Friday, April 29, 2016

Ufunguzi wa Kikao cha 14 cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Rwanda


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda Balozi Jeanine Kambanda akifungua Kikao cha 14 cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Rwanda katika Hoteli ya Lake Kivu Serena tarehe 29 Aprili 2016

Sehemy ya Ujumbe wa Tanzania (kushoto) na Rwanda (kulia) wakifuatilia hotuba za wakuu wa ujumbe wa pande mbili ambapo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa. 

Sehemu ya ujumbe wa Tanzania 





Thursday, April 28, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Kikao cha Mwaka cha Menejimenti ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha UNICEF jijini Dar es Salaam (25 – 29 Aprili 2016)

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amelihakikishia Shirika La Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (The United Nations Children's Emergency Fund-UNICEF) kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na shirika hilo katika harakati zake za kuboresha ustawi, kutetea na kulinda haki za watoto duniani.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha mwaka cha Menejimenti ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha Shirika hilo kilichoanza tarehe 25 Aprili na kinahitimishwa leo kwenye Hoteli ya Ramada.
Dkt. Mahiga alisema kuwa UNICEF ni shirika kubwa linalojulikana duniani kwa mchango wake katika ustawi wa nchi zinazoendelea, hususan katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za kimsingi.

Waziri Mahiga aliendelea kueleza kuwa katika kuhakikisha kuwa watoto wanapatiwa haki zao ipasavyo, hakuna budi UNICEF ikashirikiana na Serikali husika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma harakati hizo. Alizitaja changamoto kubwa kwa ustawi wa watoto  ni pamoja na sera, mifumo ya kisheria, ufinyu wa bajeti na urasimu katika taasisi za Serikali. “Tunakabiliwa na changamoto nyingi katika harakati za kuimarisha ustawi, kutetea na kulinda haki za watoto ambazo ili ziweze kutatuliwa kwa wepesi lazima Serikali, UNICEF na wadau wengine tufanye kazi kwa pamoja”.

Waziri wa Mambo ya Nje aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kuna masuala mengi yanayosababisha matatizo kwa watoto duniani ambayo yanatakiwa yatafutiwe ufumbuzi kwa pamoja. Masuala hayo ni pamoja na usafirishaji haramu wa watoto, biashara haramu ya dawa za kulevya, unyanyasaji dhidi ya wanawake, machafuko ya kisiasa, kushindwa kuwawezesha wanawake na kuwahudumia watoto. Alisema hayo na masuala mengine yanasababisha changamoto kubwa kwa watoto. 

Aidha, Dkt. Mahiga alizungumzia changamoto zinazowakabili watoto wa Tanzania ambazo ni pamoja na mauaji ya watoto, hususan wenye ualbino, kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watoto ambako kunasababisha ukosefu wa ajira, ukatili dhidi ya watoto na ukandamizaji wa haki nyingine za watoto.

Alishauri UNICEF iwe na mikakati mahsusi ya kushughulikia changamoto zinazoikabili nchi husika kwa kushirikiana na taasisi za nchi hiyo. Kwa upande wa Tanzania, alisema kuwa inakabiliwa na changamoto ya mauaji ya watu wenye ualbino na kuongezeka kwa mahitaji katika sekta ya elimu ili kuboresha ubora wa elimu, kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kwa sababu ya Serikali ya awamu ya tano kutangaza elimu ya awali hadi ya sekondari bure.

Dkt. Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa jambo kubwa linalomsumbua ni kuhakikisha kuwa watoto katika kipindi cha ujauzito hadi miaka mitano wanaishi bila kupoteza maisha kutokana na magonjwa na ukosefu wa lishe bora pamoja na kuwalinda hususan katika maeneo ya machafuko.

Ziara ya Waziri wa Nchi wa Viwanda na Biashara wa Singapore, Mhe Dkt. Koh Poh Kun nchini Tanzania tarehe 27 Aprili 2016.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe Dkt. Koh Poh Kun amefanya ziara ya kikazi nchini tarehe 27 Aprili 2016. Pamoja na mambo mengine, Dkt. Koh amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) mjini Dodoma. Katika mazungumzo yao, Dkt. Koh amemhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kwamba makampuni ya Singapore yataendelea kufanya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini. Hadi hivi sasa Makampuni ya Singapore yaliyokwishawekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant) kitakachojengwa kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani. Aidha, kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani Milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa makampuni ya gesi. Dkt. Koh pia alimfahamisha Mhe. Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi (Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo 37,000.  Jiwe la Msingi la Mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage (Mb).

