Wednesday, October 3, 2012

VIFO VYA AKINA MAMA HAVIVUMILIKI-JK‏



Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa katika picha ya pamoja na  Bw. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mjini New York, nchini Marekani.  Rais Kikwete alikutana na Bw. Ki-moon kwa ajili ya mazungumzo ya namna kuendeleza ushirikiano, hususan katika masuala ya Mama na Watoto.


Mhe. Rais Kikwete akisaini kitabu cha wageni. 


Mhe. Rais Kikwete (wa tatu kushoto), akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon.  Wengine ni wajumbe kutoka pande zote mbili, Tanzania ikiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Y. Sefue (wa nne kushoto), Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa kwanza kushoto), Afisa Mwandamizi wa Rais Kikwete (masuala ya diplomasia), Mhe. Balozi Tuvako Manongi (wa pili kushoto), Mwakilishi wa Kudumu wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Ndugu Prosper Mbena (wa tano kushoto), Msaidizi wa Rais Kikwete.  Wengineo ni Wajumbe kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon, mara baada ya mazungumzo yao mjini New York.




VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI HAVIKUBALIKI- JK

Na MAURA MWINGIRA, New York
2 Oktoba, 2012
Rais Jakaya Mrisho Kikwete  amesema,  vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo wakati  wakujifungua havipaswi kutokea na havikubaliki.
Na kwa sababu hiyo, anasema juhudi zaidi zinahitajika katika kubabiliana na hali hiyo na hasa ikizingatia kwamba   sababu zinazosabisha kutokea kwa vifo hivyo zinazuilika.

“ Vifo vya wanawake wajawazito havikubaliki” akasema na kuongeza “ na ndiyo kwasababu tunahitaji kuongeza  juhudi zaidi kuokoa maisha ya wanawake, kwa sababu si haki na si jambo jema kwa mwanamke kufa wakati wa kujifungua , si haki afe wakati akimleta kiumbe mwingine duniani, na cha kusikitisha zaidi wanakufa kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika”, akasisitiza Rais Kikwete.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa  awamu ya pili ya mpango wa ubunifu wa uboreshaji wa huduma ya  afya ya mama na mtoto katika maeneo ambayo huduma hiyo haipatikani kwa urahisi nchini Tanzania.

Uzinduzi wa mpango huo umefanyika mbele ya waandishi wa habari siku ya  jumanne  hapa  Makao Uakuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki  Moon, Rais Jakaya kikwete na wafadhili wakuu wa mpango huo ambao ni Meya wa Jiji la New  York  na philanthropist Michael Bloomberg na Dkt. Helen Agerup, Mkuu  wa Mfuko wa  H&B Agerup.

Wafadhili hao wawili wametoa dola za kimarekani  milioni 15 kufadhili huduma za uboreshaji wa vituo vya afya,  na mafunzo ya huduma za upasuaji wa dhararu kwa  waganga,  wakunga na manesi lengo likiwa ni kuokoa maisha ya wanawake wanapojifungua na kupunguza umbali wa  kuifuata huduma hiyo.

Rais Kikwete amesema kwamba, uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto na afya kwa ujumla  ni moja ya vipa umbele  vyake muhimu na ni jambo lililo ndani ya moyo wake.

“Tumefanya mengi na tunaendelea kufanya, lakini tunahitaji kuongeza kasi ya juhudi hizi,  uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto ni kupaumbele changu ni jambo lililo moyoni mwangu na tunapopata wafadhilli kama nyinyi kuchangia juhudi zetu tunafarijika zaidi na kutiwa moyo na tunawashukuru” akasema Rais.

Naye  katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kupigania nakutetea  haki za wanawake na watoto, amesisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi kuokoa maisha ya wanawake na watoto kwa kuboresha huduma zao.

“Tunahitaji marais, mameya, wanaharakatiwa   kuboresha huduma za afya na wafanyakazi wa afya hadi ngazi ya chini kabisa. Leo tunashuhudia matokeo ya ushirikiano huu ambapo kwa ushirikiano wa viongozi watatu tumeweza katika kipindi cha miaka miwili  kupunguza kwa  asilimia kubwa vifo vya wanawake wajawazito katika  maeneo ya mikoa ya Kigoma,  Morogoro na Pwani ambako mpango huu wa ubunifu umekuwa ukitekelezwa” akabainisha Ban ki Moon.

Aidha  Ban Ki Moon amemuelezea  Rais Jakaya kikwete kama  mmoja wa viongozi  wa kwanza duniani kuungua mkono mkakati wa Kimataifa kuhusu Afya ya mama wajawazito na watoto, mpango uliozinduliwa mwaka 2010 ambapo kiasi cha  dola milioni 400 zitaelekezwa katika  uboreshaiji wa huduma hizo. Na ni   mpango unaokwenda sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo  Millenia ( MDGs).

Kwa upande wake Meya na philanthropies Michael Bloomberg  akizungumza  kwenye uzinduzi huo anasema aliamua kuichagua Tanzania  kufadhili  uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto kutokana na kuvutiwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kukabiliana na  vifo vitokanavyo na uzazi.

“Mwaka 2006 niliamua kuwekeza Tanzania kwa kubuni mpango huu wa kuboresha huduma ya dharura ya uzazi  hasa katika maeneo  ambayo hayafikiki na hakuna huduma za afya. Niliamua hivi kwa sababu nilivutiwa sana na juhudi za Rais Kikwete, ni kiongozi makini, imara na  ambaye amekuwa mstari wa mbele katika suala hili, Tanzania inabahati ya kuwa na kiongozi kama huyo” akasisitiza.

Na kuongeza kwamba mpango wake huo ambao amesema ni wa aina yake na wa kwanza kufanyika na  umeanza katika maeneo machache kwa lengo la kuona maendeleo na mafaniko yake  ili baadaye uweze kusambazwa katika maeneo mengine ya nchi.
Naye Dkt. Helen Agerup, yeye amesema ameamua kuugana na Meya Bloomberg kufadhili mpango huo  kutokana  kuvutiwa na  kazi nzuri inayofanywa na Meya na kubwa zaidi baada ya kujionea kwa macho yake kile ambacho kimekuwa kikifanyika nchini Tanzania.

“Nilikwenda Tanzania  mimi na binti yangu na mume wangu, tukajionea kazi nzuri ya  ubunifu huu na namna ilivyoweza kuokoka maisha ya wanawake wajawazito. Tumeamua kuwekeza kwa sababu kile tulichokiona Tanzania kimekidhi malengo ya mfuko wetu, kwa sababu tunahitaji kufanya jambo ambalo matokeo yanapimika,  yanaonekana na yanazaa matunda na haya yote tumeyashuhudia Tanzania”, akabainisha Dkt. Hellen.

Uzinduzi wa mpango huo ulikwenda sambamba na onesho la video fupi iliyoonyesha  kile kilichokuwa kikifanyika nchini Tanzania, kwa maana ya uokoaji wa vifo vya wanawake wajawazito kwa utoaji wa huduma za dharura za upasuaji baada ya waganga na wakunga kupewa mafunzo ya upasuaji wa dharura.

Aidha video hiyo imeonyesha wanawake wakipoteza maisha aidha kutokana na kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua au kupata maambukizo wakati wa kijifungua. Lakini imeonyesha pia jinsi ya wataalamu hao wakitoa huduma hiyo kwa uhodari na uadilifu mkubwa na nyuso zao zikiwa zimejaa faraja hasa baada ya kupewa mafunzo kupitia mpango huo.






No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.