Monday, March 31, 2014

Tanzania: Sports Diplomacy Will Transform Local Athletes



TANZANIA has embarked on sport diplomacy to enable its athletes perform better and bring in medals from international events including the Commonwealth Games set for July, this year in Glasgow, Scotland.

The diplomacy which is meant to enhance capacity building amongst the sportsmen and women will include sending local athletes to other countries and learn new tactics and improve their performance.
Minister for Foreign Affairs and International Relations, Bernard Membe, said that at the moment the country does not have international standard facilities for training its athletes and this has prompted the government to seek assistance from advanced countries.
To start with, the government will send 50 athletes and about 16 coaches abroad to train. A total of ten athletes will train in Ethiopia, ten in New Zealand, ten in China and ten others in Turkey and the government will provide tickets and per diem allowances while the rest of the expenses will be covered by the host countries.
We applaud the government for coming up with this brilliant idea and as Minister Membe said, this is indeed good news for the country's ambitious plan to revive the ailing standard of sports.
Previously, our sportsmen and women were training on facilities that don't meet international standards and this led to their dismal performance in international competitions but now, the government is committed to bring to an end scenario of failure to win medals in big games.
Yes! The embarrassing failure has to end now and the country should retain its old lost glory, especially in such events as Commonwealth Games, where the country has a history of performing well.
Without our sportsmen and women winning in sports competitions, locally and internationally, Tanzania will not be able to make any diplomatic sports impact at home and abroad.
We should remember that sports diplomacy has helped a number of countries in the world in pushing forward their agendas, some of which had absolutely nothing to do with sports.
However, at this juncture, the major focus should remain on helping our athletes step up and improve their career and instil winning mentality. We always believe that good preparations will definitely pay off.

Wednesday, March 26, 2014

Mhe. Membe azungumzia miaka 50 ya Muungano na mafanikio ya Wizara

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard K. Membe (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari, kuhusu Mafanikio ya Wizara kwa kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 katika nyanja mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, ushiriki wa Tanzania kwenye harakati za ukombozi na utatuzi wa migogoro Barani Afrika na Diplomasia ya Michezo .
Waandishi wa Habari waliokuwepo wakati wa mkutano kati yao na Waziri Membe (hayupo pichani).
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa  wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (katikati) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo ya Waziri Membe  na Waandishi wa Habari.
Waziri Membe (Mb) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) huku Naibu wake Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akisikiliza.
Mazungumzo yakiendelea.(Picha na Reginald Kisaka)




WIZARA IMEJIPANGA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI: WAZIRI MEMBE

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sasa imejipanga katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi hususan katika kukuza biashara, kuhamasisha uwekezaji na kuvutia watalii kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Hayo yalisemwa na Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam alipozungumza na Waandishi wa Habari kuwaeleza mafanikio ya Wizara yake yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo maadhimisho yatafikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014.

Mhe. Membe alisema kuwa mara baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 Sera ya Mambo ya Nje ilijikita katika masuala ya ulinzi na usalama na pia ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo viongozi wengi kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika zikiwemo Namibia, Angola, Msumbiji na nyingine walitumia ardhi ya Tanzania katika kupigania uhuru wa mataifa yao.

Aliongeza kuwa, tangu kipindi hicho cha harakati za ukombozi hadi sasa Tanzania imeweka historia duniani katika utatuzi wa migogoro na ulinzi wa amani ambapo imekuwa mstari wa mbele kwenye kuchangia Vikosi vya kulinda amani katika nchi mbalimbali zinazokabiliwa na migogoro ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Comoro, Sudan (Darfur) na Lebanon.

“Katika kudumisha amani, vyombo vyetu vimevuka mipaka kisheria ili kuhakikisha amani inapatikana, hivyo ninatoa pongezi kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi nzuri ya ulinzi wa amani”, alisema Mhe. Membe.