Mbali na ushirikiano katika sekta ya Biashara na Uwekezaji, Dkt. Koh amemfahamisha Mhe Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta. Alisema  Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania. Vilevile, Singapore imeahidi kuandaa mafunzo mahususi kwa ajili ya Makatibu Wakuu wa Tanzania. Mafunzo hayo ya wiki moja yatatumika kubadilishana uzoefu na makatibu wakuu wa Singapore pamoja na Mawaziri. Dkt. Koh alisema Serikali ya Singapore inatoa kipaumbele cha juu katika kuwajengea ujuzi watumishi wa umma kwasababu msingi wa mafanikio ya Taifa lao ni kuwa na rasilimali watu walio na weledi,ujuzi,uzoefu na uadilifu.

Kwa upande wake, Mhe Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada ya kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.

 Ili kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Mhe Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kuanzisha viwanda, hoteli, kilimo na nishati. Aidha, alimuahidi Dkt. Koh kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia na kulinda uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (Bilateral Investment Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru mara mbili (Avoidance of Double Taxation Agreement) ili kuvutia uwekezaji zaidi kati ya mataifa hayo mawili.  

Kuhusu fursa za mafunzo, Mhe Waziri Mkuu ameiomba Serikali ya Singapore itoe fursa zaidi katika mafunzo ya wataalam wa sekta za gesi na uchukuzi.

Awali, Dkt. Koh alifanya mazungumzo na: Mwenyeji wake Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa (Mb), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb).

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,

Dar es Salaam, 28 Aprili, 2016

Friday, April 22, 2016

Taarifa kwa Umma



TAARIFA KWA UMMA

Sekretariati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imetangaza nafasi mbalimbali 16 za ajira kupitia tangazo lao lililotolewa tarehe 16 Aprili, 2016 Kumb. Na. SADC/2/3/3/3 katika tovuti ya http://www.sadc.int

Hata hivyo, kulingana na utaratibu wa “quota points” kwa ajira za Sekretariati, kila nchi mwanachama ana jumla ya pointi 121 ambapo kwa Tanzania tumebakiza pointi 5 tu. Pointi hizi hazitoshi kwa wananchi wetu kufanya maombi ya aina yoyote ya ajira za Sekretariati kwa kipindi hiki.

Pointi zinazohitajika kwa ajili ya kuomba nafasi ya ajira ni kuanzia pointi 12. Kwa sababu hiyo, Tanzania haimo katika orodha ya nchi wanachama ambao wanakidhi vigezo (eligible) kwa wakati huu.

Tunawaomba Watanzania waendelee kutembelea tovuti ya SADC na tovuti ya Wizara kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu fursa zingine zitakazojitokeza. 


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam, 22 Aprili, 2016.

Thursday, April 21, 2016

Wizara ya Mambo ya Nje yafanya mkutano na Vyombo vya Habari

 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)   kuhusu majukumu  na taarifa mbalimbali za utekelezaji za Wizara pamoja na kufafanua taratibu za kiutumishi katika Balozi za Tanzania, sambamba na kuelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara ya wafanyabishara kutoka nchini Oman kwenye mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Afisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Tahir Khamis ambaye alikuwa miongoni mwa waratibu wa ziara ya wafanyabiashara kutoka nchini Oman akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea.
Wakati mkutano ukiendelea

===============================================


Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa imejipanga kuwapeleka kwenye Balozi zake nje Watumishi wapatao 105 na kuwarejesha nchini wengine 79 ambao miongoni mwao muda wao wa utumishi balozini (Tour of Duty) umemalizika na wengine kustaafu kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma. Kwa kawaida tour of duty kwa Watumishi nje ni ya muda wa miaka minne (4).


