Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amewambia Waandishi wa Habari kuwa Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania katika
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ili iamue mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa
Nyasa unaozozaniwa baina ya nchi hizi mbili.
Mhe. Membe alibainisha hayo mbele ya Waandishi wa Habari
jijini Dar es Slaam siku ya Jumamosi tarehe 06 Oktoba, 2012. “Tanzania ni mjumbe wa ICJ lakini bado
haijatambua Mamlaka ya Mahakama hiyo, hivyo Malawi
haiwezi kuipeleka Tanzania ICJ isipokuwa Tanzania
inaweza kuipeleka Malawi”,
alisema Mhe. Membe.
Mhe. Waziri aliitolea wito Malawi irudi
katika meza ya majadiliano na kuiomba Serikali ya nchi hiyo kutuma wawakilishi katika
kikao walichokubaliana kufanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 07 - 10 Oktoba,
2012. Kikao hicho kinakusudia kupendekeza msuluhishi ambaye atakubalika na pande
zote baada ya kubainika kuwa Tanzania
na Malawi
zenyewe hazitaweza kusuluhisha mzozo huo.
Mhe. Waziri aliwafahamisha waandishi kuwa alipokea
kwa mshtuko taarifa kwamba Malawi
haitashiriki katika kikao kilichopangwa kufanyika Dar es Salaam kwa hoja kuwa
lazima Serikali ya Tanzania
itoe maelezo ya kina kuhusu boti ya kijeshi iliyoonekana kufanya doria kwenye Ziwa
Nyasa ambayo inasemekana kuwaletea hofu kubwa wakazi wa maeneo ya Ziwa kwa
upande wa Malawi.
Aidha, Malawi
inataka kupatiwa maelezo kuhusu toleo jipya la Ramani ya Tanzania lililotolewa na Mamlaka za Tanzania ambayo
inaonyesha mpaka baina ya nchi hizo mbili umepita katikati ya Ziwa Nyasa.
Akitolea ufafanuzi masuala hayo, Mhe. Membe alisema
kuwa toleo hilo jipya lilikuwa na lengo la
kuionyesha Mikoa mipya minne na Wilaya mpya 19 katika ramani ya nchi, na kuonyesha
mpaka kupita katikati ya Ziwa, hilo
si jambo jipya kwani ndivyo ramani ya nchi yetu ilivyokuwa katika matoleo yote
manne yaliyotolewa na Serikali kabla na baada ya uhuru.
Kuhusu boti ya kijeshi kufanya doria kwenye Ziwa
Nyasa, Mhe. Waziri alisema taarifa hizo sio sahihi, ila kinachofanyika ni doria
ya kawaida ambayo inaendeshwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
kuwasaka wavuvi haramu na wale wanaotumia zana za uvuvi zilizopigwa marufuku.
Mhe. Waziri aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali
ya Tanzania
inapenda kuona mgogoro huo unamalizika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne
inayongozwa na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete na kitendo cha Malawi kutishia
kugomea majadiliano hakitarudisha nyuma dhamira ya Serikali.
Alisema Serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa
inakuwa na hoja za kisayansi na kisheria ili ishinde katika mgogoro huo. Moja
ya mikakati ya Serikali imeunda Kamati tatu ambazo zimeshaanza kazi na kazi yao inaendelea vizuri.
Kamati hizo moja inahusika na utafutaji wa nyaraka kuhusu Ziwa Nyasa, ya pili
inahusika na masuala ya kisheria na ya tatu inahusika na masuala ya majadiliano.
Alidokeza kuwa katika kufuatilia kesi
zilizohukumiwa na ICJ hakuna nchi iliyodai umiliki wa ziwa lote au mto uliopo
mpakani baina ya nchi mbili ilishinda kesi. Hivyo, aliwataka Watanzania wasiwe
na wasiwasi kwani Serikali yao
itaibuka mshindi katika mgogoro huo.
Alihitimisha mazungumzo yake kwa kuwataka Wananchi
wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa kufanya shughuli zao kama kawaida pasi na kuhofia
chochote kwani hakuna tishio la vita kabisa baina ya Tanzania
na Malawi.
Habari na Ally Kondo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.