Thursday, April 14, 2016

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje azungumza na Waandishi wa Habari

Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea Wizarani ikiwemo maandalizi ya ziara ya kikazi ya  Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Salva Mayardit Kiir atakayoifanya nchini tarehe 15 Aprili, 2016. Mkutano huo ulifanyika Jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) tarehe 14 Aprili, 2016.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Miundombinu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Abdilah Mataka akiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa iliyokuwa Wizara ya Afrika Mashariki, Bi. Robi Bwiru wakati wa mkutano wa Wizara na Waandishi wa Habari
Wawakilishi kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara nao wakifuatilia mkutano kati ya Wizara na waandishi wa habari. Kulia ni Bi. Praxeda kutoka Taasisi ya Mpango wa Nchi za Afrika kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) na Bi. Beatha Hyera kutoka Taasisi ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).
Bw. Mataka naye akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala wakati wa mkutano huo.
Mwandishi wa Habari akiuliza swali.
Mkutano ukiendelea. 
=========================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara ya kikazi nchini Rwanda tarehe 06 na 07 Aprili 2016. Ziara hiyo ilianzia wilayani Ngara ambapo kwa kushirikiana na mwenyeji wake, Mhe. Paul Kagame, Rais wa Rwanda walizindua Daraja la Rusumo na Kituo cha Pamoja cha kutoa Huduma Mpakani (OSBP). Baada ya uzinduzi, Waheshimiwa Marais walielekea Kigali ambapo walifanya mazungumzo ya pande mbili katika kijiji cha Muhanzi. 
-Katika mazungumzo hayo Wakuu hao wa Nchi walikubaliana mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
·      - Kudumisha na Kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda;

·    Kuboresha miundombinu katika Ushoroba wa Kati ikiwemo ujenzi wa reli kutoka Tanzania hadi Kigali;

·       Ushirikiano katika sekta ya usafiri wa Anga kati ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na lile la Rwanda (Air Rwanda);

·   Kushirikiana katika usimamizi wa mradi wa umeme wa Rusumo ili kuzalisha Mega Watts 80. Mradi huo utakapokamilika utazifaidisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi; na

·       Kuagiza Mkutano wa Tume yaKudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ufanyike Kigali tarehe 29 na 30 Aprili 2016.

Uzinduzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (One Stop Border Post - OSBP) Tarehe 6 Aprili, 2016
Marais wa Tanzania na Rwanda walizindua Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo.  Tukio hili lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu Serikalini kutoka Tanzania na Rwanda, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.

Ujenzi wa Daraja na Kituo hiki cha Huduma kwa Pamoja Mpakani ni mradi uliotekelezwa kwa msaada kutoka Serikali ya Japan kwa nchi za Tanzania na Rwanda kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA). Mradi huu umegawanyika katika sehemu mbili: 

    i.          Sehemu ya kwanza ni ujenzi wa Daraja la Rusumo linalounganisha nchi  za Tanzania na Rwanda; na

  ii.           Sehemu ya pili ni ujenzi wa majengo na eneo la Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) kwa pande zote mbili za Tanzania na Rwanda.
Kazi zilizotekelezwa katika Mradi huu ni pamoja na:
·       Kujenga daraja lenye urefu wa Mita 80 la njia mbili zenye upana wa mita 3.75;
·       Kujenga sehemu ya wapita kwa miguu yenye upana wa mita 1.5;
·       Kujenga maingilio ya barabara kwa kiwango cha zege la lami lenye unene wa milimita 150 wa mita 7;
·       Kujenga barabara ya kilometa 2 na mabega ya barabara yenye upana wa mita 1.5; na
·       Kujenga Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja mpakani (OSBP).
Mradi huu kwa upande wa Tanzania umegharimu jumla ya Shilingi 33,206,508,072.07 ambapo kati ya fedha hizo Serikali ya Tanzania ilitoa Shilingi 542,385,122.07 kwa ajili ya fidia na uunganishaji wa huduma ya maji na umeme.
Faida
Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani ni kiungo muhimu katika barabara za Ushoroba wa Kati (Central Corridor). Ushoroba wa Kati una mtandao wa barabara unaounganisha barabara kuu ya Dar es Salaam -  Chalinze – Morogoro – Dodoma – Singida – Nzega – Tinde – Isaka – Lusahunga - Rusumo hadi Kigali Nchini Rwanda.
Barabara hii inaunganisha barabara kuu ya kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na kuifanya kuwa kiungo muhimu cha usafiri na usafirishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara kuelekea nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC). Aidha, barabara hii ni sehemu ya mtandao wa barabara mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki zinazoendelea kujengwa.
Kukamilika kwa ujenzi wa Daraja na Kituo hiki cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) Rusumo kutafungua fursa nyingi, ikiwa ni pamoja na:
    i.        Kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa kati ya Jamhuri  ya Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na nchi yetu pamoja na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na COMESA;
  ii.        Kukuza na kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, viwanda na utalii;
iii.        Kuimarisha ushirikiano na kuhamasisha biashara ndani ya nchi na baina ya nchi jirani; na
iv.        Kuwezesha urahisi wa mawasiliano ya kijamii kati ya watu wa Tanzania na Rwanda na Wanaafrika Mashariki kwa ujumla.