Mhe. Membe aliongeza kuwa, kwa sasa Wizara inakwenda vizuri katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ambapo kwa kushirikiana na Wizara, Idara na Taasisi nyingine imekuwa mstari wa mbele kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara wenye vigezo na sifa ambao wana nia ya kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo gesi. “Wizara inajitahidi kwenda duniani kutafuta wawekezaji, kwani ni kipindi cha kufanya hivyo, na wale wenye sifa na vigezo tunavyovihitaji watachukuliwa”, alisisitiza Mhe. Membe.

Aidha, Mhe. Membe alieleza kuwa, kutokana na hali ya amani na utulivu hapa nchini pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha Sekta ya Uchukuzi, Utalii utaendelea kuongezeka.

Katika hatua nyingine, Mhe. Membe alisema kwamba ili kukuza vipaji vya michezo kwa vijana hapa nchini,  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inahamasisha Diplomasia ya Michezo kwa kuzishirikisha nchi marafiki katika kuchangia sekta hiyo kiufundi, kitaaluma, vifaa na masuala mengine yanayohusu sekta hiyo.

Alifafanua kuwa, kwa sasa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la sehemu za kufanyia mazoezi zenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya kuwawezesha wanamichezo kufanya mazoezi kabla ya kwenda kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa. 

Aidha, aliongeza kuwa kwa jitihada za Wizara nchi nne ambazo ni Uturuki, Ethiopia, China na New Zealand zimekubali kuwapokea wanamichezo 50 na Walimu wao kuanzia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kwa ajili ya kwenda kujifua tayari kwa kushiriki mashindano ya michezo ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Glasgow, Uingereza mwezi Jalai 2014.

“Kutokana na Tanzania kukosa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya mazoezi na ili kuwawezesha vijana wetu kufanya vizuri michezoni, Wizara ilianza kutafuta maeneo nje ya nchi kwa ajili ya mazoezi ambapo tayari nchi za Ethiopia, New Zealand, China na Uturuki zimekubali tupeleke vijana 50 kwa ajili ya mazoezi, nchi tatu kati ya hizo zitapokea vijana kumi kila moja na China itapokea vijana 20”. Alisisitiza Mhe. Membe.

Mhe. Membe alieleza kuwa ana imani mkakati huu utasaidia Tanzania kuanza kupata medali na pia utaamsha ari ya vijana kupenda na kushiriki michezo kikamilifu.

Wakati wa mkutano huo, Mhe. Membe pia alitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo Mgogoro wa Mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi ambapo alisema, baada ya kukutana na Jopo la Usuluhishi chini ya Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chissano hivi karibuni, nchi hizo mbili zimeachwa ziangalie faida na hasara za mpaka kupita katikati au pembezoni mwa Ziwa hilo. Hiki ni kikao cha kwanza cha usuluhishi ambapo pande mbili zilikutana ana kwa ana. Aidha, baada ya uchaguzi mkuu nchini Malawi mwezi Mei mwaka huu, kikao kingine kitapangwa.

Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Rwanda, Mhe. Membe alisema kwamba Tanzania haina ugomvi na Rwanda na kwamba tatizo lililopo ni kutokuaminiana kunakotokana na mashitaka na madai ya uongo yanayotolewa na watu wasiozitakia mema nchi hizi. Hivyo alieleza kuwa Tanzania inaamini katika majadiliano ya amani na diplomasia ili kuweza kutatua tatizo hili.

Vile vile, Mhe. Membe alitumia fursa hiyo pia kuwaasa Watanzania wanaopata fursa ya kusafiri au kuishi nje ya nchi kujiepusha kufanya makosa ya jinai kwa kufuata sheria na taratibu za nchi wanazokwenda. Mhe. Membe aliyasema hayo kufuatia taarifa alizopokea wakati wa ziara yake nchini China hivi karibuni kuhusu vijana wadogo wa kike kutoka Tanzania wanajihusisha na biashara haramu ya ukahaba huko Guangzhou, China.

“Tuna Watanzania wapatao milioni tatu wanaoishi vizuri nje ya nchi, hata hivyo wapo wachache wanaofanya mambo mabaya kama ugaidi, ukahaba na biashara za madawa ya kulevya. Nawaomba sana Watanzania wanapokuwa nje waishi kulingana na sheria na taratibu za nchi hizo ili kujilindia heshima na utu na pia heshima ya nchi yetu”, alisisitiza Mhe. Membe.



