Friday, April 15, 2016

Sudan Kusini Mwanachama rasmi wa EAC baada ya kusaini mkataba


Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akisaini Mkataba wa Kuiwezesha Sudan Kusini kuwa Mwanachama Kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), tukio hilo la kihistoria limefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Tukio hilo limeshuhudiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndungai, Jaji Mkuu Mhe. Chande Othmani, Mwanasheria Mkuu, Mhe. George Masaju na Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Augustine Mahiga    
Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit naye akiweka saini kwenye Mkataba wa Kuiwezesha nchi yake ya Sudan Kusini kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sehemu ya Mabalozi waliohudhuria tukio hilo la kihistoria la Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa mwanachama kamili wa Jamhuri ya Afrika Mashariki mara baada ya kusaini Mkataba wa kuwa Mwanachama wa Jumuhiya hiyo. 
Sehemu nyingine ya Mabalozi wanazoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wa kwanza kushoto ni Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida, Balozi wa Misri nchini Mhe Mohamed Yasser Elshawaf (katikati)
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Susan Kolimba (Mb.), akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Ramadhan Muombwa Mwinyi naye akisalimiana na Rais Kiir.
Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa ,Bw. Hassan Mwamweta akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir alipokuwa akisalimiana na wageni waliohudhuria Tukio hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa nne kutoka kulia) na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir Mayardit (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi Wakuu wa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa nne kutoka kulia) na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao nchini.

===============================
Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit (kulia), akipokea zawadi ya ua kutoka kwa mtoto Sharon Innocent Shiyo wakati wa mapokezi yake rasmi Ikulu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kushoto) akimpokea rasmi Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir Mayardit alipo wasili Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Sudan kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit akiwa pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wakipigiwa nyimbo za mataifa yote mawili.
Kikosi cha Bendi ya Jeshi
Mhe. Salva Kiir akikagua Gwaride la Heshima lililokuwa limeandaliwa kwa ajili yake
Rais Magufuli na Rai Kiir wakifurahia jambo kwa pamoja alipokuwa akimtambulisha Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Augustine Mahiga 
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimtambulisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa Mhe. Susan Kolimba (Mb.) kwa Mhe. Rais Salva Kiir (katikati).
Salva Kiir akiwapungia mkono viongozi mbalimbali walijitokeza kumpokea
========================= 



Waziri Mahiga akiagana na Rais Salva Kiir kabla hajaanza safari ya kurudi Sudan Kusini mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku moja iliyomwezesha kusaini mkataba wa kuingia rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki

Afisa Mambo ya Nje Bi. Olivia Maboko  akiagana na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir alipokuwa akielekea kwenye ndege tayari kwa kuanza safari ya kurudi nchini kwake.
Rais Salva Kiiri akipunga mkono wa kwaheri.
Picha na Reginald Philip

==================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Sudan Kusini yasaini rasmi Mkataba  wa kujiunga Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja na Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini wamesaini Mkataba wa kuiwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tukio hilo la kihistoria limefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2016.

Akizungumza wakati wa haflya hiyo, Mhe. Dkt. Magufuli aliipongeza nchi hiyo na kusema kuwa anajivunia tukio hili la kihistoria kutokea wakati Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba ukurasa mpya wa ushirikiano na mahusiano na nchi hiyo umefunguliwa.

Aliongeza kuwa kihistoria  Sudan Kusini, imekuwa  na mahusiano ya karibu na nchi za Afrika Mashariki katika nyanja mbalimbali ikiwemo mwingiliano wa tamaduni, ushirikiano wa kibiashara na uchumi na ukaribu wa kijografia.  Aidha, alieleza kuwa kujiunga kwa Sudan Kusini kwenye EAC kunaifanya Jumuiya hii kuwa na soko kubwa lenye takriban watu milioni 160.

Vile vile Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa ili Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kuwa na maendeleo endelevu suala la kudumisha amani ni la msingi, hivyo aliwahimiza Sudan Kusini kuendeleza juhudi kwenye mazungumzo ya amani.

‘’Dhana ya Mtangamano ni kukuza biashara, uwekezaji na miundombinu ili kujiletea maendeleo endelevu katika Jumuiya yetu,  hivyo nahimiza  umuhimu wa nchi wanachama kudumisha amani ili kufikia malengo tuliyojiwekea ‘’ alisema Rais Magufuli.

Wakati huohuo, Rais Magufuli alimpongeza Rais Kiir kwa jitihada zake katika kuhakikisha nchi yake inajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki haraka ambapo miezi minne baada ya nchi hiyo kupata uhuru iliwasilisha maombi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka mitano imeweza kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Rais Kiir alieleza kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa na nchi yake ya kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, alimshukuru Rais Magufuli na Marais wa Nchi zote wanachama kwa kuiunga mkono nchi yake kwa kauli moja.

Mhe. Kiir aliongeza kuwa uamuzi wa nchi yake wa kujiunga na Jumuiya ni wa dhati na kwamba una nia ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa ujumla, ambapo nchi yake imeshaanza kufanyia mabadiliko mifumo mbalimbali kwenye Serikali yake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za mtangamano ikiwemo kuunda Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

‘’Hatimaye Sudan Kusini imerudi nyumbani. Jumuiya ya Afrika Mashariki ni sehemu sahihi kwa nchi yangu kwani Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mtangamano unaoheshimika Afrika na Duniani kwa ujumla’’ alisisitiza Rais Kiir.

Pia, Rais Kiir alitangaza kufunguliwa rasmi kwa Ubalozi wa nchi yake hapa nchini na tayari amemteua Balozi Mariano Deng Ngor kuwa Balozi wa Sudan Kusini nchini Tanzania.

Awali akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha wananchi wa Sudan Kusini waliothirika na migogoro na kuikimbia nchi yao wanarejea kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.

Jamhuri ya Sudan Kusini ilipata uhuru wake tarehe 09 Julai, 2011 na iliwasilisha maombi rasmi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 10 Novemba, 2011. Aidha, Tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa  Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha mwezi Machi 2016.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
Dar es Salaam, 15 Aprili, 2016



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.