==============================
Mhe. Wilson
M. Masilingi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani,
akifuatana na Bw. Paul Mwafongo alihudhuria mkutano na Bw. Louis Rene Peter
Larose, Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya Dunia, Kundi la Nchi za Afrika.
Wengine
waliohudhuria ni pamoja na Bw. Andrew Ndaamunhu Bvumbe, Mkurugenzi Mtendaji
Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, na Bw. WilsonToninga Banda, Mshauri,
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Shabaha ya
Mkutano ilikuwa ni kufuatilia mazungumzo yaliyofanyika Lima, Peru kuhusu
kuimarisha ushirikiano kwa maslahi ya Afrika.
Mhe. Balozi
Masilingi alishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano mzuri uliopo na kwa misaada
na mikopo wanayotoa kuunga mkono juhudi za kujenga uchumi na kufanikisha
mipango ya maendeleo kwa manufaa ya Watanzania wote.
Aidha
aliwahakikishia ushirikiano muda wote atakapokuwa katika kutekeleza wajibu wake
wa kazi kwa maslahi ya Taifa. Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Dunia, Kanda la
Afrika, Bw. Louis Larose, alieleza kwa upande wake kuridhirishwa kwake na
ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Aidha Bw.
Larose aliipongeza Tanzania kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25
Oktoba , 2015 kwamba ulikuwa huru na wa haki. Pia, alimpongeza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John P. Magufuli kwa ushindi na kwa juhudi zake
katika kuangalia udhibiti wa ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuziba mianya
ya uvujaji wa mapatao ili zipatikane fedha kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya
Watanzania.
Mkurugenzi
Mtendaji aliahidi kwamba Benki ya Dunia iko tayari kutoa msaada wowote wa
haraka utakaohitajika na kuombwa na Serikali ya Tanzania ili kufanikisha mpango
wa kukusanya mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza program za maendeleo na
huduma za serikali.
Bw. Larose, alimdokeza Mhe. Balozi kwamba Benki ya Dunia itaandaa
siku maalumu mjini Washington, D.C. kwa ajili ya kuitangaza Tanzania na vivutio
vyake nchini Marekani na kuomba kwamba Benki ya Dunia itamwalika Mhe. Balozi
kuzindua siku hiyo. Akijibu hoja hiyo Mhe. Balozi alikubali mwaliko huo.