Thursday, April 28, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Kikao cha Mwaka cha Menejimenti ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha UNICEF jijini Dar es Salaam (25 – 29 Aprili 2016)

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amelihakikishia Shirika La Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (The United Nations Children's Emergency Fund-UNICEF) kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na shirika hilo katika harakati zake za kuboresha ustawi, kutetea na kulinda haki za watoto duniani.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha mwaka cha Menejimenti ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha Shirika hilo kilichoanza tarehe 25 Aprili na kinahitimishwa leo kwenye Hoteli ya Ramada.
Dkt. Mahiga alisema kuwa UNICEF ni shirika kubwa linalojulikana duniani kwa mchango wake katika ustawi wa nchi zinazoendelea, hususan katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za kimsingi.

Waziri Mahiga aliendelea kueleza kuwa katika kuhakikisha kuwa watoto wanapatiwa haki zao ipasavyo, hakuna budi UNICEF ikashirikiana na Serikali husika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma harakati hizo. Alizitaja changamoto kubwa kwa ustawi wa watoto  ni pamoja na sera, mifumo ya kisheria, ufinyu wa bajeti na urasimu katika taasisi za Serikali. “Tunakabiliwa na changamoto nyingi katika harakati za kuimarisha ustawi, kutetea na kulinda haki za watoto ambazo ili ziweze kutatuliwa kwa wepesi lazima Serikali, UNICEF na wadau wengine tufanye kazi kwa pamoja”.

Waziri wa Mambo ya Nje aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kuna masuala mengi yanayosababisha matatizo kwa watoto duniani ambayo yanatakiwa yatafutiwe ufumbuzi kwa pamoja. Masuala hayo ni pamoja na usafirishaji haramu wa watoto, biashara haramu ya dawa za kulevya, unyanyasaji dhidi ya wanawake, machafuko ya kisiasa, kushindwa kuwawezesha wanawake na kuwahudumia watoto. Alisema hayo na masuala mengine yanasababisha changamoto kubwa kwa watoto. 

Aidha, Dkt. Mahiga alizungumzia changamoto zinazowakabili watoto wa Tanzania ambazo ni pamoja na mauaji ya watoto, hususan wenye ualbino, kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watoto ambako kunasababisha ukosefu wa ajira, ukatili dhidi ya watoto na ukandamizaji wa haki nyingine za watoto.

Alishauri UNICEF iwe na mikakati mahsusi ya kushughulikia changamoto zinazoikabili nchi husika kwa kushirikiana na taasisi za nchi hiyo. Kwa upande wa Tanzania, alisema kuwa inakabiliwa na changamoto ya mauaji ya watu wenye ualbino na kuongezeka kwa mahitaji katika sekta ya elimu ili kuboresha ubora wa elimu, kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kwa sababu ya Serikali ya awamu ya tano kutangaza elimu ya awali hadi ya sekondari bure.

Dkt. Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa jambo kubwa linalomsumbua ni kuhakikisha kuwa watoto katika kipindi cha ujauzito hadi miaka mitano wanaishi bila kupoteza maisha kutokana na magonjwa na ukosefu wa lishe bora pamoja na kuwalinda hususan katika maeneo ya machafuko.

Ziara ya Waziri wa Nchi wa Viwanda na Biashara wa Singapore, Mhe Dkt. Koh Poh Kun nchini Tanzania tarehe 27 Aprili 2016.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe Dkt. Koh Poh Kun amefanya ziara ya kikazi nchini tarehe 27 Aprili 2016. Pamoja na mambo mengine, Dkt. Koh amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) mjini Dodoma. Katika mazungumzo yao, Dkt. Koh amemhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kwamba makampuni ya Singapore yataendelea kufanya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini. Hadi hivi sasa Makampuni ya Singapore yaliyokwishawekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant) kitakachojengwa kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani. Aidha, kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani Milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa makampuni ya gesi. Dkt. Koh pia alimfahamisha Mhe. Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi (Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo 37,000.  Jiwe la Msingi la Mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage (Mb).

Mbali na ushirikiano katika sekta ya Biashara na Uwekezaji, Dkt. Koh amemfahamisha Mhe Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta. Alisema  Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania. Vilevile, Singapore imeahidi kuandaa mafunzo mahususi kwa ajili ya Makatibu Wakuu wa Tanzania. Mafunzo hayo ya wiki moja yatatumika kubadilishana uzoefu na makatibu wakuu wa Singapore pamoja na Mawaziri. Dkt. Koh alisema Serikali ya Singapore inatoa kipaumbele cha juu katika kuwajengea ujuzi watumishi wa umma kwasababu msingi wa mafanikio ya Taifa lao ni kuwa na rasilimali watu walio na weledi,ujuzi,uzoefu na uadilifu.

Kwa upande wake, Mhe Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada ya kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.

 Ili kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Mhe Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kuanzisha viwanda, hoteli, kilimo na nishati. Aidha, alimuahidi Dkt. Koh kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia na kulinda uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (Bilateral Investment Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru mara mbili (Avoidance of Double Taxation Agreement) ili kuvutia uwekezaji zaidi kati ya mataifa hayo mawili.  

Kuhusu fursa za mafunzo, Mhe Waziri Mkuu ameiomba Serikali ya Singapore itoe fursa zaidi katika mafunzo ya wataalam wa sekta za gesi na uchukuzi.

Awali, Dkt. Koh alifanya mazungumzo na: Mwenyeji wake Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa (Mb), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb).

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,

Dar es Salaam, 28 Aprili, 2016

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.