Wednesday, December 9, 2015

Wizara ya Mambo ya Nje na Siku ya Uhuru - 9 Desemba 2015

Tangazo la kurasa za Google Swahili mahsusi kwa siku ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Disemba 2015. Kufuatia tamko la Mhe. Rais John Pombe Magufuli la kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Mambo ya nje wameshiriki kwenye zoezi la usafi kwenye maeneo ya makazi yao. Pia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zaohapa wameitikia wito huo na kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam. 

Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa katika zoezi la usafi kwenye uzio wa nyumba yake maeneo ya Mbezi jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Disemba 2015



Nje ya uzio wa nyumba ya Balozi Simba Yahya, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya kufanyiwa usafi kwenye maeneo ya Mbweni jijini Dar es salaam katika kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba 2015.

Balozi Mohammed Juma Maharage, Mkuu wa Itifaki na Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akiwa kwenye zoezi la usafi kwenye gari maalum la "Rapid Deployment Unit" huko nyumbani kwake maeneo ya Makongo Juu, jijini Dar es salaam.


Mhe. Juma Khalfan Mpango, Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kiongozi wa Mabalozi wa wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania naye akiwa kwenye zoezi la usafi nje ya ofisi za ubalozi maeneo ya Upanga jijini Dar es salaam. Usafi huo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru kufuatia maagizo ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Uhuru na Kazi. 


Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa naye akisafisha maeneo ya pembezoni mwa bararabara kuu inayopita nyumbani kwake, Migombani maeneo ya Mikochini jijini Dar es salaam. 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje Bi. Mindi Kasiga akisafisha ngazi za jengo la makazi yake Garden Avenue, jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru tarehe 9 Disemba 2015. 

Jumuiya ya Wachina wanaoishi hapa nchini wakifanya usafi kwenye maeneo yao ya kazi huku bendera ya nchi yako ikipepea ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Disemba 2015.

MHE.BALOZI WILSON M. MASILINGI ATEMBELEA KITENGO CHA VISA KATIKA OFISI ZA UBALOZI WA TANZANIA, WASHINGTON D.C, SIKU YA KUMBUKUMBU YA UHURU, TAREHE 9 DISEMBA, 2015

 Mhe. Balozi Masilingi akisalimiana na Bi. Mariam Mkama, Mtumishi wa Ubalozi, kitengo cha Visa
Mhe. Balozi Wilson M. Masilingi akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Visa na huduma za Uhamiaji na wafanyakazi wa kitengo hicho na watumishi wengine. Kulia ni Bi. Swahiba H. Mndeme, Mkuu wa Utawala na Fedha, Ubalozini.
Mhe. Balozi Wilson M. Masilingi (kulia) akipolewa na Bw. Abass Missana, Mkuu wa Kitengo cha Visa na huduma za Uhamiaji ubalozini hapo.
Mhe. Balozi Masilingi akisalimiana na mmoja wa wateja wa Visa aliyefika Ubalozini kupata huduma hiyo
Mhe. Balozi Masilingi akizungumza na Bw. Arnold NzuaMtemi Nzali wa Las Vegas, Nevada aliyefika Ubalozini kupata huduma ya Pasipoti        
=================================

Katika kutekeleza agizo la Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ubalozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Washington D.C umeendelea kufanya kazi na kutoa huduma za Visa na Pasipoti kama sehemu ya maadhimisho ya sikukuu hiyo. 

 Pamoja na kazi zingine za Ubalozi kuendelea kama kawaida, Mhe. Balozi Wilson M.Masilingi alitembelea kitengo cha Visa na huduma za Uhamiaji na kufanya mazungumzo mafupi na Mkuu wa Kitengo hicho Bw. Abbas A. Missana, Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi, (Minister Plenipotentiary).  Bw. Missana alimweleza Mhe. Balozi kuwa kumekuwa na ongezeko la wageni wanaokuja Ubalozini kuchukua Visa, mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 kumalizika salama. 

Hapo awali, kabla ya uchaguzi idadi ya wageni waliokuwa wanafika Ubalozini kuomba Visa ilipungua kwa kiasi kikubwa.

 Mhe. Balozi aliwapongeza Wafanyakazi wa Ubalozi kwa kuitikia wito wa “Uhuru na Kazi” kwa hamasa kubwa, jambo linalodhihirisha uzalendo na kuheshimu miongozo sahihi toka kwa Mkuu wa Nchi na wasaidizi wake. 