-Mwisho-



Matukio mbalimbali ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani nchini

Ndege iliyombeba Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier ikiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Machi, 2014.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) akimpokea Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Mhe. Frank-Walter-Steinmeier alipowasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja nchini. Lengo la ziara ya Waziri Steinmeier lilikuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani hususan katika nyanja za biashara na uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Mhe. Frank-Walter-Steinmeier  akisaini Kitabu cha Wageni alipowasili Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. 
Mhe.Steinmeier akiongea na Wahadhiri, Wanafunzi, Mabalozi na watu mbalimbali ( hawapo pichani) kuhusu ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Ujerumani. Katika mjadala huo Mhe. Steinmeier aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika kwa ujumla. Mhadhara huo ulifanyika katika Ukumbi wa Nkurumah chuoni hapo.
Waziri Membe pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo  Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza Mukandala wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mhe.Steinmeier ( hayupo pichani ).
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb) naye akifuatilia kwa makini hotuba ya Mhe.Steinmeier ambaye hayupo pichani. 
Washiriki mbalimbali waliokuwepo wakati wa Mhadhara uliotolewa na Mhe.Steinmeier (hayupo pichani).  
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu ( kushoto) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi wakifuatilia kwa makini mhadhara uliokuwa ukitolewa na Mhe. Steinmeier ambaye hayupo pichani.
Kaimu Balozi wa Ujerumani hapa nchini Bw. Hans Koeppel (wa kwanza kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Philip Marmo (wa tatu kulia), Balozi  Dora Msechu, (watano kulia) pamoja na Washiriki wengine wakifuatilia Mhadhara uliokuwa ukitolewa na Mhe.Steinmeier (hayupo pichani)
Baadhi ya  Wajumbe waliofuatana na Mhe. Steinmeier (hayupo pichani) 
Picha ya Pamoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianio wa Kimataifa, Bw. John Haule akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Mhe. Steinmeier.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) pamoja na Mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Mhe. Steinmeier walipokuwa wakiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)  
Waziri Membe (Mb) akifafanulia jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani)
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Mhe. Steinmeier. Wakati wa ziara hiyo Mhe Steinmeier alimkabidhi Waziri Nyalandu ndege ndogo kwa ajili ya kukabiliana na uwindaji haramu  wa wanyamapori.
Waziri Membe akiagana na Waziri Steinmeier mara baada ya kumaliza ziara yake nchini. 
Mhe. Steinmeier akiagana na Balozi Philip Marmo.
Mhe. Steinmeier akiagana na Balozi Msechu.
Mhe. Steinmeier akipunga mkono kuaga kabla ya kuondoka nchini.


Picha na Reginald Philip

Tuesday, March 25, 2014

Wizara ya Mambo ya Nje na Ubalozi wa China wafanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule (kushoto) akiwa pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youqing wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari maelezo siku ya Jumanne tarehe 25 Machi, 2014. Mkutano huo ulizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano wa kidiplomasia  kati ya Tanzania na China na mafanikio ya ziara ya Rais wa China aliyoifanya nchini ambayo imetimiza mwaka mmoja.

Sehemu ya waandishi wa habari walioshiriki mkutano wa waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari maelezo. 

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji wa Serikali, Bw. Assah Mwambene wakati wa Mkutano wa Pamoja na waandishi wa habari kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Balozi wa China.

Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bibi Mindi Kasiga akisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikitolewa. wengine ni maafisa wa Ubalozi China.
Baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje walioshiriki mkutano huo. 
Picha ya pamoja, kutoka kulia ni Balozi wa China, Mhe. Lu Youqing; Katibu Mkuu, Bw. John M. Haule; Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Nathaniel D. Kaaya; Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bibi Mindi Kasiga na Afisa kutoka Ubalozi wa China




HOTUBA YA BW. JOHN HAULE, KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA WAKATI WA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI JUU YA MAFANIKIO YA ZIARA YA MHE. XI JINPING, RAIS WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, NCHINI TANZANIA, UKUMBI WA HABARI MAELEZO, DAR ES SALAAM, TAREHE 25 MACHI, 2014


Mheshimiwa Balozi Lu Youqing, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania,

Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

Ndugu waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya umma na binafsi,

Mabibi na Mabwana,

Ni  heshima kubwa na furaha kwangu kujumuika na wenzetu wa Ubalozi wa China katika siku hii ya leo, kwa ajili ya kuelezea mafanikio ambayo Tanzania na China zimepata kutokana na mahusiano ya muda mrefu na ya kidugu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kijamii. Mwaka huu, Tanzania na China zinajivunia kuadhimisha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi hizi mbili. Ikumbukwe kwamba, moja ya vielelezo vikubwa kabisa vya ushirikiano wa nchi hizi mbili ni Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na kwa wale wapenzi wa Soka, ni Uwanja wa Kisasa wa Mpira wenye Uwezo wa Kuchukua Watu elfu sitini (60,000) wakiwa wamekaa.

Kama mnavyofahamu, katika kipindi cha mwaka 2013, Tanzania ilipata bahati ya kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kutembelewa na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China tangu ateuliwe kuwa Rais wa nchi hiyo. Vilevile, kupitia ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Xi Jinping alipata fursa ya kutangaza Sera ya Mambo ya Nje ya China kwa bara la Afrika, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere. Hii inaonesha si tu historia ya uhusiano mzuri na madhubuti uliopo baina ya Tanzania na China, bali pia utayari wa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazotokea hivi sasa duniani kote.

Ziara ya Rais Xi Jinping nchini Tanzania, iliyofanyika mwaka mmoja uliopita ilikuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kidugu ulioanza tangu mwaka elfu moja mia tisa sitini na nne (1964) pamoja na kukuza uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili. Ziara hiyo ilishuhudia kusainiwa kwa Mikataba mbalimbali katika nyanja za kilimo, miundombinu, afya, nishati, utamaduni pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano.

MAFANIKIO YA ZIARA YA MHESHIMIWA RAIS XI JINPING NCHINI TANZANIA

Mahusiano ya watu-kwa-watu kati ya Tanzania na China
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Mahusiano ya watu-na-watu kati ya Tanzania na China ni mazuri na yanazidi kukua siku hadi siku. Tangu kufanyika kwa ziara ya Mhe. Rais Xi Jinping nchini, takwimu ya idadi ya wageni wenye uraia kutoka China waliotembelea Tanzania kwasababu mbalimbali zikiwemo utalii na biashara inakadiriwa kuongezeka kutoka 10,790 mwaka 2013 hadi kufikia takribani 11,555 mwaka 2014. Wakati huohuo, idadi ya Watanzania waliotembelea China inakadiriwa kuongezeka kutoka 7,657 mwaka 2013 hadi kufikia takribani 8,114 mwaka 2014.

Kwa upande mwingine, ziara ya Mhe. Rais Xi Jinping nchini imekuwa chachu kwa viongozi wa ngazi za juu kutoka Serikali ya Tanzania na China kutembeleana kwa nyakati tofauti. Ziara hizo zimeendelea kuwa ishara ya mahusiano mazuri na ya muda mrefu yaliyopo baina ya nchi hizi mbili. Kwa mfano; kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu ujio wa Mhe. Rais Xi Jinping nchini, viongozi mbalimbali wa Kitaifa na wa ngazi za juu wa Tanzania walitembelea China. Viongozi hao ni pamoja na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye alifanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia tarehe 27 Mei hadi 02 Juni, 2013. Wakati wa ziara yake, jumla ya Mikataba minne (4) ya maendeleo katika nyanja za Afya, Bahari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na Mafunzo, iliwekwa saini kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Vilevile, Mhe. Mizengo Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizuru nchini China Mwezi Oktoba, 2013. Kupitia ziara ya Mhe. Waziri Mkuu, Serikali ya China ilitoa ahadi ya kuipatia Tanzania msaada wa fedha kiasi cha Yuan million 200 (sawa na dola za Kimarekani milioni 33) na mkopo wa masharti nafuu wa Yuan milioni 100 (sawa na dola za kimarekani milioni 16). Vilevile, Serikali ya China imekubali kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo katika mpango wa “Matokeo Makubwa Sasa- (BRN)” ambayo Serikali ya Tanzania tayari imekwisha iwasilisha kwa Serikali ya China.