Dhana ya Vituo vya Pamoja vya Utoaji Huduma Mipakani

Dhana ya Vituo vya Pamoja vya Utoaji Huduma Mipakani inahusu Nchi zinazopakana kushughulikia huduma na shughuli za udhibiti kama forodha, uhamiaji, usalama na afya kwa kushirikiana. Hivyo, abiria au msafirishaji bidhaa hulazimika kusimama na kukaguliwa au kukamilisha taratibu za udhibiti sehemu moja wakati wa kutoka kwenye nchi moja na kuingia nchi nyingine. Hatua hii inawezesha Idara, Taasisi na Wakala zinazotoa huduma na udhibiti mpakani kufanya kazi kwa pamoja na hivyo kupunguza muda wa kukaa mpakani na kuondoa vikwazo  visivyo vya kiforodha.

Ziara ya Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Tarehe 15 Aprili 2016
Katika hatua nyingine, Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini atafanya ziara ya siku moja nchini Tanzania tarehe 15 Aprili 2016. Rais Kiir anakuja nchini kusaini Mkataba wa kuwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha mwezi Machi 2016.
Sudan Kusini ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuzifaidisha Nchi Wanachama wa EAC ikiwemo Tanzania endapo mipango madhubuti itawekwa kuzichangamkia. Fursa hizo ni pamoja na kibiashara kwa kuwa karibu kila bidhaa inayotumia Sudan Kusini inaagizwa kutoka Nje ya nchi. Sudan Kusini inakabiliwa na uhaba wa chakula, huduma za kibenki, bima na wataalamu mbalimbali. Hivyo, jamii ya wafanyabiashara wa Tanzania wanahimizwa kuchangamkia fursa zinazopatikana nchini humo.

Wakati huo huo,  Serikali imepokea viongozi wa ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali duniani. Viongozi hao ni : 

    i.        Mhe. Dkt. Mario Giro, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia alifanya ziara nchini tarehe 5 – 7 Aprili, 2016. Mhe. Giro aliambatana na Dr. Raffaele De Lutio, Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia. Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo, kuomba kuungwa mkono na Serikali ya Tanzania katika uchaguzi wa nafasi isiyo ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) na kuomba Waziri wa Mambo ya Nje kushiriki katika Mkutano wa Kwanza kati ya Afrika na Italia (First Africa – Italy Conference) utakaofanyika tarehe 18 Mei, 2016;

  ii.        Mhe. Gerd Müller, Waziri wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani alifanya ziara ya kikazi nchini, kuanzia tarehe 30 Machi hadi 1 Aprili, 2016. Katika ziara hiyo, Mhe. Müller aliambatana na viongozi mbalimbali wa Wizara, Wabunge na wawakilishi wa asasi za kiraia. Mhe. Gerd Müller ni Waziri mwenye dhamana ya fedha za misaada na ana ushawishi mkubwa katika kufanya maamuzi kwenye Serikali ya Ujerumani. Serikali ya Ujerumani imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Tanzania inapata fedha kila mwaka kwa ajili ya sekta za kipaumbele ambazo ni maji, afya, viumbe hai (biodiversity) na kukabiliana na ujangili;

iii.        Ujumbe wa Wabunge nane (8) wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Finland ulifanya ziara ya kikazi hapa nchini, kuanzia tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2016. Lengo la ziara hiyo lilikuwa  kuwajengea ufahamu zaidi Wabunge hao kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Finland hapa nchini. Wabunge hao walianza ziara yao kwa kutembelea Mbuga ya wanyama ya Mikumi. Baada ya hapo walielekea mkoani Iringa na kutembelea Chuo Kikuu cha Iringa ambacho ni moja ya vyuo vinavyofaidika na ufadhili wa Serikali ya Finland kupitia mradi wa TANZICT unaolenga kukuza masuala ya ubunifu na ugunduzi kwa kutumia TEHAMA. Kabla ya kuondoka Iringa, Ujumbe huo ulikutana kwa mazungumzo pia na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.

iv.        Mhe. Marián Jurečka, Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Czech amefanya ziara nchini tarehe 12 hadi 13 Aprili, 2014. Katika ziara hiyo Mhe. Jurečka aliambatana na Manaibu Waziri wafuatao:-
·       Mhe. Vladimír Bärtl, Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Czech;
·       Mhe. Jiří JIRSA, Naibu Waziri wa Kilimo (Utawala); 
·       Mhe. Zdeněk Adamec, Naibu Waziri Kilimo  (Uchumi na Teknolojia ya Habari);
·       Mhe. Pavel Sekáč, Naibu Waziri wa Kilimo (Jumuiya ya Ulaya, Sera za Uvuvi) na
·       Mhe. Jiří Šir, Naibu Waziri wa Kilimo (Bidhaa, Utafiti na Ushauri)
Mawaziri hao waliambatana pia na maofisa mbalimbali wa Serikali ya Czech pamoja na wafanyabiashara wamiliki wa makampuni mbalimbali takribani 15. 
Madhumuni ya ziara hii yalikuwa ni kujadiliana masuala mbalimbali ya kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili hususan katika masuala ya kilimo, nishati, uwekezaji, biashara na maendeleo ya viwanda.
Mhe. Marián Jurečka, Waziri wa Kilimo wa Czech alionana na Mhe. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na viongozi wengine wa Wizara hiyo. Katika mkutano wake aliambatana na Manaibu Waziri wake watatu.
Mhe. Vladimír Bärtl, Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Czech alionana na Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Katika mazungumzo hayo ilikubalika kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na ushirikiano kati ya Tanzania na Czech (Economic Cooperation and Bilateral Agreement) rasimu ya Mkataba wa Double Taxation na Investment Protection.
v.Aidha, Mhe. Dkt. Ali Masoud Al Sunaidy, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Oman aliwasili nchini tarehe 12 Aprili 2016 akiongozana na ujumbe wa wafanyabiashara zaidi ya 100 kwa ajili ya kutafuta fursa za biashara na uwekezaji hapa nchini.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam
14 Aprili, 2016





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.