Aidha, aliwataka Watumishi wa Ubalozi kuendelea kuboresha huduma kwa wateja ili kulinda heshima ya nchi yetu.

Wizara ya Mambo ya Nje na Mfuko wa UTT/PID watiliana saini makubaliano ya kuendeleza viwanja vya Balozi za Tanzania nje

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (kulia) wakiweka saini Mkataba wa Hati ya Makubaliano (MoU) na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Umoja Unit Trust (UTT/PID),  Dkt. Gration Kamugisha,  Makubaliano hayo yatatoa fursa kwa Mfuko wa UTT/PID kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje katika kuendeleza viwanja na majengo mengine ya Ofisi za Balozi zilizopo nje ya nchi.  
Balozi Mulamula na Dkt. Kamugisha wakibadilisha Mkataba huo mara baada ya kuweka saini 
Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Mambo ya Nje nao wakishuhudia zoezi hilo la uwekaji saini Kutoka kulia ni Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi wa Sera  na Mipango, Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria na Bw. Gerald Mbwafu, Afisa Mambo ya Nje.
Ujumbe ulioambatana na Dkt. Kamugisha nao wakishuhudia tukio hilo
Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Dkt. Kamugisha
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Liberata Mulamula na Mtendaji Mkuu Dkt. Kamugisha wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi Luvanda (wa tatu kutoka kulia),  Bi. Kasiga (wa kwanza kulia), na Maafisa Mambo ya Nje, Bw. Mbwafu (wa pili kutoka kulia) na Bi. Happy Ruangisa (wa kwanza kushoto) 

Picha na Reginald Philip


========================

TAARIFA YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUSAINIWA KWA HATI YA MAKUBALIANO KATI YA WIZARA NA MFUKO WA UTT/PID

Ndugu wanahabari nimewaita leo ili mshuhudie tukio muhimu la uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mfuko wa Umoja Unit Trust (UTT/PID). 

Makubaliano haya yatatoa fursa kwa Mfuko wa UTT/PID kwa kushirikiana na Wizara yangu kuendeleza viwanja na majengo mengine ya Ofisi zetu za Balozi zilizopo nje ya nchi.

Kama mnavyofahamu, Serikali ina Balozi 35 katika nchi mbalimbali duniani. Tumefanikiwa kuwa na majengo yetu wenyewe kwa ajili ya ofisi na makazi ya maafisa wetu katika Ofisi za Balozi za baadhi ya nchi. Majengo hayo yamejengwa au kununuliwa kwa kutumia fedha za Bajeti ya Maendeleo za Serikali na imesaidia kupunguza mzigo mkubwa kwa Serikali wa kulipa gharama kubwa za kodi ya pango katika nchi hizo.

Ieleweke kwamba, nia ya Wizara ni kuendeleza viwanja na majengo yote yanayomilikiwa na Ofisi za Balozi nje ya nchi.  Hivyo, Wizara imebuni mkakati wa kushirikiana na wabia mbalimbali kuhakikisha kuwa viwanja au majengo yanayomilikiwa na Balozi nje ya nchi vinaendelezwa.

UTT/PID ni mmoja wa washirika aliyeitikia wito wa mkakati huo wa Wizara ambapo baada ya kusainiwa kwa Makubaliano haya, Wizara katika siku chache zijazo itakabidhi kwa UTT/PID ripoti ya viwanja na majengo mengine inayomiliki nje ya nchi ili waainishe maeneo watakayoanza kuyaendeleza kwa kuzingatia kigezo cha fursa za kiuchumi.

Lengo la Wizara kuviendeleza viwanja hivyo, sio tu kupata ofisi na makazi ya kudumu ya maafisa wa Ubalozi bali pia kwa ajili ya vitega uchumi ambapo ofisi za ziada zitapangishwa kwa ajili ya kuingizia mapato Serikali.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
08 Desemba, 2015

Friday, December 4, 2015

Kaimu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje aongoza maadhimisho ya miaka 44 ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)



Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya akitoa hotuba wakati wa maadhimisho ya miaka 44 ya  Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zilizofanyika kwenye Ubalozi wa UAE hapa nchini hivi karibuni. Katika hotuba yake Balozi Yahya alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na UAE ili kujiletea maendeleo.
Sehemu ya Mabalozi na Wageni waalikwa walioshiriki maadhimisho ya miaka 44 ya UAE
Balozi wa UAE hapa nchini, Mhe.Abdulla Ibrahim Alsuwaidi nae akitoa hotuba wakati wa maadhimisho hayo ambapo aliisifu Tanzania kuwa ni nchi inayoshirikiana kwa karibu na UAE katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Abdallah Kilima akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara hiyo, Bi. Mindi Kasiga (katikati) pamoja na wageni wengine waalikwa wakifuatilia hotuba ya Balozi Alsuwaidi (hayupo pichani).
Balozi Yahya kwa pamoja na Balozi Alsuwaidi na Mabalozi wengine wakikata keki kuashiria maadhimisho ya miaka 44 ya UAE
Balozi Yahya na Balozi Alsuwaidi wakimkabidhi tiketi ya ndege ya shirika la Emirates Afisa kutoka Ubalozi wa Msumbiji alipojishindia tiketi hiyo katika droo iliyoendeshwa kusherekea miaka 44 ya uhuru wa UAE
Balozi Yahya nae akifurahia tiketi ya Ndege ya Shirika la ETIHAD baada ya kushinda bahati nasibu katika halfa hiyo. Shirika hilo kutoka UAE limezindua safari zake hapa nchini tarehe 01 Desemba, 2015
Kiongozi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa DRC, Mhe. Juma Halfan Mpango nae akifurahia zawadi aliyojishindia
Mtoto mdogo aliyeshiriki maadhimisho hayo ni mmoja kati ya wale waliojishindia tiketi ya Ndege ya Shirika la ETIHAD

Balozi Kilima akiwa na Bw. Seif Kamtunda, Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia matukio
Afisa Mambo ya Nje, Bw. Hangi Mgaka nae akifuatilia matukio wakati wa maadhimisho ya UAE.

.............Matukio mengine kwenye maadhimisho ya miaka 44 ya UAE


Balozi Abdulla Ibrihim Alsuwaidi akimpokea Balozi Yahya alipowasili Ubalozini hapo kabla ya kuanza maadhimisho ya miaka 44
Balozi Alsuwaidi akimpokea Balozi Abdallah
Balozi Alsuwaidi akimkaribisha Balozi wa Uganda hapa nchini
Balozi Alsuwaidi akimkaribisha Balozi wa Vatican hapa nchini
Bi. Mindi akibadilishana mawazo na mmoja wa wageni waalikwa wakati wa maadhimisho ya miaka 44 ya UAE
Bw. Omar Mjenga (kushoto) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nae akiwa kwenye maadhimisho hayo.
Wageni waalikwa
Bi. Ester Baruti (kulia), Mwakilishi wa Kampuni ya Dangote hapa nchini akishiriki maadhimisho ya UAE
=======================
Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Ujenzi wa Mahakama ya Kimataifa waanza jijini Arusha.



Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Baraka Luvanda (wa pili kulia), Msajili wa MICT Bw. John Hocking (wa pili kushoto) Afisa wa MICT Bw. Bw. Samwel Akorimo (wa kwanza kulia) na Afisa Mambo ya Nje Bw. Elisha Suku (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja. 

Umoja wa Mataifa umeanzisha mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Masalia ya kesi za Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (Mechanism for International Criminal Tribunals (MICT) katika eneo la Lakilaki jijini Arusha.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Baraka Luvanda, kwa niaba ya Wizara hiyo ametembelea mradi huo tarehe 02/12/2015 ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo.

Ujenzi huo unahusisha masijala ya nyaraka mbalimbali za Mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ambayo inahitimisha shughuli zake tarehe 31/12/2015.

Eneo hilo la Lakilaki limetengwa mahsusi kwaajili ya taasisi mbalimbali za kimataifa ambapo mpaka sasa taasisi kama United Nations for International Criminal Tribunal (UNMICT), African Union Advisory Board on Corruption (AUABC), African Institute of International Law (AIIL) na African Court on Human and Peoples' Rights (ACHPR) zinatarajiwa kuwa na ofisi katika jengo hilo.

Pamoja na ziara hiyo, Balozi Luvanda alipata fursa ya kushiriki kwenye uzinduzi wa mnara wa amani (The Arusha Peace Park Monument), tarehe 30/12/2015 mnara ambao  umejengwa  na ICTR kama kumbukumbu ya kudumu kufuatia kuhitimisha shughuli zake jijini Arusha.