Kufuatia ziara hiyo ya Mhe. Waziri Mkuu nchini China, Mikataba na Makubaliano mbalimbali takriban kumi na miwili (12) iliwekwa saini. Mikataba hiyo inahusu sekta ya nishati na uzalishaji umeme, kuanzisha ukanda maalum wa viwanda kwa lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje, uendelezaji wa sekta ya nyumba na makazi pamoja na ushirikiano wa kitaalamu katika sekta ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wa Serikali ya China, Mhe. Yang Huanning, Naibu Waziri wa Usalama wa Umma wa China alitembelea Tanzania mwezi Mei, 2013. Vyombo vya Usalama vya Tanzania na China vimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha usalama wa nchi hizi mbili hususan kupambana na uhalifu wa kimataifa kama vile biashara za pembe za ndovu, meno ya tembo na madawa ya kulevya.

Madhumuni ya ziara hizo za viongozi hao wa ngazi za juu kutoka Serikali za Tanzania na China yalikuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kidugu uliopo na wa muda mrefu na kuimarisha mahusiano yaliyopo katika nyanja mbalimbali hususan za kiuchumi na biashara.

Mikataba
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Wakati wa ziara ya kihistoria ya Rais Xi Jinping jumla ya Makubaliano na Mikataba kumi na sita (16) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China iliwekwa saini pamoja na misaada mbalimbali kutolewa. Baadhi ya Mikataba na Makubaliano hayo yameanza kutekelezwa; na mingine kufikia hatua nzuri za utekelezaji.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda na wingi wa Makubaliano ambayo nchi hizi mbili ziliafikiana wakati wa ziara ya Rais Xi Jinping, nitatumia sehemu ya muda niliopewa kutoa mifano michache ya mafanikio na matarajio ya utekelezaji wa baadhi ya miradi hiyo ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kuwekwa saini kwa Makubaliano hayo.

Kilimo
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kwa upande wa kilimo, Serikali ya China imefungua milango kwa zao la tumbaku ya Tanzania kuuzwa nchini humo kutokana na utekelezaji wa Mkataba unaohusu Masharti ya Afya ya Mimea kwa majani ya Tumabaku inayotoka Tanzania. Mkataba huo ambao uliwekwa saini wakati wa ziara ya Mhe. Rais Xi nchini unatoa fursa ya soko la Tumbaku ya Tanzania nchini China na hivyo kuchangia katika kuleta urari wa biashara. Hivi sasa, bidhaa za tumbaku zaa Tanzania zinaruhusiwa kuuzwa katika soko la China.

Uwekezaji
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Tanzania na China zimeingia Mikataba mbalimbali kwa lengo la kukuza biashara na kuongeza uwekezaji. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba unaohusu Msaada wa Fedha za Miradi ya Maendeleo nchini Tanzania na ule wa Uimarishaji na Kulinda Uwekezaji.

Utekelezaji wa Mikataba hiyo utasaidia kufikia Malengo yetu ya Dira 2025 kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali iliyopo chini ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011-2016) na Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now). Vilevile, Mkataba wa Kuimarisha na Kulinda Uwekezaji ni mmoja ya Mikataba muhimu ya kiuchumi ambayo inalenga kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji nchini hivyo, hutoa nafasi nzuri ya kukuza na kuvutia uwekezaji kutoka kwa makampuni makubwa ya China.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Tayari Makampuni ya China yameonyesha nia ya kuwekeza katika Sekta ya Nishati nchini. Kampuni ya Nishati ya China {China Power Investment (CPI)} inatarajia kuwekeza katika Mradi wa Kuzalisha MegaWatts 300 za Umeme (300MW) ujulikanao kama Kinyerezi III. Kadhalika, Kampuni nyingine ya Kichina ya Poly Technologies nayo inahusika katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Kinyerezi IV wa 330MW ambazo zinategemea kuongezeka hadi 450MW. Miradi hii ya Kinyerezi kwa kiasi kikubwa itaondoa tatizo la upatikanaji wa Nishati hiyo hapa nchini na hivyo kuwahakikishia wananchi, pamoja na wawekezaji, upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wakati wote na kwa kiwango cha kutosha.