Tanzania ina Balozi 35 nje ya nchi ambazo kwa ujumla wake zina Watumishi 234. Miongoni mwa Watumishi watakaorejea nchini wamo Mabalozi, Maafisa, Wahasibu na Makatibu Muhtasi.

Hadi sasa Mabalozi waliorejea nchini ni watatu (3) ambao ni Balozi Peter Kalaghe aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na Balozi Batilda Burian aliyekuwa Japan.

Itakumbukwa kuwa, Januari 25, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi hao ambao mikataba yao iliisha na wengine kwa ajili ya kupangiwa majukumu mengine.

Aidha, jumla ya Watumishi tisa  wa kada mbalimbali waliokuwa Balozini wamerejea nchini hadi sasa na wengine wanaendelea kurejea kulingana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo.

Utaratibu wa kuwapeleka na kuwarejesha Watumishi Balozini ni wa kawaida na upo duniani kote kwa mujibu wa sheria za kimataifa ukiwemo Mkataba wa Vienna unaotoa mwongozo kwenye masuala ya kidiplomasia.

Wizara itaendelea kupeleka Watumishi wenye sifa na tija kwa taifa ili kuiwakilisha nchi kikamilifu.

WAKATI HUOHUO, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Oman Mhe. Dkt. Ali Bin Masoud Al Sunaidy alifanya ziara  ya kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 April hadi 14 April, 2016.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni  kushiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Oman, kongamano hili lilikuwa na kauli mbiu ya ‘’ Oman Tanzania Road show : Exploring Opportunities in Investment and Business between Tanzania and Oman’’.

Ziara na kongamano hili  imelenga zaidi katika sekta za Madini, Kilimo na uboreshaji wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Miundombinu na Mawasilisno, Uvuvi, Usafirishaji, Utalii, Petroli na Gesi. Mgeni Rasmi katika kongamano hili alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Katika ziara hii, Mhe. Waziri Al Sunaidy aliongozana na ujumbe wa watu 108 ambapo 12 walikuwa ni Maafisa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali ya Oman na wengine waliobaki kutoka Sekta Binafsi kutoka nchi hiyo kwa lengo la kukutana na Taasisi kama hizo hapa nchini.

Kwa upande wa Tanzania wafanyabiashara 190 walishiriki na wenzao kutoka Oman katika kongamano na baadae katika mikutano ya ana kwa ana (Business to Business meetings).

MAFANIKIO YA ZIARA

1.      Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Oman zilisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce  na Oman Chambers of Commerce wa kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment Company (OTIC). Kampuni imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za Marekani milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji ;

2.      Serikali ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera (Kagera Sugar) na kukipa uwezo wa kuzalisha tani 400,000 ambazo zitauzwa katika soko la Tanzania. Uzalishaji huu pia utahusisha uzalishaji wa Umeme, spiriti na hamira  itokanayo na mabaki katika kuchakata sukari. Umeme utaingizwa katika gridi ya Taifa wakati spiriti ambayo ni muhimu katika matumizi ya tiba itauzwa katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania. Aidha, Oman inahitaji hamira ambayo inahitajika kwa kiasi kikubwa nchini humo na nchi zingine za mashariki ya kati ;

3.      Mbali na uzalishaji wa sukari, Serikali ya Oman pia inakusudia kuingia ubia na Kagera Sugar katika kilimo cha umwagiliaji cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi ya Oman na Tanzania. Utekelezaji wa miradi hii utaleta faida kwa Tanzania ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa sukari na hivyo kupunguza pengo kati ya uzalishaji na mahitaji halisi ya sukari, lakini pia unategemea kuzalisha nafasi zaidi ya 5,000 za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira ;

4.      Serikali ya Oman pia ilionyesha nia yake ya kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika mradi wa uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Tanga lakini pia kuziwezesha bandari za Tanzania kuwa na ushirikiano na zile za Oman ;

5.      Wawekezaji kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za kisasa mkoani Mtwara ili kuondoa tatizo la makazi stahili kwa watendaji wakuu wa makampuni ya mafuta na shughuli zinazoendana na sekta hii ambao hulazimika kila siku kusafiri kwa ndege kutoka Dar Es Salaam kwenda Mtwara na kurudi jambo ambalo lina gharama kubwa pamoja na ombi la hekta 1,000 kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na maua;

