Thursday, September 22, 2016

BAN KI MOON AISIHI TANZANIA ISICHOKE KUZISAIDIA NCHI ZENYE MIGOGORO

Katibu Mkuu Ban Ki Moon alipomkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augutine Mahiga ambaye anamwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na ujumbe wake akiwa katika Mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.    
Ban Ki Moon akimkabidhi kitabu Waziri Mahiga, kitabu ambacho Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anasema kimeandika na kuelezea utekelezaji wa majukumu yake na kwamba ni kitabu kizuri kutumika kama hadidu ya rejea.

********************************************
Na Mwandishi Maalum, New York 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameitaka Tanzania kuendelea na kazi nzuri ya usuluhishi wa migogoro katika baadhi ya nchi za Maziwa Makuu.Ban Ki Moon ametoa wito huo jana ( jumatano) wakati alipokutana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augustine Mahiga, ambaye anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea hapa Jijini New York, Marekani.Katika mazungumzo hayo Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, Tanzania ni kutovu cha Amani, usalama na demokrasia, na kutokana na sifa hizo Tanzania, inapashwa kuendelea na juhudi zake za kuzisaidia nchi zenye migogoro.

Akazitaja nchi hizo kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi na Sudani ya Kusini ambayo ameitaja kuwa ipo katika kipindi kigumu sana. “ Ninawashukuru sana viongozi wa Serikali ya Tanzania kwa kazi nzuri ya utafutaji wa Amani katika nchi zenye matatizo, Sudani ya Kusini ni nchi ambayo inatupa mashaka makubwa. Rais asaidie katika kurejesha hali ya utulivu.Tanzania ni nchi kubwa kwa hiyo bado ninaendelea kuitumainia.” akasisitiza Ban Ki Moon.Vile vile Katibu Mkuu Ban Ki Moon ametoa pia shukrani wa ushiriki wa Tanzania katika operesheni za ulinzi wa Amani na kazi na weledi mkubwa unaoonyeshwa na wanajeshi wa Tanzania.

Akatumia fursa hii kuishukuru Tanzania na viongozi wake kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha yeye kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Na akatoa pole zake kwa serikali na kwa watanzania baada ya kupata taarifa kuhusu tetemeko la ardhi lililosababisha vifo na uharibifu wa mali.

“Naishukuru sana Tanzania, namshukuru Rais Mstaafu Jakaya Kiwete na wewe ( Waziri) na viongozi wengine, mlichangia sana kwangu mimi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ninawashukuru sana sana. ” .Katibu Mkuu Ban Ki Moon anamaliza kipindi chake cha uongozi cha miaka kumi mwishoni wa Mwaka huu.Na tayari mchakato wa upigaji kura wakumtafuta mrithi wake unaendelea katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Kwa upande wake, akiwasilisha salamau za Rais John Pombe Magufuli, Waziri Mahiga amesema. “ Ninawasilisha salamu za Mhe. Rais, alipenda sana kuhudhuria mkutano huu wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa bahati mbaya ilimbidi kuahirisha safari yake kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibu nchini kwetu ”.
Aidha Waziri Mahinga ametumia pia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Katibu Mkuu kwa utekelezaji wa kutukuka wa majukumu yake katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake. 

“Kwa niaba ya serikali ya Tanzania nikupongeza kwa utekeleaji wa majukumu yake. Ulionyesha ushirikiano wa karibu na Tanzania, ushirikiano uliokuwezesha kumteua Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu na msaidizi wako wa karibu. Lakini pia uliniteua mimi kuwa Mjumbe wako Maalum huko Somalia . Tanzania inashukuru kwa haya na mengine” akasema Mahiga. 


Aidha amemwelezea Katibu Mkuu kama kiongozi ambaye aliifanya Afrika kuwa kipaumbele chake, lakini pia aliibeba sana ajenda ya wanawake jambo ambalo amesema limemjenga sifa kubwa.Akizungumzia kuhusu Tanzania kuendelea na juhudi za usuluhishi wa migogoro. Waziri amemhakikisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba, Tanzania na viongozi wake wataendelea na kujukumu hilo.

