Wednesday, April 13, 2016

Makamu wa Rais afungua rasmi Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Oman

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Oman lililofanyika leo kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo la siku mbili litawakutanisha Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman.
Katika hotuba yake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Oman katika masuala ya biashara na uwekezaji pamoja na kudumisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akifuatilia Mkutano wa kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Oman unaoendelea katika Hoteli ya Hyatt Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Abdallah Kilima.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Mhe. Charles Mwijage (kushoto kwa Makamu wa Rais); Waziri wa Biashara na Viwanda wa Oman, Mhe. Dkt. Ali Masoud Al Sunaidy (kushoto kwa Makamu wa Rais) pamoja na baadhi ya Viongozi na watendaji wa Serikali ya Tanzania na Oman. Waliosimama ni baadhi ya Wabunge waliohudhuria mkutano huo.
Mmoja wa wajumbe wa Mkutano akichangia hoja.


Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman wanaokutana jijini Dar es Salaam leo katika kongamano la siku moja, wamehimizwa kufanya majadiliano yatakayoweka misingi na mikakati ya kutumia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana katika nchi zao. 


Hayo yalisemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa anafungua kongamano hilo kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.


Makamu wa Rais alieleza kuwa Oman ina uzoefu, ujuzi, teknolojia na mtaji mkubwa, wakati Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi na nguvu kazi ya kutosha, hivyo nchi hizo zikishirikiana kupitia wafanyabiashara wao, hatua kubwa ya maendeleo itafikiwa kwa muda mfupi kwa faida ya pande zote mbili.

Mhe. Hassan alibainisha kuwa malengo ya Tanzania ni kuwa nchi yenye uchumi wa kati kupitia maendeleo ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Ili kufanikisha malengo hayo, mchango mkubwa wa wafanyabiashara wakiwemo kutoka Oman unahitajika kwa kiasi kikubwa kupitia uwekezaji wao.

Mhe. Makamu wa Rais alihitimisha hotuba yake kwa kupongeza uwekaji saini wa Mkataba wa Kulinda na Kuhimiza Vitega Uchumi (Protection and Promotion of Investments Agreement) kati ya Tanzania na Oman na kusisitiza umuhimu wa kukamilisha uwekaji saini wa Mkataba wa Kuepuka Tozo ya Kodi Mara Mbili (Avoidance of Double Taxation Agreement). Alisema mikataba hiyo itachochea biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Akitoa salamu za ukaribisho katika kongamano hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Charles Mwijage (Mb) aliweka wazi dhamira ya Serikali ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi kupitia maendeleo ya viwanda. Alisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika viwanda ili nchi iweze kuziongezea thamani malighafi zinazozalishwa nchini kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Oman, Dkt. Ali Masoud Al Sunaidy aliongelea ujenzi wa  Bandari ya Bagamoyo utakaofanywa kwa ushirikiano baina ya Mfuko Mkuu wa Akiba wa Oman, Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kupitia Kampuni ya China Merchant International. Alisema mradi huo utakapokamilika utafungua na kuongeza kiwango cha biashara baina ya Tanzania na nchi za Kiarabu na dunia nzima kwa ujumla.

Taasisi mbalimbali zikiwemo TIC, ZIPA, EPZA ziliwasilisha mada katika kongamano hilo ambazo zililenga zaidi vivutio na fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini.
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.