Kampuni ya Poly Technologies pia imeingia Makubaliano na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 200 (USD 200 Million) kwa ajili ya uendelezaji wa sekta ya makazi nchini (real estate development).

Miradi ya Mikopo Nafuu na Misaada
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Katika juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, Tanzania na China zinashirikiana kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji wa nishati ya umeme kupitia gesi; mfano ukiwa ni mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya umeme. Mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, si tu utaiwezesha Tanzania kuzalisha nishati ya umeme ya kutosha kwa matumizi ya ndani pamoja na kuuza nje ya nchi, lakini pia umekuwa ukitoa ajira kwa Watanzania wengi. Mradi huu unatekelezwa sanjari na miradi mingine ya uzalishaji umeme kama ule wa usafirishaji kupitia korido la Kaskazini na Kusini {North East Power Transmission Line (400kV) Dar-Chalinze-Arusha and North West Power Transmission Line (220kV) Nyakanazi-Kigoma-Mpanda-Rukwa-Mbeya} na ya Kinyerezi.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kama mtakavyoona, miradi ambayo Tanzania na China inaitekeleza ina umuhimu mkubwa katika kuchangia maendeleo ya Taifa letu na hivyo kusaidia katika juhudi za Serikali ya Tanzania za kupambana na umasikini. Kwa mfano, Kampuni ya Sichuan Hongda Group ya China inashirikiana na Shirika la Maendelo la Taifa (NDC) kutekeleza Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga. Miradi hiyo yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni Tatu (USD 3 billion), inatarajiwa si tu itachangia katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, bali pia, inatarajiwa kutoa ajira zisizopungua elfu thelathini na tatu (33,000), kuongeza pato la Taifa la fedha za kigeni la Shilingi bilioni 1.73 kwa mwaka pamoja na kusaidia uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya chuma nchini.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Utekelezaji wa Mradi wa Taifa wa Miundombinu ya TEHAMA Awamu ya III umeanza kutekelezwa. Mradi huu wa Taifa unalenga kusambaza miundombinu na kuiunganisha mikoa yote nchini kwa lengo la  kuwawezesha wananchi wa ngazi zote kupata habari za uhakika, za kuaminika na kwa wakati na pia, kupata huduma za TEHAMA kwa gharama nafuu na ufanisi.



Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kadhalika, katika kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata habari za uhakika na kwa wakati, Serikali ya Tanzania na China zilibadilishana Hati kuhusu kulipatia Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) Gari Maalumu la Matangazo ya Runinga (TV Broadcast Truck). Makabidhiano ya gari hilo maalumu yatakayofanyika mwezi ujao (Aprili, 2014), pia yanajumuisha ujio wa timu ya wataalamu kutoka China kwa ajili ya kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya gari hilo la kisasa.