“Ni kuhakikishie kwamba Serikali yangu itendelea na jukumu hili la usuluhisi. Na kwa upande wa Burundi Tanzania, inaushukuru Umoja wa Mataifa, kwa kutambua na kuamini kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kuushughulikia mgogoro huu. Tanzania ambayo imekabidhiwa jukumu la uwezeshaji wa mazungumzo ya Amani inataka kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa hivyo misaada ya hali na mali kutoka Idara za Umoja wa Matifa ni jambo muhimu”.Amesisitiza Waziri Mahiga. 


Mkurugenzi wa Afrika akutana na Mabalozi wa Afrika nchini kuzungumzia ushirikiano

Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo (kushoto) akizungumza katika kikao na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika hapa nchini. Mazungumzo yao yalijikita katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na nchi zao. Mkutano huo umefanyika katika Hoteli ya Slipway iliyopo Jijini Dar es Salaam  tarehe 22 Septemba, 2016 
Sehemu ya Mabalozi kutoka nchi za Afrika wakiwa kwenye Mkutano wao na Balozi Shelukindo. Kutoka kulia ni Balozi wa Uganda hapa nchini, Mhe. Doroth Samali Hyuha, akifuatiwa na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Yasser El shawaf na Balozi wa Msumbiji, Mhe. Monica Patricio Mussa
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika, Bw. Suleiman Saleh wakati wa mkutano kati ya Wizara na Mabalozi wa Afrika waliopo nchini
Mkutano ukiendelea.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje awapokea madereva waliokuwa wametekwa nchini DRC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuwapokea Madereva kumi (10) waliokuwa wametekwa nchini DRC. Katika maelezo yake Mhe. Kolimba ameishukuru Serikali ya DRC kupitia Ubalozi wake hapa nchini kwa kuonyesha ushirikiano mzuri na kufanikisha kupatikana kwa madereva hao.Kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hapa nchini, Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo. Madereva hao wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam 21 Septemba, 2016.
Balozi wa DRC nchini Tanzania, Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba akizungumza kwenye mkutano na wanahabari, ambapo alitumia fursa hiyo kuwapa pole madereva hao kwa mkasa uliowakuta na alisisitiza suala la kutoa taarifa Ubalozini pindi wanapoanza safari kuelekea nchini Kongo.
Mmiliki wa Kampuni ya Simba Logistics, Bw. Azim Mohamed Dewji akiishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ushirikiano mzuri waliouonyesha mpaka kufanikisha upatikanaji wa Madereva hao.
Sehemu ya Madereva hao wakiwasikiliza viongozi waliojitokeza kuwapokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Mmoja wa Madereva Bw. Athumani Fadhili akisimulia jinsi tukio lilivyotokea mpaka kuokolewa na Vyombo vya usalama nchini Kongo
Naibu Waziri Dkt. Suzan Kolimba, Balozi wa Kongo hapa nchini Mhe. Mutamba Jean Pierne na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Samweli Shelukindo wakiwapokea madereva hao
Naibu Waziri, Dkt. Susan Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na madereva waliokuwa wametekwa nchini Kongo.

Tuesday, September 20, 2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje apokea Nakala za Utambulisho za Balozi Mteule wa Sudan nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Sudan nchini, Mhe.Mahjoub Ahmed Abdallah Sharfi. Tukio hilo lilifanyika Wizarani tarehe 20 Septemba, 2016.
Mhe. Dkt. Kolimba akizungumza na Balozi Sharfi mara baada ya Balozi huyo kuwasilisha Nakala zake za utambulisho
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo akiwa pamoja na Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo kati ya Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Kolimba na Balozi Mteule wa Sudan, Mhe. Sharif (hawapo pichani).


Friday, September 16, 2016

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Uingereza nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Uingereza Mhe. Sarah Cooke na kufanya mazungumzo naye. Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Tukio hilo lilifanyika Wizarani tarehe 16 Septemba, 2016.
Dkt. Mahiga akizungumza na Balozi Mteule wa Uingereza nchini, Mhe. Cooke mara baada ya kupokea Nakala zake.
Balozi Mteule Mhe. Sarah Cooke akizungumza huku Dkt. Mahiga akimsikiliza.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Itifaki Bw. James Bwana (wa kwanza kulia) akielezea jambo kwa Dkt. Mahiga na Balozi Cooke
Mazungumzo yakiendelea.