6.      Wawekezaji kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika maeneo kadhaa ikiwemo uzalishaji wa mitamba na chakula cha mifugo huko Mivumoni, Tanga, ranchi na machinjio ya Ruvu, miundombinu na viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za kisasa  Kigamboni na Zanzibar pamoja na miradi mingine katika sekta ya utalii  pamoja na kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo ;

7.      Wafanyabiashara wa Tanzania wamepata nafasi ya kutambua fursa zilizopo Oman ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa soko kwa bidhaa za chakula kama vile matunda, nyama, unga, sukari, hamira nk; na

8.      Tanzania kwa ujumla ilinufaika kwa kutangaza fursa za uwekezaji ambazo zipo katika sekta zinazolengwa na wawekezaji wa Oman lakini pia kubaini fursa zilizopo Oman ambazo wafanya biashara wa Tanzania wanaweza kunufaika nazo pamoja na kuwaunganisha wafanya biashara wa Tanzania na wenzao wa Oman katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.

Hivyo, utekelezaji wa matarajio haya unategemea kuongeza ajira, kuongeza ubora na thamani ya mazao ya kilimo na kutanua wigo wa masoko kwa bidhaa za Tanzania na pia kukuza sekta ya viwanda nchini.

Tuesday, April 19, 2016

Serikali ya Brazil kufadhili miradi ya kilimo Mkoani Simiyu

 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka kulia akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Brazil nchini Mhe. Carlos Alfonso Iglesia Puente, mazungumzo ambayo yalifanyika leo katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
 Katika mazungumzo hayo Mhe. Balozi alieleza kuwa Serikali ya Brazil katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania itafadhili miradi ya kilimo katika Mkoa wa Simiyu kwa upande wa Tanzania, mradi ambao utakuwa na gharama ya Dola za Kimarekani milioni tano na lengo la mradi huo ni kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa za kilimo hasa katika zao la Pamba ambalo ndio zao kuu la kilimo Mkoani humo ili kuliongezea thamani
 Mhe. Mtaka katika mazungumzo hayo alipata nafasi ya kueleza fursa nyingine za uwekezaji zinazopatikana katika Mkoa huo ambapo alieleza licha ya kilimo cha pamba shughuli nyingine za kiuchumi ni uvuvi pamoja na  ufugaji ambapo alieleza sehemu kubwa ya wakazi wa Mkoa huo ni wafugaji wa ng'ombe na kwamba kitaifa ni mkoa wa tatu kwa ufugaji wa ng'ombe
Wakati mazungumzo yakiendelea
Wakiagana mara baada ya mazungumzo

Waziri Mahiga akutana na Mjumbe Maalum wa Haki za Binadamu wa Australia

 Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi  Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akimkaribisha Mhe. Philip Ruddock, Mjumbe Maalum wa Haki za Binadamu na Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja ya Bunge nchini Australia, ambaye alimtembelea jana katika Ofisi za Wizara  na kufanya naye mazungumzo.
Waziri Mahiga katika mazungumzo yake alieleza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Australia katika kuhakikisha inazisimamia na kuziwezesha Taasisi za Haki za Binadamu za hapa nchini na kuhakikisha haki hizo zinasimamiwa kikamilifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia nafasi yake ya uenyekiti katika Jumuiya hiyo.
 Mhe. Philip Ruddock naye alieleza nia ya wazi ya Australia kutaka kushirikiana kwa kufanya kazi pamoja na Serikali ya Tanzania katika Taasisi za Haki za Binadamu zilizopo nchini katika kuhakikisha haki za binadamu zinasimamiwa kikamilifu na changamoto zilizopo zinapata ufumbuzi mwafaka.
Ujumbe wa viongozi na Maafisa kutoka Ubalozi wa Australia nchini walioambatana na Mhe. Philip Ruddock wakifuatilia mazungumzo
          Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa,  Bi. Eliet Magogo (kushoto) akiwa na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Ngusekela Nyerere nao wakifuatilia mazungumzo.
Wakiwa katika picha ya pamoja