Ni dhahri kuwa, upatikanaji wa habari na huduma za mawasiliano na teknolojia unachangia kujenga jamii yenye maarifa na ufahamu, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Uchukuzi
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kwa upande wa sekta ya uchukuzi, Tanzania na China ziliingia Mkataba wa Ubia kuhusu kuendeleza Bandari na Eneo la Viwanda la Bandari kwenye eneo Maalumu la Uwekezaji la Bagamoyo. Hadi hivi sasa, hatua zilizofikiwa za utekelezaji wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni za kuridhisha. Ni mategemeo yetu kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutakuza uchumi wa nchi kwa kutoa nafasi nyingi za ajira kwa Watanzania katika viwanda hivyo vya uzalishaji na miradi hiyo pia itaimarisha sekta ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa zenye thamani za Tanzania na kuwezesha bidhaa hizo kuingia katika soko la ushindani la biashara nje ya nchi.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kadhalika, katika kukuza ushirikiano wa karibu wa kuimarisha usalama, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea vifaa vya kisasa vya kukagua makontena katika bandari ya Zanzibar. Vifaa hivi vinavyotumia teknolojia ya kisasa vimefika kwa wakati kwani vitasaidia katika kuimarisha usalama wa shughuli za bandari ikiwemo ukaguzi wa mizigo na bidhaa zinazoingia na kutoa kupitia Bandari hiyo. 

Afya
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Katika sekta ya Afya, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya China zimekubaliana kutekeleza mradi wa ukarabati wa hospitali ya Abdullah Mzee ya mjini Pemba.

Katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi huo, hatua mbalimbali zimekwisha chukuliwa zikiwa ni pamoja na; mchakato wa kulipa fidia kwa wakazi wanaoizunguka hospitali hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Utalii
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi, 2013, wakati wa ziara ya Mhe. Rais Xi Jinping nchini, alimkabidhi rasmi Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Kituo hicho cha Mikutano ambacho ni kikubwa kuliko vyote jijini Dar es Salaam,
kimekuwa chachu ya kukuza na kutangaza Utalii wa Mikutano (Conference Tourism) kutokana na uwezo wa kuhudumia Mikutano ya watu zaidi ya elfu moja na mia nane (1,800) kwa wakati mmoja. Kadhalika, kituo hiki kina manufaa ya kiuchumi kutokana na kutoa nafasi za ajira kwa wananchi na kukuza mapato ya mara kwa mara kwa wakazi wa Dar es Salaam kutokana na biashara ya huduma hususan wakati wa Mikutano mikubwa ya kimataifa.

Utamaduni
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kama mnavyofahamu ‘Utamaduni ni Kioo cha Taifa’. Kwa kulitambua hilo, Serikali ya China iko mbioni kujenga kituo cha utamaduni cha Jamhuri ya Watu wa China nchini (Chinese Cultural Centre).

Lengo la kituo hicho ni kukuza utamaduni wa China kwa kujifunza lugha, michezo na sanaa mbalimbali za Kichina. Kadhalika, tayari Serikali ya China imeweza kufungua Taasisi ya Kujifunza lugha ya Kichina (Confucius Institute) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma. Taasisi hizi hudhamini masomo ya lugha ya kichina nchini China na pia, kuhitimu lugha hiyo, huchukuliwa kama kigezo kwa nafasi za ajira katika makampuni ya Kichina yaliyopo Tanzania.

Mahusiano ya kijamii
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Kama nilivyokwisha eleza awali, mahusiano kati yetu na China ni ya kidugu. Hili linadhihirishwa na msaada wa vitu mbalimbali wenye thamani ya Shilingi milioni 30 uliotolewa na Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Wachina kwa waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro mwezi Janauri, 2014.

Hii ni ishara tosha ya kuonyesha kuwa, ushirikiano uliopo na China, haujaishia tu katika ngazi za juu za Serikali, lakini pia katika ngazi za wananchi wa kawaida.

HITIMISHO
Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana,
Ujio wa Rais Xi Jinping nchini, mwaka jana umeimarisha mahusiano kati ya Tanzania na China hususan katika kipindi hiki tunachoelekea katika kilele cha kusherehekea maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Maadhimisho haya ni ishara ya mshikamano wa kirafiki na udugu ulipo kati ya nchi hizi.
Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuwasihi Watanzania kwa ujumla, kutumia vyema fursa za kibiashara na kiuchumi zinazotokana na mahusiano mazuri na ya muda mrefu kati ya nchi zetu.
Tanzania na China zimeazimia kuendelea kufanya juhudi za pamoja kuimarisha ushirikiano wa kirafiki, katika sekta mbalimbali na kuhimiza uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.