kuheshimiana zaidi.  Tofauti zetu ndiyo sababu na nguzo yetu ya kutaka kushikamana.  Mimi naamini hili ni jambo linalowezekana kama tutasikilizana na kuelewana. Tuzichukue changamoto tulizonazo kama ndiyo daraja la kutuvusha kwenda kwenye ukomavu zaidi wa kidemokrasia.

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu Ibariki Afrika!

Asanteni Sana Kwa Kunisikiliza.
   
         


Viongozi wa Tume ya Mipango na Wizara ya Mambo ya Nje wakutana jijini Dar



Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa John Haule (aliesimama) akiwakaribisha Wajumbe kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa ajili ya kuasilisha mada kuhusu Mfumo wa Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa leo tarehe 02 Oktoba 2012.


Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (aliesimama) akiwasilisha mada katika mkutano wa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Mfumo wa Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo leo tarehe 02 Oktoba 2012.




Naibu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Mhandisi Hapiness Mgalula (Miundombinu na Huduma) aliyesimama kushoto akijitambulisha katika mkutano wa Mfumo wa Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa leo tarehe 02 Oktoba 2012.



Monday, October 1, 2012

Video: Hon. Membe's Speech at the 67th Session of the UN General Assembly


Hon. Bernard K. Membe (MP), Minister for Foreign Affairs and International Co-operation addresses the 67th Session of the United Nations General Assembly on behalf of H.E. Jakaya Mrisho Kikwete, President of the United Republic of Tanzania.


Video of the Speech; click below: